Sunday, August 25

aina saba za maana kwa mujibu wa leech(1981)

0


Waandishi
Hashim Juma
Habsh Ibrahim
 
Katika makala hii tumeigawa katika sehemu kuu tatu, sehemu ya kwanza ni utangulizi ambapo tumefasili dhana mbalimbali, sehemu ya pili ni kiini  ambapo tutabainisha aina saba za maana kama zinavyopendekezwa na Leech (1981), na mwisho ni hitimisho la makala.

Dhana ya maana ni telezi, hivyo kutokana na utelezi huo wa kufasili dhana ya maana imepelekea kuibuka nadharia mbalimbali zinazoelezea maana.

Mathalani, nadharia mojawapo inayoelezea au inayofasili maana ya maana ni nadharia ya matumizi iliyoasisiwa na mwanafalsafa wa kijerumani Ludwig Wittgenstein (1963): Anayedai kuwa maana ya neno ni matumizi yake katika lugha.
Wittgenstein (keshatajwa), anafafanua kuwa maana ya neno au tungo inapatikana kutokana na muktadha wa matumizi ambayo wahusika wanashirikiana. Kwa mfano tungo “amevaa mitini” maana yake kwa mujibu Kamusi ya TUKI (2014).

 Pia neno hili maana yake kimuktadha ni mtu aliyepotelea pasipojulikana.
Baada ya kuangalia dhana ya maana, vilevile kuna taaluma ijulikanayo kama semantiki inayojihusisha na maana katika lugha.

Richard na wenzake (1985), wakinukuliwa na Habwe na Karanja (2004), wanasema kwamba semantiki ni stadi ya maana.

 Pia, TUKI (1990), wanadai kwamba semantiki ni tawi la isimu linalojishughulikia maana katika lugha. Ukitazama fasili ya TUKI (keshatajwa), utaona kuwa ina mapungufu kwani  inaichukulia semantiki kama tawi la isimu ilhali semantiki inahusiana na matawi mengine nje ya  isimu isimu kama vile falsafa, saikolojia na sosholojia.

Kwa ujumla semantiki ni taaluma inayojihusisha na maana katika lugha.
Aidha, baada ya kuangalia maana ya maana na taaluma inayojihusisha na maana, zifuatazo ni aina saba (7) za maana kama zilivyopendekezwa na Leech (1981) katika kitabu chake cha Semantics: The Study of Meaning.
Maana Msingi, ni maana ambayo inakuwa inarejelea kwenye kamusi. Aidha Resani (2014), anadai kuwa maana msingi ni maana inayowakilishwa na vidahizo katika kamusi.

Maana ya msingi huwiana na maana ya kikamusi na huwa haibadiliki badiliki kufuatana na miktadha mbalimbali.
                                   

                                   Mfano 1.
                                                     –    Mama- mzazi wa kike
                                                     –    Neno la heshima ambalo hutumika kumwita mwanamke.                                              Hii ni kwa mujibu wa Kamusi Pevu ya Kiswahili (2016).

                                   Mfano 2.
Muundo- umbo la kitu, jinsi kilivyoundwa
Jinsi ya utengenezaji wa kitu.
Jinsi ya kazi ya kifahisi ilivyoundwa.
                                   Mfano 3.
Mtini- Mtu asiyejua lolote
Aina ya mti unaozaa tini au matunda ya umbo la duara lenye rangi ya hudhulungi.

Hivyo, ni dhahiri kwamba maana ya msingi hupatikana hasa kwenye kamusi na huwa haibadiliki badiliki katika miktadha mbalimbali.

Maana ya Ziada, hii ni maana ambayo hutegemea uelewa, uzoefu na tajriba ya mtu mmoja mmoja katika kutumia lugha, kuielewa na hata kuichangua. Pia Leech (keshatajwa), anaendelea kusema kuwa aina hii ya maana inatofautiana kulingana na tamaduni, nyakati za kihistoria na tajriba ya mtu binafsi.

Mfano; neno ‘simba’ linaweza kutumika kumuelezea mtu ambaye anatabia zinazofanana na mnyama huyo.
                       Mfano
Mnyama mkubwa wa porini wa jamii ya paka mwenye manyoya ya rangi ya majani makavu na ambaye hula nyama. Kwa mujibu wa Kamusi ya Kiswahili Sanifu. (2014)
Jina, mfano; klabu ya mpira wa miguu.
Sifa, mfano; Juma ni simba.

