Monday, March 25

Yanga yamtafuta ubaya Mo

0


*Kwa
walichopanga kukifanya, Wekundu wa Msimbazi lazima walie Ligi Kuu Bara

NA ZAITUNI KIBWANA

ZIKIWA zimebaki siku tatu kabla ya Yanga kuvaana na
Biashara United katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaopigwa Uwanja wa Taifa,
Dar es Salaam, Kocha Mkuu wa Wanajangwani hao, Mwinyi Zahera, ametamba
kuendeleza ushindi lengo likiwa ni kuzidi kujikita kileleni mwa kipute hicho
hadi mwisho.

Kauli hiyo ya Zahera huenda zikawa ni habari mbaya
kwa watu wa Simba, akiwamo mwekezaji wao, Mohammed Dewji ‘MO’, ambao wanatamani
kukiona kikosi cha Wekundu wa Msimbazi hao kikiendelea kutamba kwa kutetea
ubingwa wao.

Japo Mo na mabosi wenzake wa Simba akili yao ni
kuipa timu yao mafanikio katika anga ya kimataifa, lakini hawawezi kuudharau
ubingwa wa Bara unaowapa tiketi ya kushiriki michuano inayosimamiwa na
Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Ikumbukwe kuwa Simba ilihaha misimu mitano kuusaka
ubingwa wa Bara bila mafanikio kabla ya kubeba ‘mwali’ msimu uliopita, ikiwa ni
baada ya Yanga kutamba ndani ya kipindi hicho, ikibeba kombe mara nne na Azam
mara moja.

Akifahamu pengo la pointi lililopo baina yao na
Simba, yaani pointi 11, Zahera aliliambia BINGWA kuwa amejizatiti kuhakikisha
hawashuki kileleni mwa ligi hiyo kwa kushinda mechi zao zote zijazo, ikiwamo
dhidi ya Biashara United wikiendi hii ili mwisho wa siku waweze kuurejesha
ubingwa wa Bara Jangwani.

Akizungumzia mchezo wao huo unaofuata utakaopigwa
Jumapili, Zahera alisema: “Kikosi chetu kipo fiti na tayari kwa mechi zote za
ligi kuu zinazofuata, ikiwemo ya wikiendi hii dhidi ya Biashara United.
Tumejipanga kuibuka na pointi tatu ili tuendelee kujiweka pazuri.”

Alisema baada ya kikosi cha Yanga kurejea Dar es Salaam
jana mchana kikitokea mkoani Mbeya kilipocheza mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya
Tanzania Prisons, kikosi chake kinatarajia kuingia kambini leo kuanza
maandalizi ya kuivaa Biashara United.

Katika hatua nyingine, Mratibu wa timu hiyo, Hafidh
Saleh, amesema kambi hiyo wataitumia vema kwa ajili ya kujiandaa na mchezo huo
na mingine minne inayofuata kuhakikisha wanashinda yote ili watwae ubingwa wa
ligi hiyo.

Baada ya kushuka dimbani mara 14, Yanga
wamejikusanyia pointi 38 huku Simba waliocheza mechi 12, wakiwa na 27,
wakishika nafasi ya tatu nyuma ya Azam waliojikusanyia pointi 35 kutokana na
michezo 14.

Share.

About Author

Leave A Reply