Thursday, August 22

Usajili ni zaidi ya sinema

0


*ZAITUNI KIBWANA

WAKATI msimu wa Ligi Kuu Tanzania Bara ukihitimishwa
leo kwa timu zote 20 kushuka dimbani kwenye viwanja tofauti, suala la usajili
wa nyota wa Yanga, Ibrahim Ajib, limekuwa kama sinema.

Baada ya taarifa kuwa TP Mazembe ilikuwa na mpango
wa kumsajili nyota huyo, hatimaye juzi klabu hiyo ya DR Congo, ilitangaza
kuachana naye kwa madai ya kushindwana katika masilahi binafsi.

Lakini habari zilivuma kuwa Ajib ameshindwa kutua TP
Mazembe kwa kuwa alishafanya makubaliano ya awali na Simba ambao waliwabana
wababe hao wa DR Congo wakitaka wapate asilimia fulani ya usajili wa mchezaji
huyo anayemaliza mkataba wake Jangwani mwezi ujao.

Iko hivi, inadaiwa kiungo huyo anayevalia jezi namba
10 katika kikosi cha Yanga, amesaini mkataba wa awali na timu ya Simba huku
ikidaiwa kuwa amepatiwa milioni 50 na gari aina ya Crown rangi nyeupe.

Kwa tetesi ambazo zimezagaa mitandaoni, zinadai kuwa
Ajib alitaka kiasi cha Dola za Marekani 100,000 (milioni 220 za Tanzania) ili
asaini mkataba na kikosi cha TP Mazembe, lakini klabu hiyo ilikataa kwa kuwa
tayari walishakubaliana dau lililotajwa kuwa dola 25,000 kabla ya baadaye
kufika 30,000 (takribani Sh mil 70).

Baada ya Ajib kuonekana kung’ang’ania dau jipya la dola
laki moja, TP Mazembe waliamua kuachana naye na hivyo mchezaji huyo kurejea
nchini kuangalia ni wapi ataangukia kati ya Yanga au Simba.

Japo kwa upande mwingine, ilielezwa kuwa kiungo huyo
alitaja dau hilo la dola laki moja ili apate fedha ambayo angerejesha Simba kisha
kujiunga na mabingwa hao wa DR Congo baada ya msimu huu kumalizika.

Pamoja na kuhusishwa na Simba kwamba ameshasaini
makubaliano ya awali, lakini imedaiwa kuwa Ajib ataendelea kubaki Yanga
akitarajiwa kusaini mkataba mpya muda wowote kuanzia jana jioni.

Mmoja wa vigogo wa Yanga aliliambia BINGWA akisema:
“Hakuna ukweli wowote, Ajib hajasaini mkataba Simba, ni kweli alitaka kwenda TP
Mazembe, lakini wameshindwana na anarejea nyumbani Yanga. Muda wowote anasaini
mkataba mpya.”

Akizungumzia sarakasi ya mchezaji huyo katika suala
zima la usajili wake, Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera, aliliambia BINGWA jana
akisema ni vema Ajib angeenda TP Mazembe kuliko hata kubaki Jangwani au kwenda
Simba.

“Hakuna kinachomuweka Ajib Tanzania, anatakiwa
kwenda kucheza nje kwani ni mchezaji mwenye kipaji, anatakiwa kuongezewa baadhi
ya vitu, kule angeweza kujitangaza zaidi.

“TP Mazembe wapo juu, hata vifaa tu vya mazoezi
wametuzidi, unabaki vipi Tanzania wakati hakuna cha maana hapa? Kama anapenda
anavyotajwa na kuandikwa kwenye magazeti, sawa… lakini anatakiwa kifikiria mara
mbili,” alisema Zahera.

Kocha huyo alisema kama angekuwa ni baba yake Ajib,
angemshauri kuikubali ofa hiyo ya TP Mazembe kuliko kubaki Tanzania.

 “Kama
ningekuwa mshauri wake, kama baba, basi ningemwambia aende TP Mazembe, kule
atapata changamoto mpya, zingeweza kumsaidia,” alisema.

Alisema kitu pekee kinachokera kwa Ajib ni uvivu na kutojituma
kwake, akiamini kama mkali huyo wa ‘asisti’ angeenda Mazembe, angebadilika
kwani kule hakuna staa kama ilivyo Yanga kwani kujituma kwa mchezaji ndiko
kunakomfanya ajulikane.

Alisema kama Ajib atasajili Yanga, kwake itakuwa ni
sawa na iwapo akiondoka na kwenda Simba au kokote kule, pia ni poa tu.

Ajib mwenye umri wa miaka 22, ameitumikia Yanga kwa
misimu miwili akitokea Simba, lakini tangu ametua Jangwani, hajawahi kutwaa taji
lolote.

Share.

About Author

Leave A Reply