Saturday, August 24

Ziara ya Sevilla yaacha gumzo soka la Bongo 

0


NA MWANDISHI WETU

ZIARA ya mabingwa mara
tano michuano ya Europa League, Sevilla inayoshiriki Ligi Kuu ya Hispania
maarufu La Liga ambao walikuja nchini kwa udhamini wa kampuni ya michezo ya
kubahatisha ya SportPesa, ilihitimishwa kwa mchezo dhidi ya mabingwa wa Ligi
Kuu Bara, Simba.

Mchezo huo uliotambulika
kama ‘La Liga World SportPesa Challenge’ na kuonyeshwa mubashara kwa zaidi ya
nchi 20 Afrika na DSTV kupitia chaneli ya SuperSport 9, ilichezwa usiku kwenye
Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Ni mchezo ambao pia ulitazamwa
na mamilioni ya mashabiki wa soka duniani kupitia Youtube Channel ya La Liga
Santander na kushuhudia Simba ikionyesha kandanda safi licha ya kufungwa mabao
5-4.

Laiti mchezo huo ungemalizika
kipindi cha kwanza, basi Simba wangetoka na ushindi wa mabao 3-1 lakini uwezo
mkubwa walionao Sevilla iliyomaliza nafasi ya sita kwenye msimamo wa La Liga
msimu huu, ulidhihirika kipindi cha pili na kupata mabao yaliyowahakikishia
ushindi.

Takribani mashabiki 35,000
walijitokeza Uwanja wa Taifa kuwashuhudia nyota wa Sevilla kama vile Roque
Mesa, Ever Banega na Nolito ambao walitua nchini na kupata mapokezi mazuri
yakiongozwa na bendi ya Mrisho Mpoto.

Nolito na mchezaji wa
kimataifa wa Uholanzi, Quincy Promes kila moja alifunga mabao mawili huku jingine
likipachikwa na Sergio wakati John Bocco naye alifunga mabao mawili kwa upande
wa Simba na mengine yakifungwa na Meddie Kagere na Clatous Chama.

Akizungumza baada ya
mchezo huo, kocha wa Sevilla, Joaquin Caparros, ambaye huo ndiyo ulikuwa mchezo
wake wa mwisho kabla ya kuanza majukumu yake mapya ya ukurugenzi wa ufundi wa
timu hiyo, alisema walijua mchezo utakuwa mgumu kutokana na Simba tayari
walikuwa wameshatetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara.

“Ni burudani kwa mashabiki
hususan mabao mengi yanapofungwa… Tumefarijika kuja kucheza Tanzania tena na
mabingwa wa ligi,” alisema Caparros.

Naye mshambuliaji wa Sevilla,
Promes, alisema walitaka kushinda mchezo huo na walifanikiwa kuubadili kipindi
cha pili.

Nolito ambaye pia ashawahi
kukipiga Manchester City, alisema wamefarijika na namna mchezo ulivyokuwa na
sasa wanataka kuendelea na kasi hiyo hiyo msimu mpya utakapoanza Agosti mwaka
huu.

“Tulibadilika kadiri
mchezo ulivyokuwa unaendelea. Ninafuraha sana kwa sababu ni muda sasa tangu
nicheze dakika zote 90. Nimepata bahati ya kucheza mchezo wa mwisho wa msimu
kwa dakika zote,” alisema mchezaji huyo raia wa Hispania.

Katika ziara yao ikiwa ni
sehemu ya LaLiga Worldproject, Sevilla imekuwa timu ya kwanza kutoka Hispania
kucheza mchezo wa kimataifa wa kirafiki nchini Tanzania. Mara tu baada ya
kuwasili Dar es Salaam Jumanne iliyopita, msafara wa Sevilla iliyowajumuisha Rais
Jose Castro, mkurugenzi wa ufundi, Ramon Rodriguez ‘Monchi’ na nyota wa kikosi
cha kwanza kama vile Wissam Ben Yedder, Jesus Navas na Munir El Haddadi,
walishiriki shughuli mbalimbali kama vile kliniki ya soka ya wachezaji vijana
wa timu ya BomBom katika Uwanja wa Taifa, semina ya utawala na viongozi wa
klabu na taasisi na kutembelea Makumbusho ya Taifa.

Sevilla walijua
wanawakabili wapinzani wao, Simba ambao mechi yao dhidi ya Singida United ambao
walishinda 2-0 iliwapa taji ya 20 Ligi Kuu Bara. Aidha, Simba walifika robo
fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu wakitumia vyema uwanja wa nyumbani
kuwafunga vigogo wa Afrika kama vile Al-Ahly ya Misri na AS Vita ya Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Congo.

*Kuhusu LaLiga World
Challenge

LaLiga World Challenge ni
programu iliyoanzishwa 2014 na LaLiga kwa msaada wa Serikali ya Hispania, Baraza
na Michezo na Taasisi ya Biashara ya Mambo ya Nje Hispania. Lengo ni kupeleka
klabu za Hispania duniani kote kwa miradi yenye sura ya soka la Hispania
kimataifa.

Share.

About Author

Leave A Reply