Sunday, August 25

Yanga inahitaji akili ya ‘Makamu Mwenyekiti’ Mwakalabela

0


NA MARKUS MPANGALA

UCHAGUZI wowote unapofanyika ndani ya timu ya soka ya Yanga unakuwa
na mvuto wa kipekee. Yanga wana historia ya kujenga na kusisimua katika soka la
Tanzania kabla ya uhuru. Kwa sasa Yanga wanakabiliwa na uchaguzi mkuu wa mwenyekiti.
Ni timu ambayo inakadiriwa kuwa na mashabiki wengi kuanzia viongozi wa Serikali
na wananchi wa kawaida.

Jina la Frederick Mwalebelea ni miongoni mwa wagombea wa
uenyekiti Yanga. Binafsi ninaamini kabisa Frederick Mwakalebela ndiye kiongozi
sahihi wa kuongoza Yanga sasa na kuivusha kuelekea kwenye mafanikio zaidi
kuwazidi Simba. Ninaeleza sababu.

‘SPOTI
KIZAAZAA’

Nakumbuka hata baada ya kuondoka kwenye uongozi wa
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), hakuwa mbali na mchezo huo. Nilikuwa
sambamba na Mwakalebela kwenye urushaji wa kipindi cha michezo cha ‘Spoti
Kizaazaa’, kikitangazwa na rafiki yangu Ezekiel Kamwaga.

Kwa jinsi ambavyo alikuwa anatoa mafunzo kwa mashabiki
tuliokuwa tunahudhuria siku za kurekodi kipindi hicho, hakika ilikuwa wazi analala
na kuamka akilini mwake akiwa na ndoto za kulifanya soka letu lipige hatua
kubwa zaidi.

Kwenye kurekodi kipindi hicho. kulikuwa na malumbano ya
hoja, mihemko na kila hoja zilirushwa nje ya kipindi ili kujiweka sawa. Kwa
jinsi alivyokuwa akiwaelekeza watu waliohudhuria, ilikuwa kama mwalimu
anaelekeza wapi tunatakiwa kupita ili kuleta mafanikio ya soka letu.

Mwalimu ambaye alikuwa anatujengea uwezo mashabiki wa soka
na kupata mwanga ni nini kinachotakiwa kufanyika katika soka letu. Kwangu mimi
Mwakalebela ni dira ambayo inatembea mitaani kila siku na ambayo inatakiwa
kupewa nafasi ya kutekelezwa kwa sasa na wanachama wa Yanga.

Nakumbuka tulikuwa na mjadala wa moto sana kuhusiana na
nafasi za makocha wetu nchini kutamba ndani na nje. Tulijadili mambo chanya na
hasi, nikagusia namna Gareth Southgate alivyokuja kupewa nafasi ya ukurugenzi
wa kituo cha michezo.

Tulijadili juu ya nani anawajibika kuendeleza soka. Hakika
tulichimba na kuonyesha wazi kuwa Mwakalebela alikuwa anatamaa kubwa ya kuona
soka la Tanzania linapiga hatua kubwa mno.

Nakumbuka siku hiyo ilibidi rafiki yangu Ezekiel Kamwaga
anikumbushe nimezidisha dakika za kuongea kwenye kipindi. Mwakalebela akawa
anacheka mno pembeni, akiona mnyukano wa hoja na namna Watanzania walivyo na
tamaa ya mafanikio ya soka nchini. Tatizo alilioona ni njia ya kupita na namna
viongozi wanavyoweza kuwapitisha kwenye mafanikio wachezaji wetu pamoja na
kuimarisha soka.

Pili, ukiangalia majina na wasifu wa wagombea wa nafasi ya uenyekiti
wa Yanga, utaona wazi kuwa Frederick Mwalebela ni mtu ambaye ana ufahamu mkubwa
na mpira wa miguu hapa nchini. Si kwa maneno au masimulizi ya kusadikika bali
kwa vitendo kutoka ngazi ya klabu hadi uongozi wa taifa.

Mwakalebela kwenye uongozi wake wa taifa, amefanya kazi na
majina makubwa kama mwanandinga maarufu nchini Leodgar Tenga. Chini ya uongozi
wa Mwakalebela ndipo alipokuwapo kocha kipenzi cha Watanzania, Marcio Maximo.

Na kipindi hicho hicho ndipo tukafanikiwa kufuzu kwa
mashindano ya CHAN yaliyofanyika nchini Ivory Coast. Katika kipindi cha uongozi
wake, wadhamini walimiminika kuidhamini Taifa Stars au Ligi Kuu Tanzania Bara.
Uongozi wake ndio uliojenga msingi kuhusiana na mafanikio ya Taifa Stars.

MWAKALEBELA
KAMA ‘MERITOCRACY’

Neno ‘Meritocracy’ (tamka Meritokrasi) limechukuliwa kutoka
lugha ya Kigiriki kwenda Kiingereza. Linatumika zaidi kwenye maeneo ya
kitaaluma na uongozi kama ambavyo Yanga wanahitaji uwezo wa Mwakalebela.

