Sunday, August 18

MBUNGE HUSSEIN BASHE AKABIDHI NYENZO ZA KUFUNDISHIA KIDATO CHA TANO NA SITA NA VIFAA VINGINE ZAIDI YA 400, MKUU WA SHULE ASEMA NI KIONGOZI WA KUIGWA

0


Mbunge wa Jimbo la Nzega mkoani Tabora, Hussein Bashe (CCM) leo Machi 24, 2018 amekabidhi vitabu, mbao za matangazo na vifaa mbalimbali vya kujifunzia vya kidato cha tano na sita katika shule ya Sekondari Burunde iliyopo wilatani Nzega.

Wilayani humo shule ya sekondari ya Burunde ni ya pekee yenye masomo ngazi ya kidato cha tano na sita iliyojengwa kwa juhudi za mbunge huyo (Mh. Bashe) ili kuinua Elimu katika jimbo hilo.

Akipokea vitabu hivyo Mkuu wa shule hiyo, Mwalimu Fares Shedrack amesema katika nchi hii mbunge Bashe ni miongoni mwa viongozi wa kuigwa kwa kile alichosema ana moyo wa kuwahudumia wananchi, maana alianza katika ujenzi na sasa ameleta vifaa na vitabu.

“Mh. Bashe ni miongoni mwa viongozi wa mfano wa kuigwa katika nchi hii, ni kutokana na moyo wake wa kipekee katika kuwahudumia wananchi,

Alianza na ujenzi wa Bweni na akahamasisha serikali ikajenga madarasa, akajenga maabara na kusaidia kuleta vifaa na kompyuta kwa ajili ya maabara, ni wapi unaweza kupata Mbunge wa kufanya mambo yote haya??”. Amesema mwalimu Faresi na kuhoji.

Aidha kwa upande wa Mh. Bashe amesema kuwa yanayofanyika ni sehemu tu ya mchango wao kama wabunge na viongozi ili kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri Mh. John Pombe Joseph Magufuli za kutoa Elimu bure bila ubaguzi.

“Kwetu sisi tulizaliwa katika familia masikini, tukasoma katika shule ambazo hazikuwa na hata vitabu leo hii tunajua thamani ya uwepo ya nyenzo hizi kwa wadogo zetu, Elimu ni vazi la utu lisiloharibika kamwe” amesema Mh. Hussein Bashe.

Kabla ya kutoa msaada wa vitabu hivyo, Mbunge huyo (Hussein Bashe) alianza kwa kusaidia ujenzi wa Bweni kubwa na vyoo katika shule hiyo vilivyogharimu zaidi ya Shilingi milioni (37,000,000) yote ikiwa ni pesa yake binafsi huku akiamini serikali itamuunga mkono baaadae.

Baada ya juhudi za mbunge huyo katika kuisaidia Shule hiyo ili kuinua Elimu kuonekana, serikali iliamua kutoa kiasi cha jumla ya shilingi Milioni mia mbili Hamsini na tisa (259,000,000) ili kusaidia ujenzi wa vyumba vya madarasa ambapo baada ya kukamilika tayari wanafunzi wameshaanza kusoma lakini pia na ujenzi wa Bweni jingine la pili.

Vilevile Mh. Bashe amefanikisha kusaidia ufadhili wa masomo kwa wanafunzi zaidi ya 70 waliofaulu kujiunga na masomo ya kidato cha tano na sita kwenye shule mbalimbali nchini kupitia programu yake Bashe Scholarship Awards ya kuinua Elimu, idadi hiyo ikiwa ni ya Januari mwaka huu 2018.

Wengi wanaonufaika wanafunzi wanaotoka kwenye kaya masikini, ambao wamekuwa wakinufaika na ufadhili huo, yote ni kutokana na kauli mbiu anayoiishi kuwa
“Elimu ndio msingi na njia pekee ya kumkomboa mtoto masikini, ili kutokuurithi umasikini wa wazazi na kutoka katika mzunguko huo wa umasikini”

Kwa maendeleo hayo, Mzega inakuwa ni moja ya miji inayokua kwa kasi nchini katika uboreshaji wa huduma za kijamii kuazia uboreshaji wa huduma za afya, Elimu na maji.

Huku mbunge huyo wa Nzega mjini Mh. Bashe akiwa amejikita kwenye kipaumbele chake cha Elimu kama njia ya kuuondoa umasikini uliokithiri miongoni mwa wananchi wa jimbo hilo mkoani Tabora.Read More

Share.

About Author

Comments are closed.