     
             Aidha neno jingine kama vile ‘Mchepuko’ lina maana kama vile
Tendo la kubadili mwelekeo wa kupita. Kwa mujibu wa Kamusi ya Kiswahili Sanifu. (2014)..
Njia ya muda inayojitokeza pemezoni mwa barabara kuu
Kimada, huyu ni mwanamke wa pembeni asiyekuwa mke halali au ‘hawala’
Hivyo, tunaona kuwa kuna baadhi ya maneno yanamaana zaidi ya ile ya msingi ambazo huibuka kutokana na uelewa na tajriba za watumiaji wa lugha husika.
Maana Hisi, Leech (keshatajwa), anadai kuwa maana hii inazingatia vipengele viwili vya mawasiliano ambavyo vimejigawa kutokana na hali pamoja na mazingira ambapo neno au sentensi ilivyotumika katika lugha. Pia Massamba (2009), anadai kuwa hii ni maana ambayo si ya moja kwa moja, bali inakuwa ni ya kuashiria tu kutokana na hisia na matakwa ya mtu. Vilevile Resani (Keshatajwa), anadai kuwa maana ambayo mtu anakuwa anaelezea hisia binafsi au mtazamo wake juu ya kitu Fulani.
                                     Mfano, “samahani unaweza kupunguza kidogo sauti”? Ina maana kwamba                         sauti hizo zimekera/zimeudhi lakini msemaji ameelezea hisia hizo kwa                     upole. Maana hisi mara nyingi hutegemea kiimbo.
Katika maana hisi tungo ileile inaweza kuwa na maneno tofauti kulingana na kiimbo kilichotumika.
Lakini pia mtu akiwa amechukia hutumia kiimbo cha juu kuonyesha hisia kuwa amekereka/ ameudhika. Mfano, ‘Tokeni nje” hivyo msemaji ameeleza hisia kwa ukali.
Maana Kijamii, hii ni maana ambayo inatokana na lugha inayotumika katika mazingira ya jamii fulani ambapo lugha hiyo inaweza kueleweka na mtu wa ndani wa jamii hiyo.

Aidha lugha hii inakuwa si rahisi kueleweka na watu ambao hawatoki katika jamii hiyo, aidha hutofautiana kulingana na tofauti za kilahaja na mtindo wa mazungumzo. Aidha maana kijamii inafanana na namna mtu anavyolitumia neno katika lugha.
             

                            Mfano neno ‘tembo’ Kiunguja ni ‘mnyama’ lakini Kimakunduchi ni sehemu za                siri za mwanamke.  Pia neno ‘Kinu’ kwa watu wa Kaskazini mwa Tanzania                humaanisha sehemu za siri za mwanamke lakini kwa watu wa pwani ‘Kinu’ ni                kifaa kinachotumika kutwangia nafaka mbalimbali.
                       Kiswahili                          Kikurya
                                       Kula                                 Kura
                                       Mtoto                               Ntoto (wamakonde)
                                       Bibi (Tanzania)                Nyanya (Kenya)
Katika mifano hiyo utaona kwamba maana ya maneno hayo unaweza kuzipata kulingana na jamii husika inayotumia maneno hayo.
Tano, maana akisi, hii ni maana ambayo inaibuka pale neno linapokuwa na maana msingi moja au zaidi ya moja. Maana ya neno moja inazalisha au inapelekea kuibuka kwa maana nyingine. Mara nyingi vikundi vya vijana ndio wanakuwa na maana akisi katika mazungumzo yao.
                           Mfano;
                         Neno; shoga- rafiki wa kike wa mwanamke (kwa mujibu wa Kamusi ya Kiswahili                      sanifu (2014).
                                            –  Mtoto wa kiume mwenye tabia za akina dada kama kama kupiga                                              umbea, tabia ya kupaka manukato ya wakina dada.
                                            –  watu wa jinsia ya moja hususani ya kiume wanaofanya ngono.
                            Chomeka- tia kitu katika kitu kingine (kwa mujibu wa Kamusi ya Kiswahili                                    Sanifu (2004).                                
                                       
