Sunday, August 25

Yanga imepewa mbinu kuwaangamiza waethiopia

0


Mchambuzi wa soka ambaye pia ni mchezaji wa zamani wa Yanga na timu ya taifa ya Tanzania Ally Mayay ametoa ushauri kwa klabu yake ya zamani (Yanga) kuhakikisha inapata taarifa za kutosha kuhusu wapinzani wao Wolaitta Dicha kabla ya mchezo wao wa play off kufuzu hatua ya makundi kombe la shirikisho Afrika.

“Hata kama ni timu mpya kwenye michuano hii lakini kuwatoa tu Zamalek kunatosha kuwapa kujiamini vya kutosha na kuonesha kwamba wana uwezo.”

“Kuwafunga Zamalek 2-1 pale Ethiopia halafu kufungwa 2-1 ugenini Misri na kwenda hatua ya penati ni kiashiria tosha kwamba hii timu ina uwezo ingawa ni mara yake ya kwanza kushiriki michuano ya kimataifa na kufika hatua hii. Tayari inawapa kujiamini akilini mwao wanafikiri kama wameweza kuitoa Zamalek timu yoyote watakayokutana nayo wanaweza kuitoa.”

“Kwa hiyo haitakuwa kazi rahisi kwa Yanga kama ambavyo watu wengi wanafikiria kuwa uzoefu walionao Yanga katika michuano hii ukilinganisha na wa Wolaitta lakini wao watakuwa wanajiamini zaidi kuliko Yanga.”

“Kikubwa ni kupata taarifa zao za kutosha kwa sababu ni timu ngeni na watu wengi wanazijua Coffee, St. George lakini hawa Wolaitta  ni timu ngeni hivyo Yanga wanahitaji kujua ubora wao na udhaifu uko wapi.”

“Timu zetu zote (Simba na Yanga) ziliondolewa kwenye mashindano kwa sababu wapinzani wao walikuwa wana taarifa zao za kutosha ndio maana waliweza kuwadhibiti John Bocco, Emanuel Okwi hata Ajib.”

“Jambo jingine ni kujipanga kwa ajili ya mechi ya nhumbani kwa sababu mara nyingi tumekuwa tukianzia nyumbani kwa hiyo kikubwa ni kuhakikisha mechi ya kwanza wanapata matokeo ili mechi ya marudiano isiwe mzigo mzito bali iwe ni kulinda matokeo yaliyopatikana kwenye mechi ya kwanza.”Read More

Share.

About Author

Comments are closed.