Saturday, August 17

Wanachama, hii ni nafasi yenu ya mwisho kuiokoa Yanga

0


NA HUSSEIN OMAR

KAMPA kampa tena! Wakimataifa, Watoto wa Jangwani
na Wazee Ndege! Ni baadhi tu ya majina ambayo Klabu ya Yanga ilibatizwa miaka
kadhaa iliyopita, kabla ya hali ya sasa inayowakumba mithili ya kupigania uhai
wake.

Kutoka kuyasikia majina hayo mpaka kubatizwa
mengine kama Wazee wa Bakuli, Chura Churani, Omba Omba FC, Wazee wa Buku, si
jambo zuri hata kidogo, lakini Waswahili wanasema kupanga ni kuchagua.

Wakongwe hao wa soka nchini hivi sasa wanatia huruma
kila kona ya mji. Imefika sehemu hata wachezaji wake wanaona aibu kusema
wanaichezea timu hiyo kwa jinsi mambo yalivyokwenda kombo.

Yanga ndiyo klabu ya kwanza kumiliki uwanja wake
yenyewe ambao ni Uwanja wa Kaunda, uliopo makao makuu ya klabu hiyo, Jangwani,
japo hauna faida na inasikitisha umegeuzwa kuwa maskani ya wahuni wanaotumia
mihadarati.

Licha ya mara kadhaa kupata viongozi wa kuliongoza
jahazi hilo la Jangwani, lakini walishindwa kutambua thamani ya klabu hiyo sambamba
na kuutelekeza uwanja hadi kufikia kutumika kwa matumizi yasiyo rasmi kwa
binadamu.

Kwa kiasi kikubwa walijali zaidi maslahi yao.
Walizingatia kuzinufaisha nafsi pamoja na familia zao hadi sasa Yanga imekuwa
yatima.

Yanga ndiyo klabu ya kwanza katika ukanda wa Afrika
Mashariki na Kati kutoa mchezaji kwenda kucheza soka la kulipwa barani Ulaya.

Ilikuwa ni mwaka 1977 ambapo Sunday Manara
‘Computer’, alipata nafasi ya kuichezea klabu ya Heracles iliyopo Uholanzi na
huko alikutana na mmoja wa wakongwe wanaoheshimika nchini humo, Ruud Krol.

Yanga, ambao walikuwa wakiwatambia Simba kwa
misimu kadhaa kutokana na jeuri ya fedha waliyokuwa nayo, kwa sasa imekuwa ni klabu
ya kawaida sana. Isiyoogopeka na timu pinzani kama ilivyokuwa hapo nyuma.

Ikumbukwe
enzi za uongozi wa Yusuf Manji, Yanga ilitisha na kujaza mashabiki wengi uwanjani
kila ilipocheza. Hivi sasa imepoteza mvuto.

Imepoteza
haiba iliyokuwa nayo zamani baada ya bilionea huyo kuachia ngazi kutokana na
matatizo binafsi yaliyokuwa yakimkabili.

Misimu
ambayo bilionea huyo alikuwapo Jangwani, Yanga ilikuwa na uwezo wa kusajili
wachezaji wa kiwango cha juu kwa gharama yoyote ile.

Yanga
chini ya Manji iliweza kuweka kambi nje ya nchi. Historia inaonesha Yanga
iliwahi kujichimbia katika moja ya hoteli za gharama nchini Uturuki kujiandaa
na Ligi Kuu Bara pamoja na michuano ya kimataifa.

Kwa
sasa klabu hiyo inakwenda katika uchaguzi mkuu ambao utafanyika Mei 5 mwaka huu.
Kwa wanachama wa Yanga ambao watapata nafasi ya kupiga kura katika uchaguzi huo,
wanatakiwa kufahamu kitu kimoja.

Hiyo
ni nafasi yao ya pekee kama si ya mwisho, kuifanya klabu hiyo ya Yanga kuwa
maskini au tajiri kwa kuchagua viongozi bora na si bora viongozi.

Wanachama
wa Yanga wanatakiwa kuepuka kuchagua viongozi ambao wana maneno mengi, huku
wakionekana kuwa na mipango mingi katika kuongoza timu, lakini kumbe wengine
walijificha katika kivuli cha Manji.