                             Papa- Samaki mkubwa wa baharini asiye na miiba mwenye ngozi nene ya                                kijivu. Kwa mujibu wa Kamusi ya Kiswahili Sanifu (2014).
                                        -sehemu ya uzazi wa mwanamke.
                           Weka- tua kitu mahali.
                                     – Kitendo cha kumuunganishia mwanaume kimapenzi na jinsia ya kike.
Hivyo, katika mifano hiyo utaona kwamba pindi maneno hayo yanapotumika katika mazungumzo huweza kuibua maana nyingine, pia maneno haya yanapotumika huakisi maana nyingine miongoni mwa wazungumzaji.
Maana Ambatani, hii ni ile maana ambayo inatokana na uhusiano wa neno na neno ambapo zinatokana na tabia au mazoea ya utokeaji wa pamoja wa maneno hayo. Aidha katika maana hii maneno sharti yaendane na mitazamo ya jamii.
                          Mfano:
Bibi kizee- Shaibu (katika neno hilo neno ‘shaibu’ haliendani na Bibi kizee, hivyo hapo ilipaswa iwe ‘ajuza’)
Saa yeyote- saa yoyote (katika mfano huu neno ‘yeyote’ mara nyingi hutumika kwenye nomino hisivu, hivyo kutumia neno ‘yeyote’ kwenye neno saa si sahihi kwani inabidi litumike neno ‘yoyote’).
Kudamshi- mwanaume (neno kudamshi hutumika kumwambia mwanamke au jinsi ya kike kuwa amependeza, hivyo neno kudamshi linaendana na jinsi ya kike.
Hivyo, kutokana na mifano hiyo ni dhahiri kuwa maneno katika lugha huweza kuambatana na kutokana na uambatano huo ndio hutusaidia kuweza kupata maana fulani.
Maana Kidhima, ni ile ambayo kile kinachozungumzwa na msemaji au mwandishi katika kupangilia ujumbe wake kwa kuzingatia mtiririko, lengo na msisitizo katika kufikisha ujumbe. Pia maana kidhima inaweza kuelezwa kwa kutumia mkazo na kiimbo kuonyesha msisitizo katika sehemu mojawapo ya sentensi. Pia katika Kiswahili msisitizo wa jambo au sentensi mara nyingi huwa ni mwanzoni mwa tungo.
                          Mfano.
Mwalimu aliwapa wanafunzi zawadi – katika tungo hii msisitizo upo kwenye neno ‘zawadi’.
Wanafunzi walipewa zawadi na mwalimu – msisitizo upo kwenye neno ‘wanafunzi’.
Zawadi ilitolewa na mwalimu kwenda kwa wanafunzi – msisitizo upo kwenye neno ‘zawadi’.
Kesho nitakuja kukutembelea – hapa ujumbe upo kwenye neno ‘kesho’.
Nitakuja kukutembelea kesho – msisitizo upo kwenye neno ‘nitakuja’
Hivyo katika mifano hiyo utaona kwamba, maneno flani huweza kubebea uumbe au dhamira juu ya kile anachokisema mzungumzaji.
Kwa ujumla, baada ya kuzitazama aina saba za maana kwa mujibu wa Leech (1981), Tunaweza kusema kuwa Leech (keshatajwa), amewasaidia watumiaji wa Lugha katika kutofautisha maana kwani katika kila aina ya maana ameonyesha ni kwa namna gani neno moja linaweza kuwa na maana zaidi ya moja kimuktadha. Pia licha ya kuwasaidia watumiaji lugha, tumebaini kuwa kuna udhaifu katika uainishaji wake wa maana kwani amegawa aina nyingi za maana ambazo zingeweza kuainishwa kwa kutumia aina kuu mbili tu za maana ambazo ni maana msingi na maana ziada, ambapo katika maana ya ziada ndipo tunapata: Maana Akisi, Maana Kijamii, Maana Ambatani, Maana Kidhima na Maana Hisi.
                         

                                                             

                                                                   MAREJELEO
Habwe. J na Karanja P. (2004). Misingi ya Sarufi ya Kiswahili. Nairobi: Phoenix Publishers Ltd.
Leech. G. (1981). Semantic- A Study of Meaning. London: Penguin
Massamba. D. P. B. (2009). Kamusi ya Isimu na Falsafa ya Lugha. Dar es Salaam: TUKI
Resani. M. (2014). Semantiki na Pramatiki ya Kiswahili. Dar es Salaam: Karljamer Print Technology.
TUKI (2014). Kamusi ya Kiswahili sanifu. Nairobi: Oxford University Press.
Wamitila, K.W. (2016). Kamusi Pevu ya Kiswahili. Nairobi: Vide Muwa.

Share.

About Author

Leave A Reply