Friday, August 23

Wizara izikumbuke sanaa za ufundi na ubunifu

0


NA CHRISTOPHER MSEKENA

HIVI karibuni hotuba
ya makadirio ya bajeti ya mwaka 2019/20 ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa
na Michezo ilisomwa bungeni jijini Dodoma na Waziri Dk. Harrison Mwakyembe.

Miongoni mwa mambo
yaliyoibuka katika hotuba hiyo ni wasanii marehemu kama Steven Kanumba na Mzee
Majuto kulipwa fedha zao za fidia baada ya upitiaji upya wa mikataba ya kazi
walizowahi kufanya na kampuni mbalimbali enzi za uhai wao.

Wakati hayo
yakiendelea, nimejaribu kuangalia upande mwingine wa sanaa za ufundi na ubunifu
ambazo zipo kwenye wakati mgumu zaidi ya ilivyo kwa wasanii wa muziki na
filamu.

Tumeona mafanikio
makubwa kwa muziki hasa ule wa Bongo Fleva. Wasanii wake kwa kiwango fulani
wananufaika na kazi zao kutokana na 
muziki wao kufanya vizuri kwenye masoko ya ndani na nje ya Bongo.

Halkadhalika wasanii wa filamu, hali zao si mbaya sana licha ya changamoto kadhaa ambazo ni rahisi kutatuliwa na kufanya wasanii wake wanufaike na kazi wanazozifanya.

Ila sanaa za ufundi na ubunifu kama
vile uchongaji, uchoraji, ufinyanzi, ufumaji, ushonaji na ususi zina hali mbaya
kiasi kwamba wasanii wake wanaishi maisha ya shida licha ya kufanya kazi nzuri
na kubwa ambayo nyingine zinaitambulisha vizuri nchi yetu.

Mfano ni uchoraji, hakuna ambaye
hafahamu jinsi sanaa hii inavyoitambulisha vyema Tanzania nje ya nchi ndiyo
maana picha mbalimbali za wasanii hao hutumika kama zawadi pale ambapo viongozi
wageni wanapotutembelea.

Picha za wasanii hawa zimepamba ofisi
za taasisi mbalimbali zikiwa zimebeba uwakilishi mzuri wa vivutio
vinavyopatikana Bongo, unaweza kuona picha kama hizo za kibunifu ndani ya Ukumbi
wa Bunge.

Wakati wa usomaji wa hotuba ya makadirio
ya bajeti katika wizara hii, nilivutiwa zaidi na hoja aliyoitoa Mbunge wa Geita
Vijijini, Joseph Kasheku maarufu kama Musukuma, kuhusu hali mbaya ya wasanii wa
filamu pamoja na ile alioiita mapungufu kwenye Bodi ya Filamu Tanzania.

Ila jambo la kushangaza hakuna mbunge
aliyeweza kuziongelea sanaa za ufundi na maonyesho, hakuna aliyeona thamani ya
kazi za wachoraji ambazo hazifanani kabisa na maisha wanayoishi, jambo
linaloumiza wachoraji wengi hasa wale ambao hawana majina makubwa.

Sanaa hizi za ufundi na ubunifu
hazipewi nafasi kubwa kama muziki na filamu, jambo ambalo limekuwa kilio cha
wachoraji wengi ambao wanaumizwa pale ambapo wanaona Serikali inaweka nguvu
kwenye Bongo Fleva na filamu na kuwasahau wakati umuhimu wake unajulikana.

Ingependeza Wizara sasa iweke usawa
katika kuwatengenezea mazingira rafiki wasanii wote bila kuangalia ukubwa wa
tasnia. Wasanii wa muziki, filamu, wachoraji, wachongaji na wengineo wawe
kwenye sahani moja.

Ili muziki unapofanikiwa basi
wachoraji nao wafanikiwe kwani sanaa hii bado ina soko, lakini haijatengenezewa
mazingira mazuri ya wasanii wake kunufaika na kile ambacho wanakifanya.

Share.

About Author

Leave A Reply