Monday, August 19

Vita ya ‘top four’ EPL ngoma nzito

0


LONDON, England

WAKATI vita ya kuwania ubingwa wa Ligi Kuu England
ikiwa imebaki kati ya timu za Manchester City na Liverpool, timu nyingine nne
zinapigania kumaliza zikiwa kwenye orodha ya nne bora ili ziweze kufuzu kucheza
Ligi ya Mabingwa Ulaya.

 Timu hizo
zinazopigania nafasi hiyo ni Arsenal, Tottenham, Chelsea na Manchester United.

 Mchuano
ulizidi kuwa mgumu mwishoni mwa wiki, baada ya timu hizo kujikuta zikipata
matokeo ambayo hayakutarajiwa, baada ya Tottenham kupata kipigo cha pili
mfululizo kutoka kwa Manchester City, Manchester United wakachapwa mabao 4-0
dhidi ya  Everton, Arsenal nao wakalazwa
na Crystal Palace na huku  Chelsea
wakishindwa kutumia nafasi hiyo baada ya nao kulazimishwa sare ya mabao 2-2
na  Burnley wakiwa nyumbani.

Kwa matokeo hayo, swali lilipo ni timu ipi itachukua
nafasi ya tatu na ya nne na ni timu zipi zitakazoshiriki kwenye michuano ya
Ligi ya Europa.

Tottenham
kwa sasa inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 70  na imebakiwa na mechi dhidi ya West Ham ikiwa
nyumbani, Bournemouth ambayo watakuwa ugenini na dhidi ya  Everton ambayo pia watakuwa nyumbani.

Hata hivyo, Spurs wanaonekana kutoathiriwa sana na
kipigo hicho cha bao 1-0 kutoka kwa Man City, baada ya wapinzani wao nao
kushindwa kutumia mwanya huo kuwapiku katika nafasi hiyo ya tatu.

Pengine timu hiyo ingeweza kuathirika zaidi, baada
ya mchezaji wao tegemeo, Harry Kane, wiki iliyopita kukumbwa na majeraha ya
enka ambayo yatamfanya kuzikosa mechi zote za Spurs zilizobaki, lakini wamejikuta
wakipata nafuu, baada ya nyota wao mwingine, Son Heung-Min, kuonesha uwezo
mkubwa katika jukumu alilopewa la kuiongoza timu hiyo.

Pia ikizingatiwa mechi tatu kati ya nne zilizobaki
itakuwa nyumbani, Spurs watakuwa na nafasi kubwa ya kushika nafasi hiyo ya
tatu.

 Chelsea, kwa sasa inashika nafasi ya
nne ikiwa na pointi  67 na imebakiwa na
mechi dhidi ya Manchester United, ambayo watakuwa ugenini na kisha watarejea
nyumbani kuikabili Watford, kabla ya 
kusafiri tena kwenda kuivaa  Leicester.

Huku Chelsea wakiwa hawakucheza mwishoni mwa wiki
hadi Jumatatu usiku na huku ikiwa imeshashuhudia wapinzani wao wakishindwa
kuchukua pointi yoyote, lakini Blues nao tena wakashindwa kutumia nafasi hiyo.

Katika mchezo huo ambao walikuwa ugenini, baada ya
kuwa mbele kwa bao 1-0, Ashley Barnes aliisawazishia  Burnley na kuyafanya matokeo kuwa sare na sasa
vinara hao wanakabiliwa na mechi ngumu dhidi ya Manchester United wakiwa
ugenini Old Trafford na endapo watafanikiwa kupata ushindi kutoka kwa mashetani
hao wekundu, basi wataweza kumaliza ligi wakiwa kwenye nafasi ya nne.

Chelsea kwa sasa wanashika nafasi ya nne wakiwa na
pointi 67, wakiizidi Arsenal kwa pointi moja na ambayo watakutana nayo tena
katika mechi zake zilizobaki.

Arsenal
 kwa sasa wanashika nafasi ya tano wakiwa
na pointi  66 na wamebakiwa na mechi
dhidi ya Wolves, watakayokuwa ugenini na dhidi ya Leicester (ugenini); Brighton
(nyumbani) na dhidi ya Burnley, ambayo nayo watakuwa ugenini.

Nafasi ya Arsenal kumaliza ligi ikiwa kwenye orodha
ya nne bora inategemea kama watashinda mechi zao nne zilizobaki.

Hata hivyo, Gunners inakabiliwa na kibarua kikubwa
kutokana na kuwa mechi zake tatu itakuwa ugenini na kuna uwezekano ikapoteza
pointi dhidi ya Wolves au Leicester City kama haikufungwa mechi zote mbili.

Msimu huu pia timu hiyo imekuwa ikipata matokeo
mabaya ikiwa ugenini, jambo ambalo linaweza kuwagharimu kushika nafasi hiyo.

Pengine pia kama kocha wao, Unai Emery atafanikiwa
kutatua tatizo la safu ya ulinzi, labda wanaweza wakaambulia nafasi hiyo.

Manchester
United
kwa sasa inashika nafasi ya sita ikiwa na pointi 64
na mpaka mapema jana ilikuwa imebakiza mechi zake dhidi ya Manchester City (nyumbani);
Chelsea (nyumbani); Huddersfield (ugenini); Cardiff (nyumbani).

Baada ya kufanya vizuri tangu alipoichukua kocha
wao, Ole Gunnar Solskjaer, kwa kushinda mechi 10 na kutoka sare mara mbili za
Ligi Kuu England, Manchester United imeanza kuteleza kipindi hiki cha dakika za
mwisho ambapo imeshuhudiwa ikilamba vipigo vitatu katika mechi zake tano
zilizopita kikiwamo cha mabao  4-0 walichokipata
mwishoni mwa wiki dhidi ya  Everton na
kuanza kuzua maswali kama kocha huyo alikuwa mtu sahihi kukabidhiwa mikoba
hiyo.

Wakati jana wakicheza ‘Manchester derby’, mashabiki
wa timu hiyo walikuwa bado wapo njiapanda kama timu hiyo itaweza kumaliza ligi
wakiwa kwenye orodha hiyo ya timu nne bora.

Ushindi dhidi ya Man City ndio uliokuwa ukitarajiwa
kuwapa moyo Liverpool katika vita yao ya kuwania ubingwa na pia kama watakuwa
wamefungwa, basi  watakuwa wamepoteza
matumaini ya kushika nafasi hiyo ya nne bora.

Share.

About Author

Leave A Reply