Tuesday, March 19

Vibopa Yanga wavamia Mbeya

0


*Ni mkakati kuhakikisha Prisons hawatoki leo

*Zahera kama kawaida yake, meno yote 32 nje

NA ZAITUNI KIBWANA

WAKIFAHAMU jinsi Uwanja wa Sokoine, Mbeya unavyokuwa mgumu kwao hasa wanapocheza na Tanzania Prisons, matajiri wa Yanga wameongozana na wanachama na mashabiki wao kwenda mkoani humo kuhakikisha timu yao inaondoka na pointi zote tatu.

Wanajangwani hao watashuka kwenye uwanja huo leo kuvaana na wenyeji wao hao katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, huku vijana wa Kocha Mkuu, Mwinyi Zahera, wakiwa na usongo wa kushinda ili waendelee kukaa kileleni mwa ligi hiyo yenye timu 20.

Miongoni mwa vibopa wa Yanga walioongozana na timu yao yupo mfanyabiashara maarufu, Shabani Hussein ‘Ndama Mtoto ya Ng’ombe’, huku wengine wakitarajiwa kutua jana jioni na leo tayari kulishuhudia ‘chama’ lao likiendeleza wimbi la ushindi.

Mchezo huo unatarajiwa kuwa mgumu kwani Prisons pamoja na kuanza vibaya msimu huu, lakini si timu dhaifu kutokana na aina ya wachezaji waliokuwa nao kwenye kikosi chao kinachoshika nafasi ya 19 kwenye msimamo ikiwa imekujisanyia pointi 10 mpaka sasa.

Msimu uliopita, Yanga ilivuna pointi moja tu kutoka kwa Prisons kutokana na kufungwa mabao 2-0 kwenye uwanja huo wa Sokoine, ikiwa ni baada ya timu hizo kutoka sare ya bao 1-1 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Na kutokana na kasi ya Yanga msimu huu, ikiwa haijapoteza mchezo hata mmoja, mashabiki wa timu hiyo wameonekana kupania vilivyo mchezo huo ndio maana hata matajiri wao wameamua kuungana nao kuwapandisha mzuka vijana wao.

Ndani ya mechi zao 13 za Ligi Kuu Bara, Yanga imeshinda 11 na kupata sare mbili, huku ikiwa haijapoteza hata moja.

Kuelekea mchezo huo wa leo, mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, ameliambia BINGWA jana kwamba lengo la matajiri wa klabu hiyo ni kuhakikisha kikosi chao kinapata matokeo mazuri.

“Kuna kundi la wanachama na mashabiki likiongozwa na Ndama Mtoto wa Ng’ombe’, limeshafika Mbeya kwa ajili ya kuunganisha nguvu ili timu iweze kushinda mchezo wa leo,” alisema.

Yanga ina kila sababu ya kushinda ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kutwaa taji la Ligi Kuu Bara na kurudisha heshima yao kwa mashabiki na wapenzi wa timu hiyo iliyopotea msimu uliopita baada ya kuporwa ‘mwali’ na watani wao wa jadi, Simba.

Yanga leo itaendelea kukosa huduma za nyota wao; Papy Tshishimbi, Kelvin Yondani, Beno Kakolanya, Gadiel Michael, Pato Ngonyani, Emanuel Martin, Yohana Nkomola na Yusuph Mhilu, kutokana na sababu mbalimbali, ikiwamo majeruhi.

Akizungumzia mchezo huo, Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera, alisema ataingiza kikosi chake uwanjani akiwa na lengo la kuvuna ushindi.

“Utakuwa mchezo mgumu, kwani hata wapinzani wetu wamejipanga vizuri, malengo yetu ni kuhakikisha tunashinda michezo yote ili kufanikisha kutwaa ubingwa,” alisema Zahera.

Kwa upande wake, Kocha Mkuu wa Prisons, Abdallah Mohamed, alisema: “Hatuna hofu juu ya kilichotukuta kuhusu ubutu wa washambuliaji wangu ila tumejipanga vizuri kuhakikisha haturudii makosa tuliyofanya katika michezo yetu miwili iliyopita.”

Share.

About Author

Leave A Reply