Tuesday, March 19

Yanga juu, juu zaidi

0


*Waitwanga Prisons 3-1 kwao, Tambwe apiga mbili safii Zahera apagawa, amtaja Sonso; Ngassa alambwa ‘red’

NA HUSSEIN OMAR, MBEYA

MABAO mawili ya dakika za mwishoni yaliyofungwa na mkongwe, Amissi Tambwe, yameiwezesha Yanga kuzidi kujikita kileleni mwa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kuichabanga Tanzania Prisons mabao 3-1 katika mchezo uliopigwa jana kwenye Uwanja wa Sokoine, mjini hapa.

Kwa ushindi huo, Yanga imefikisha pointi 38 na kuendelea kukalia usukani wa ligi hiyo, huku kubwa zaidi, wakiendeleza rekodi yao ya kutopoteza mchezo msimu huu, wakishinda 12 na kupata sare mbili.

Azam inayoivaa Stand United leo, ndiyo inayoshika nafasi ya pili ikiwa na pointi zake 33 baada ya kushuka dimbani mara 13, ikishinda 10 na sare tatu, ikiwa haijapoteza mchezo wowote kama Yanga.

Kwa upande wao, Prisons wameshuka hadi nafasi ya mwisho wakiwa na pointi 10 tu, baada ya kushuka dimbani mara 15, wakishinda mchezo mmoja, sare saba na kufungwa sita, huku Biashara United waliofungwa mabao 2-1 na Lipuli, wakitoka mkiani na kushika nafasi ya pili kutoka mwisho.

Baada ya kuwa nyuma kwa bao 1-0, Yanga ilionekana kuelekea kupoteza mchezo huo wa jana kutokana na wachezaji wake kadhaa kupagawa, akiwamo Mrisho Ngassa, aliyejikuta akionyeshwa kadi nyekundu kwa kumpiga kichwa mchezaji wa Prisons, huku Ibrahim Ajib na Andrew Vincent ‘Dante’, wakionyeshwa kadi za njano kwa kumzonga mwamuzi.

Ajib na mwenzake huyo walifanya kosa hilo lililowapa kadi ya njano, wakimlalamikia refa huyo kwa kuwapa Prisons penalti kwa madai ya Dante kumfanyia madhambi Jeremia Juma.

Mbali ya Ngassa, mchezaji mwingine aliyeonyeshwa kadi nyekundu ni Lauriani Mpalile wa Prisons kwa kosa la kumpiga kichwa mkongwe huyo wa Yanga.

Alikuwa ni Jumanne Elfadhili aliyeiandikia Prisons bao lao pekee baada ya kuukwamisha nyavuni mpira wa adhabu hiyo ya penalti iliyotolewa na mwamuzi Meshak Suda kutoka Singida katika dakika ya 45.

Ajib aliisawazishia Yanga kwa mkwaju wa penalti iliyotolewa na mwamuzi huyo dakika ya 75 baada ya beki wa Prisons kuunawa mpira ndani ya eneo la hatari alipokuwa akizuia shuti la Heritier Makambo.

Tambwe aliyeingia uwanjani dakika ya 72 kuchukua nafasi ya Juma Abdul, aliifungia Yanga bonge la bao dakika ya 85, akiunganisha nyavuni kiufundi krosi maridadi ya Matheo Anthony kutoka wingi ya kulia.

Katika dakika ya 90, Tambwe tena aliwainua mashabiki wa Yanga baada ya kufunga bao la tatu na kuizima kabisa Prisons iliyoonekana kupania mno mchezo huo ili kujinusuru kutoka katika janga la kushuka daraja.

Tambwe alifunga bao hilo baada ya kuinasa pasi ndefu ya Thaban Kamusoko ambapo akiwa anaelekea kuonana na kipa, Aron Kalambo, aliubetua mpira na kumpita mlinda mlango huyo aliyejikuta akishindwa la kufanya zaidi ya kuzikodolea macho nyavu zake zikiwa zinatikisika.

