Sunday, August 18

Uchaguzi Mkuu Yanga… Waliokatwa waitwa

0


NA ZAITUNI KIBWANA

SIKU chache baada ya wagombea wa nafasi za ujumbe
katika Uchaguzi Mkuu wa Yanga, Hussein Nyika na Sumuel Luckumay kuenguliwa
kwenye mchakato huo, Kamati ya Uchaguzi ya timu hiyo imetangaza wote waliopigwa
panga kwenda kukata rufaa.

Nyika, Luckumay, Thobias Lingalangala pamoja na Siza
Limo ni kati ya waliopigwa panga kwenye uchaguzi huo baada ya kuwekewa
pingamizi linalotokana na kushindwa kuwasilisha mapato na matumizi  kwa kipindi chote walichokaa madarakani.

Akizungumza na BINGWA jana, Mjumbe wa Kamati ya
Uchaguzi Yanga, Said Mlotwa, alisema wagombea wote ambao hawataridhika na
uamuzi wa kuondolewa wanakaribishwa kukata rufaa.

“Tuna siku tano za kupokea rufaa zilizoanza juzi na yeyote
ambaye hajaridhika na uamuzi wa kuondolewa aende kukata rufaa,” alisema Mlotwa.

Alisema baada ya kupokea rufaa hizo kama zitakuwapo
watazipeleka kwenye Kamati ya Uchaguzi ya Rufaa ya Shirikisho la Soka Tanzania
(TFF).

“Sisi hatuna kamati inayoweza kusikiliza rufaa,
zitapelekwa TFF ambapo tunashirikiana nao kwa ajili ya kufanikisha uchaguzi
huu,” alisema Mlotwa.

Uchaguzi huo umepangwa kufanyika Mei 5, mwaka huu
ambapo wagombea watano wanataka kurithi nafasi ya aliyekuwa Mwenyekiti, Yussuf
Manji aliyejiuzulu.

Wagombea hao wanaowania nafasi ya mwenyekiti ni Dk.
Mshindo Msolla, Elias Mwanjala, Dk. Jonas Tiboroha, Mbaraka Igangula na Erick
Ninga.

Nafasi ya Makamu Mwenyekiti inawaniwa na Frederick
Mwakalebela, Janet Mbena, Yono Kevela, Titus Osoro na Salum Chota.

Baadhi ya wagombea 25 wanaowania nafasi ya ujumbe wa
Kamati ya Utendaji ya Yanga ni Dominick Albinus, Saad Mohamed Khimji, Hassan
Yahya Hussein, Shafiru Amour Makosa, Mhandsi Bahati Faison Mwaseba, Hamad
Islam, Mhandisi Leonard Marangu, Suma Mwaitenda na Haruna Hussein Batenga.

Share.

About Author

Leave A Reply