Tuesday, July 23

ZAHERA AMUOTA MSUVA

0


NA WINFRIDA MTOI

KOCHA Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera, ameweka wazi tatizo la kikosi chake ni kukosekana kwa winga mzuri anayeweza kucheza kama vile Simon Msuva.

Zahera alisema hayo juzi baada ya mchezo wake na Ndanda FC, waliotoka sare ya bao 1-1 katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kocha huyo licha ya kuwapo kwa Deus Kaseke na Mrisho Ngassa, lakini bado hajapata winga anayeweza kucheza kulingana na falsafa yake na ndiyo sababu amekuwa akiwabadilisha kila mara na kushindwa kupata matokeo anayotaka.

“Timu yangu haina mbinu nzuri kule pembeni kutokana na kukosa mtu maalumu anayeweza kucheza kwa falsafa yangu kama anavyocheza Simon Msuva, unaona mara leo namchezesha Kaseke, kesho Ngassa, Raphael Daud na leo (juzi) nimemjaribu Jaffar (Mohamed), lakini bado hawajacheza ninavyotaka,” alisema Zahera.

Alisema hali hiyo imekuwa ikimuumiza, hivyo itakapofika usajili wa dirisha dogo ni lazima atasajili mchezaji anayeweza kucheza vizuri nafasi hiyo.

“Kweli kiwango cha timu kinashuka lakini tatizo ni kule pembeni, dirisha dogo kuna ulazima wa kusajili mtu atakayeendana na vile ninavyotaka kucheza,” alisema Zahera.

Hata hivyo, alikisifia kiwango cha timu yake kuwa walicheza vizuri katika michezo yao mitatu mfululizo na ataendelea kuwafanyisha wachezaji wake mazoezi ya kufunga.

Katika msimamo wa Ligi Kuu, Yanga wapo nafasi ya tatu na pointi 26, baada ya kucheza mechi 10, kushinda michezo nane na sare mbili.

Tangu ameondoka Simon Msuva, Yanga haijapata winga anayeendana na mchezaji huyo, hivyo kuifanya isishinde kwa mabao mengi kama ilivyokuwa zamani.

Share.

About Author

Leave A Reply