Kwa ujumla, ushindi huo ulipokewa kwa shangwe kubwa na mashabiki wa Yanga waliokuwapo uwanjani, lakini hata wale waliokuwa wakiufuatilia kupitia runinga ambao walishaanza kukata tamaa ya kuvuna pointi zote tatu baada ya timu yao kuanza kufungwa, lakini pia nyota wao, Ngassa kutolewa kwa kadi nyekundu.

Lakini pia, Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera, naye alionekana kupagawa kwa kipindi kirefu cha mchezo huo kabla ya kupata ahueni baada ya vijana wake kuwa mbele kwa mabao 2-1.

Katika mchezo huo, Yanga ndio waliokuwa wa kwanza kulifikia lango la Prisons ambapo dakika ya tatu tu, Ajib alipokea pasi ya Ngasa, lakini akiwa ndani ya 18, alipiga  shuti kali lililotoka nje ya goli.

Dakika ya tano, beki wa kati wa Yanga, Abdallah Shaibu ‘Ninja’, alifanya makosa na kunyang’anywa mpira ndani ya eneo la hatari, lakini hata hivyo hatari hiyo iliokolewa na wenzake.

Makambo nusura aifungie Yanga bao dakika ya 9 ambapo shuti alilopiga akiunganisha krosi iliyochongwa na Ngassa, lilidakwa na kipa wa Prisons, Kalambo.

Dakika ya 34, Ajib alikosa nafasi ya wazi ya bao akiwa eneo la hatari baada ya kupiga shuti lililotoka nje ya lango, ikiwa ni kutokana na piga nikupige iliyotokea langoni mwa Prisons.

Prisons walipata nafasi ya kufunga bao dakika ya 34 baada ya kupata adhabu ndogo iliyotolewa kwa Maka Edward wa Yanga kumfanyia madhambi Kelvin Friday, lakini Jeremia Juma alishindwa kuitumia vema kwa mkwaju wake kutoka nje ya lango.

Elfadhil alionyeshwa kadi ya njano katika dakika ya 52 baada kumfanyia madhambi kiungo wa Yanga, Feisal Salum ‘Fei Toto’.

Dakika ya 70, Anthony aliikosesha Yanga bao la wazi baada ya kupiga kichwa mpira wa krosi iliyochongwa na Abdul na kuokolewa na kipa wa Prisons na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.

Yanga walikosa bao dakika ya 88 kutokana na krosi iliyochongwa na Haji Mwinyi kumkuta Tambwe aliyepiga shuti kali lililowababatiza mabeki wa Prisons na kuwa kona tasa.

Kikosi cha Prisons: Aron Kalambo, Salum Kimenya, Lauriani Mpalile, Nurdin Chona, James Mwasote, Jumanne Elfadhili, Benjamin Asukile, Cleophace Mkandala, Kelvin Friday, Hassan Kapalata na Jeremiah Juma/Hamis Maigo(dk83).

Kikosi Yanga: Ramadhan Kabwil, Juma Abdul/Amis Tambwe(dk 72), Mwinyi Haji, Andrew Vincent ‘Dante’, Abdallah Shaibu ‘Ninja’, Maka Edward/Matheo Antony (dk45), Mrisho Ngassa, Feisal Salum ‘Fei Toto’/Thabit Kamusoko (dk), Haritier Makambo, Ibrahim Ajib na Raphael Daudi.

Wakati huo huo, Kocha wa Yanga, Zahera, amesema hafahamu taarifa za usajili wa beki wa Lipuli, Ally Sonso, ndani ya kikosi chake kama ambavyo imekuwa ikiripotiwa.

Katika michezo mingine ya ligi hiyo iliyochezwa jana, Lipuli wakiwa kwao Iringa kwenye Uwanja wa Samora, iliichapa Biashara United mabao 2-1, huku Mwadui waliokuwa wenyeji wa KMC, waliambulia sare ya bao 1-1.

Matokeo hayo yameibeba Lipuli na kuchupa hadi nafasi ya 13 kutoka ya 17, huku Mwadui iliyokuwa nafasi ya 15 ikipanda kwa nafasi mbili na KMC ikitoka nafasi ya 11 hadi ya 10.

 

Share.

About Author

Leave A Reply