Tuesday, August 20

Ubingwa wa Simba umetoka kwa Adel Zrane

0


UNA AYOUB HINJO

PONGEZI kwa kikosi cha Simba kufanikiwa kutetea taji la Ligi Kuu Tanzania Bara, ilikuwa safari ndefu kwao, hasa mwezi mmoja huu baada ya kucheza michezo zaidi ya 10, wala si kazi rahisi.

Ni rahisi kuona kila kinachoendelea katika kikosi cha Simba wanapokuwa uwanjani, wanacheza soka safi, wachezaji wazuri na wenye uwezo wanaunda timu hiyo huku wakiongozwa na kocha mwenye uwezo mkubwa raia wa Ubelgiji, Patrick Aussems.

Kwa upande mwingine, ni rahisi kuwaona akina Meddie Kagere, Emmanuel Okwi, Clatous Chama, John Bocco, Haruna Niyonzima na wachezaji wengine wakitawala katika kurasa za mbele za magazeti ya michezo hapa nchini.

Unajua kwanini? Sababu ni wachezaji ambao wamekuwa wakifanya vizuri tangu mwanzo wa msimu mpaka walipofikia.

Lakini pamoja na mafanikio ambayo yamepatikana ndani ya kikosi hicho chenye maskani yake Mtaa wa Msimbazi, Kariakoo, kuna mtu amesimama nyuma yao ambaye alikuwa chachu kwa kikosi kizima.

Ukimtoa kocha mkuu, katika benchi la ufundi la Simba yupo kocha na mtaalamu wa viungo na lishe raia wa Tunisia, Adel Zrane.

Adel ana leseni ya juu ya ukocha/utaalamu wa eneo hilo, akitambuliwa na Shirikisho la Soka Ulaya, UEFA, huku akiwa na elimu ya Shahada ya Uzamivu (PhD) ya masuala ya lishe na viungo.

Mtaalamu huyo kutoka Tunisia alianza kazi yake katika kikosi cha Simba wakati wa maandalizi ya msimu huu nchini Uturuki, huko ndiko timu hiyo ilipoanza kujengwa.

Kwanini Adel amechangia kupatikana kwa ubingwa msimu huu kwa kiasi kikubwa? Inawezekana hilo ni sehemu ya swali ambalo unajiuliza.

Pengine wale mashabiki wa Simba wanaoingia uwanjani au kuangalia mpira kupitia televisheni walikuwa wanajiuliza kazi yake kubwa ni nini kwenye benchi la ufundi la kikosi hicho?

Lakini kwa ufahamu zaidi, Adel kazi yake ni kuhakikisha wachezaji wanakuwa fiti muda wote wa msimu ili waweze kumudu mifumo au mbinu za kocha wao katika mashindano mbalimbali.

Si kazi rahisi hata kidogo kuandaa programu nzima ya mazoezi kwa kikosi hicho, huku upande wa pili akiwa msimamizi mkuu wa masuala ya lishe ndani ya timu hiyo.

Baada ya Simba kutolewa na TP Mazembe katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, walicheza michezo 14 ndani ya siku 35, mpaka wanatangaza ubingwa dhidi ya Singida United.

Simba walicheza michezo hiyo ndani ya saa 24, 48 hadi 72, lakini kama si uwepo wa Adel, kuna uwezekano mambo yangekuwa tofauti, pengine ingekuwa timu ambayo ina majeruhi wengi au wachezaji wangekuwa hoi kwa uchovu wa kucheza mechi nyingi mfululizo.

Labda ingeleta hali tofauti ndani ya kikosi hicho, ambacho katika michezo hiyo wamepoteza miwili tu dhidi ya Kagera Sugar, huku wakigawana pointi mara moja na Azam.

Adel ameifanya kazi yake vizuri ndani ya Simba kwa kuwajenga wachezaji kuwa tayari wakati wote watakapohitajika na kocha wao.

Tukitoa uwezo wa wachezaji wa Simba, Adel amefanya kazi kubwa kwa kuwafanya kuwa tayari kwa wakati wote, ukizingatia wala hakukuwa na shida yoyote pindi Aussems alipofanya mabadiliko ya nyota wake, iwe kwa kuwapumzisha au kuwaweka benchi.

Maisha ya wachezaji wetu wengi hayapo salama kutokana na kuishi katika mazingira hatarishi, yaani kimazoezi wanaweza kufanya, lakini bila kuwa na mtu maalumu wa kusimamia au vyakula wanavyokula, inaweza kuwaletea matatizo. 

Mabadiliko ambayo yametokea ndani ya Simba yawe chachu kimaendeleo katika soka la Tanzania kwa timu nyingine kuanza kufikiria kuajiri makocha wenye taaluma kama ya Adel.

Share.

About Author

Leave A Reply