Sunday, August 18

TFF wamjia juu Zahera

0


NA HUSSEIN OMAR

RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace
Karia, amemtaka Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera, kwenda kituo cha polisi na kutoa
ushahidi wa madai anayolalamika kila mara kuhusiana na shirikisho hilo.

Kauli hiyo ya TFF imekuja baada ya Zahera kulishutumu
shirikisho hilo kila mara kuwa linawahujumu na mara nyingine kudai kuwa
kumekuwa na matendo ya rushwa kwa waamuzi kwa mechi zao walizopoteza dhidi ya
Stand United, Simba, Lipuli FC na Mtibwa Sugar.

Malalamiko mengine ya Zahera ni juu ya TFF na Bodi ya Ligi
kuwa wanawabeba wapinzani wao, Simba kwa kuwatengezea mazingira ya kutwaa
ubingwa msimu huu kutokana na kuwa na viporo vingi.

Alisema japo timu yake ilikuwa haipewi nafasi kubwa ya
kutwaa ubingwa msimu huu, lakini walijikuta wanakatishwa tamaa na waamuzi
wanaochezesha mechi zao.

“Unajua mshindi apatikane kihalali, mara nyingi
nimekuwa nikikatishwa tamaa na jinsi waamuzi wanavyochezesha mechi zetu pamoja
na ratiba mbovu ya ligi. Hakuna haki na kungekuwa na haki nina uhakika
tungekuwa tushajihakikishia ubingwa,” alikaririwa Zahera.

Akizungumza na BINGWA juzi, Karia amesema wao kama
viongozi waliopewa dhamana ya kuongoza soka hapa nchini hawana sababu ya
kupigizana kelele na kocha huyo wa Yanga na kuagiza kama ana ushahidi na
masuala ya rushwa na malalamiko mengine aende polisi kushtaki.

“Sisi tupo ‘bize’ bwana na michuano ya vijana ya Afcon
(Kombe la Mataifa ya Afrika ya vijana chini ya umri wa miaka 17), hivyo hayo malalamiko
yake apeleke polisi na ushahidi alionao,’’ alisema Karia.

Alisema katika uongozi wake suala la kupigizana kelele
na makocha au viongozi wa soka halipo, bali yeye anaangalia ni njia gani
zinaweza kuleta maendeleo ya mchezo huo wa soka hapa nchini.

“Tukimsikiliza kila mtu tutakuwa hatufanyi kazi, anayeongea
mwacheni aongee lakini sisi tunajua nini tunachokifanya katika kuundeleza
mchezo wa soka,” alisisitiza Karia.

Share.

About Author

Leave A Reply