Saturday, August 24

Safari ya soka la Thomas Mourice tangu ‘day one’ hadi leo anatangaza rasmi kustaafu

0


Leo Jumamosi Machi 24, 2018 wakongwe wawili wa soka la Tanzania Thomas Mourice na Amri Kiemba watasema bye bye kwa mashabiki wa soka la ushindani, mchezo maalum wa kuwaaga mashabiki wao utachezwa uwanja wa Bandari, Temeke huku kila mchezaji akisindikizwa na ma-star waliotamba na wanaotamba kwenye soka la Bongo.

Inawezekana unamfaham vizuri Thomas Mourice na mambo yake aliyokuwa anayafanya wakati akitamba uwanjani lakini hufahamu historia yake alitokea wapi, alipopita hadi kuamua kutundika daruga.

Baada ya kusoma andiko hili, utapata kumfahamu Tom mwanzo mwisho kama vile umewahi kuishi nae nyumba moja.

Tom ni mchezaji ambaye alianzia chini, alianza kucheza soka katika timu za mitaani lakini baadae akaendelea kucheza alipokuwa Makongo Secondary School, baada ya Makongo akajiunga na Cargo ya Dar ambapo ndipo alicheza ligi kwa mara ya kwanza ikiwa ni ligi daraja la kwanza.

Cargo ilikuwa inautumia uwanja wa Bandari kama uwanja wao wa mazoezi wakiwa ligi daraja la kwanza uwanja ambao Thomas Mourice atacheza mechi ya kuwaaga mashabiki.

Baada ya kutoka Cargo alienda kucheza ligi kuu baada ya kusajiliwa na Kariakoo-Lindi mwaka 2002 wakati timu hiyo ikiwa na Said Mwamba ‘Kizota’ (marehemu), Rajabu Msoma (marehemu), Banza Chikala ambao walikuwa tayari ni wazoefu lakini Mourice aliingia kama kijana.

Alipotoka Kariakoo-Lindi alichukuliwa na George Lucas akapelekwa Uganda kufanya majaribio kwenye kalbu ya Sports Club Villa lakini kwa bahati mbaya hakufanikiwa kwa sababu tayari kulikuwa na wachezaji wazoefu na yeye alikuwa bado kijana akakutana na changamoto nyingi.

Kama zali vile, wakati akifanya majaribio Villa kuna jamaa wa Rwanda alikuwa anafuatilia mazoezi akamuelewa Tom na kuona ana kitu cha ziada akamchukua usiku kwa sababu Villa baada ya kuona kuna mtu anataka kuchukua baadhi ya wachezaji ambao wao walikuwa hawawahitaji wakaanza kujaribu kuweka vikwazo. Kwa hiyo ilibidi wasafiri usiku kwa kutumia gari ndogo (Land Rover) kwenda Rwanda akiwa Tom pamoja na baadhi ya wachezaji wa Uganda.

Akafanya mazoezi na APR ambao walimuelewa na kuona atawasaidia wakamsainisha mkataba, lakini Tom alikaa APR kwa msimu mmoja tu baadae alivyorudi Bongo mwaka 2004 akakutana na ofa ya Miembeni ya Zanzibar akaona kurudi Rwanda ‘miyeyusho’ kwa sababu anachokitafuta anaweza kukipata akiwa hapahapa nyumbani akaamua kusaini Mienbeni kwenda kucheza ligi ya Zanzibar.

Akiwa Zanzibar alichaguliwa kwenye timu ya taifa ya Zanzibar kikosi ambacho kilienda Ujerumani kwa ajili ya maandalizi ya mashindano lakini pia wakafanya ziara kitu ambacho ataelendelea kuwashukuru watu wa Zanzibar kwa heshima waliyompa. Tom hajawahi kucheza timu ya taifa ya Tanzania bara, alicheza timu ya taifa ya vijana ya U17 wakati akiwa anasoma Makongo.

Tom anakutana na ‘mchizi’ wake wa kitambo

Baada ya kutoka Miembeni ndipo akasajiliwa na Yanga mbapo alikutana na swahiba wake Amri Kiemba ambaye walicheza pamoja enzi zao wakisoma pale Makongo kwa hiyo hawa jamaa walitoka shule pamoja halafu wakakutana tena kwenye timu moja kwa hiyo urafiki wao uliendela, baada ya kutoka Yanga waliungana pamoja kwenda Miembeni lakini picha halikuishia hapo wakarudi bara pamoja na kucheza Moro United.

Kiemba na Tom waliachana Moro United baada ya Kiemba kwenda Simba lakini Tom pia aliondoka Moro United akaenda kucheza MajiMaji ambako hakukaa sana akahamia Mtibwa na kukaa kwa misimu miwili ikatokea nafasi ya kwenda kucheza Kenya akatimka zake kuelekea Bandari ya Mombasa ambako alikutana na akina Meshack Abel, David Naftali na Mohamed Banka. Timu ilikuwa daraja la kwanza wakaipandisha ligi kuu, ikawa ni timu bora na kushika nafasi ikiwa ndio imepanda ligi kuu ikitokea chini.

Tom kumbe kacheza timu nyingi aisee, baada ya kutoka Bandari akaelekea zake Oman akacheza kwenye timu inaitwa Majis ambayo hata Boniface Pawasa aliwahi kupita hapo, hakukaa muda mrefu akarudi Bongo akasajiliwa Ndanda kabla ya kurdi tena Oman akaenda kucheza klabu inayoitwa Al Bashaer akakaa kwa msimu mmoja alivyorudi akasaini African Lyon kabla ya kusuka daraja msimu uliopita.

Katika kipindi chote cha maisha yake ya soka la ushindani, kuna vitu hawezi kuvisahau

“Siwezi kusahau aina ya magoli ambayo nilikuwa nafunga, huwa nalala na nikikaa nakumbuka kwa sababu wakati mwingine naweza kuona mtu anashindwa kufanya kitu fulani halafu najikuta nakumbuka enzi zangu nilikuwa naweza kufanya kitu hicho.”

“Nilipata bahati ya kuwa na uwezo wa kufunga magoli tofautitofauti kwa hiyo hivyo vitu huwa vinanirudia lakini nasikitika haikuwa katika nyakati hizi, wakati mimi nafanya nilikuwa sionekani lakini sasa hivi kila kitu kinaonekana kwa hiyo natamani vitu vyangu watu wangekuwa wanaviona.”

Baada ya kuachana na soka la ushindani atafanya nini?

“Tumeanzisha taasisi ambayo itakuwa inajihusisha katika kuelimisha wanamichezo wenzetu na kuwashauri huko ndipo tunapoelekea. Kuna miradi ambayo tumeiandika tunaweza kuifanya kwa hiyo tunapumzika lakini sio kwamba tutakuwa nje ya mpira, tutakuwa ndani ya mpira na michezo lakini kwa namna nyingine.”Read More

Share.

About Author

Comments are closed.