Maana ya neno hili ni uwezo wa kuwa na ushawishi, nguvu na mvuto
kuwavutia watu ili wakuchague. Jamii inapotengeneza uongozi wake, basi
panakuwapo watu wenye ushawishi kulingana na uhodari wao kwenye utendaji kazi,
ushirikiano na kadhalika.

Wapo viongozi wanaonufaishwa na hii ‘Meritocracy’ kwa kuwa
daima hujihusisha na ujenzi wa jamii bora wakiwa na uwezo mzuri wa kutenda na kusimamia
uamuzi wa maendeleo kama soka.

Katika uongozi wowote, panaweza kuwepo mmoja wao
akapapatikiwa kukabidhiwa madaraka mbalimbali. Kiongozi anaweza kupewa madaraka
katika maeneo tofauti na akafanya kwa ufanisi. Hilo linachochea wenye uamuzi
kuzidi kuvutiwa na utendaji kazi, mawazo mazuri, fikra zenye chachu ya ufanisi
na maendeleo.

Hakuna kitu cha kuficha hapa, Mwakalebela  ni mchapakazi, mweledi na mtu anayependa ushirikiano,
misimamo, wajibu, kuvumbua fikra mbadala ya kuhakikisha Yanga na wanachama wake
wanafurahi kila kukicha. Anaweza kustahimili majukumu makubwa ambayo yanagusa
wanachama wa Yanga.

KORIDO
LA CAF, FIFA

Kitu kimoja ambacho napenda kuwasisitizia wanachama wa Yanga
ni kwamba, muda wa kumchagua mtu eti kwa kuwa ni mjanja mjanja na anawajua sana
waganga wa kienyeji, umepita.

Yanga inahitaji kiongozi mwenye kila uzoefu kuanzia kwenye
korido la Shirikisho la Soka barani AFrika hadi lile la duniani yaani FIFA.
Yanga wanamhitaji Mwakalebela ambaye ana harufu zote nzuri kutoka kwenye
makorido ya CAF na FIFA.

Kote huko amechota mawazo, uzoefu na mbinu za kuiwezesha
klabu ya Yanga kusonga mbele. Yanga inatakiwa kuwa na mtandao mkubwa duniani
ambako angalau iwe imeuza wachezaji 1,000 pamoja na kuwa na timu rafiki kama 3,000
hivi duniani.

Haya hayawezi kutokea bila mtu ambaye anaijua FIFA na CAF,
ambako viongozi wa klabu hukutana mara kwa mara kujadili masuala mbalimbali ya
soka. Yanga inatakiwa kuwa levo moja na akina TP Mazembe, Esperance, Club
Africain, Al Ahly, Mamelodi Sundowns, Raja Casablanca na nyingine zenye hadhi
ya juu.

Unapokuwa na kiongozi mwenye mtandao mkubwa ambao
unawahusisha FIFA au CAF, maana yake mnaweza kutumia fursa hiyo kujiongezea
wadhamini, mbinu za kuleta maendeleo Yanga na mengine mengi tu.

Mwakalebela tayari ni mtu ambaye amejengwa katika misingi ya
uongozi katika pande mbili; siasa na michezo. Lakini sehemu kubwa ya maisha yake
yamekuwa soka. Analala soka, anapumua soka na anakula soka. Ndiyo maana sasa anataka
kuwapa nafasi ya kupasua anga Yanga.

Hivi wana-Yanga hawana wivu wanapoambiwa kuwa wana idadi
ndogo ya wachezaji waliouzwa kwenda soka la kulipwa nje kuliko wenzao Simba?
Hayo yote yanatokana na mipango. Ni lazima kuwa na kiongozi kama Mwakalebela
ambaye anafahamu Yanga inahitaji kupendwa na wafadhili, utawala bora, kutamba
Afrika, kumiliki kiwanja chake cha kisasa na kuwa na wachezaji wengi wenye
hadhi ya Simon Msuva.

Mwakalebela ana uzoefu mkubwa kuhusu masuala ya soka nje ya
nchi. Ni kizazi ambacho kinatuondoa kwenye yale mawazo ya kijamaa hadi kwenye
msingi wa kisasa ambao watu wanabuni mawazo ya kuyaweka mezani kisha kujadili
na kutekeleza.

Yanga inamhitaji Mwakalebela ambaye anawaza kutwaa makombe
ya Afrika na kuungana na TP Mazembe kuwa klabu ya kwanza Tanzania kushiriki
Mashindano ya Klabu Bingwa duniani kuliko kuhangaishana na mambo ya CECAFA.

SOKA
LIMEMLEA

Mwakalebela anatosha na ataipasha Yanga. Ameiongoza Mtibwa
Sugar miaka minne, Mwenyekiti wa Chama cha Soka cha Wilaya ya Movero mitatu, mwanzilishi
wa Team ya Mtibwa Query, mwanzilishi wa Mtibwa United, Mjumbe wa kamati ya
kuipandisha Lipuli kwenye Ligi Kuu. Halafu ni msomi pia wa shahada ya
uzamili.  Ubongo wake umetunukiwa na
vyeti vya uongozi wa FIFA, CAF na Baraza la Michezo Taifa. Halafu aligombea
urais TFF. Wanayanga mnataka nini zaidi?

Share.

About Author

Leave A Reply