Kama
kuna kosa kubwa ambalo wanachama wa Yanga watalifanya ni kuchagua kiongozi
ambaye atakuwa na fikra za kuleta mtu mmoja tajiri na wakasahau yaliyowakuta
katika kipindi hiki cha mpito.

Kiongozi
mpya wa Yanga ajaye ni vyema akafahamu kuwa klabu hiyo yenye maskani yake
katika mtaa wa Twiga na Jangwani, ni moja ya klabu zenye historia kubwa nchini
na Afrika kwa ujumla.

Ni
klabu ambayo ilianzishwa mwaka 1935, lakini sasa ni takribani miaka 83, imeshindwa
kujiendesha na kubaki kutegemea zaidi fedha za mfukoni kutoka kwa wafadhili
mbalimbali.

Baadhi
ya wafadhili ambao waliwahi kuweka fedha zao ni pamoja na aliyewahi kuwa Mbunge
wa Kilombero na mfanyabiashara, marehemu Abbas Gulamali, Murtaza Dewji na
Manji.

Yanga
imepita katika vipindi tofauti vya shida na raha tangu kuanzishwa kwake na
inawawia vigumu kuingia akilini ukata walionao, licha ya rasilimali za kutosha
zinazoweza kuifanya kutoka katika hali hiyo.

Klabu
hiyo yenye idadi kubwa ya mashabiki, inatumia Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kama
uwanja wake wa nyumbani, ukiwa na uwezo wa kukusanya takribani watazamaji 60,000.

Kiongozi
sahihi kwa Yanga ni yule ambaye ataweza kuwabadilisha fikra wanachama wa klabu
hiyo kwa kuwepo na mchakato wa uhakika namna ya kuiendesha Yanga.

Yanga
inatakiwa kuwa klabu ya kujitegemea na si kutegemea fedha mfukoni mwa mtu mmoja
mmoja.

Hapa
wanachotakiwa kukifanya wanachama wa Yanga pindi wapatapo viongozi wapya ni
vyema wakaitisha mkutano kwa ajili ya kubadili katiba yao ili iweze kuendana na
wakati.

Moja ya
sehemu ya mabadiliko ya katiba hiyo ni kuifanya klabu ijiendeshe kisasa bila ya
kumlenga mtu mmoja, kwani kwa kufanya hivyo kunaweza kuinusuru klabu hiyo kongwe
kutoka katika ukata uliopo sasa.

Kwa
jinsi ilivyo, Yanga inatakiwa kuufanya mchakato huo kwa haraka ili kuweza
kuendana na kasi ya mabadiliko, kwani soka la sasa linahitaji uwekezaji mkubwa
wa fedha kama zinavyofanya klabu za Ulaya na kwingineko.

Kutokana
na rasilimali ilizonazo Yanga, ni wazi wana mtaji mkubwa kuliko hata wapinzani
wao, Simba, ambao hivi sasa wanakwenda katika mafanikio makubwa katika
mapinduzi ya soka hapa nchini.

Silaha
kubwa ya Yanga ni watu wake, hivyo ni wajibu wa kiongozi ajaye na jopo lake
kutambua kuwa anakuja kuongoza klabu yenye mtaji mkubwa wa mashabiki, hivyo jukumu
lililopo mbele ni kuhakikisha anaifanya iweze kujiendesha.

Lazima
atambue kuwa wapinzani wao, Simba, wamefika hapa kutokana na kasi ya mabadiliko
sambamba na kubadilisha baadhi ya vipengele vya katiba yao ambayo inawapa
kiburi.

Kwani
Simba hii ya leo hata itokee mwekezaji wake, Mohamed Dewji ‘Mo’, aachie ngazi,
kamwe haiwezi kutetereka ghafla, kwani tayari wameweza kujitengenezea mfumo wa kujiendesha
tofauti na ilivyokuwa hapo nyuma.

Lakini
pia uadilifu wa viongozi chini ya Mwenyekiti wake, Sued Mkwabi, ni sababu
nyingine inayowafanya Simba wawe na viongozi waliojitosheleza. Wasio na njaa
wala tamaa ya upigaji wa mali za klabu.

Kwa
maoni 0754 408363

Share.

About Author

Leave A Reply