Sunday, August 18

TAIFA STARS TUPO NYUMA YENU – Bingwa

0


TIMU ya soka ya Taifa, Taifa Stars, itashuka dimbani kumenyana na DR Congo katika mchezo wa kirafiki utakaochezwa katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Mchezo huo utachezwa baada ya ule wa nchini Algeria ambako Taifa Stars ilifungwa mabao 4-1 kutoka kwa wenyeji wao hao.

Licha ya kwamba ulikuwa ni mchezo wa kirafiki, matokeo hayo yalionekana kuwagawa mashabiki wa soka baadhi wakiwatupia lawama wachezaji na wengine kocha wa timu hiyo, Salum Mayanga, kwa kuwa walionyesha udhaifu katika kujipanga.

Tunaamini kwamba kila shabiki wa Tanzania alipenda kuona Taifa Stars ikishinda na haikuwa na sababu kuwatupia lawama wachezaji na benchi la ufundi la Stars.

BINGWA tunaamini Algeria ni moja kati ya timu bora barani Afrika, hivyo kufungwa kwa Taifa Stars kusisababishwe kuwakatisha tamaa wachezaji wetu.

Taifa Stars inatarajia kucheza na DR Congo inayoshika nafasi ya 39 duniani katika viwango vya Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), hivyo Taifa Stars ina kazi kubwa ya kuhakikisha wanapata matokeo mazuri.

 

Tunasema kwamba, Taifa Stars inahitaji ushindi katika mchezo huo ikizingatiwa  kumekuwa na mwendelezo wa kutofanya vizuri katika mashindano ya kimataifa.

Kufanya vibaya katika mashindano ya kimataifa kunaifanya Tanzania kuendelea kushika nafasi mbaya katika viwango vya Fifa, kwa sasa ikiwa ya 146, hivyo kupoteza dhidi ya DR Congo kunaweza kutushusha zaidi.

BINGWA tunasema licha ya DR Congo kushika nafasi ya 39 katika viwango vya Fifa, si timu ngumu kwa Taifa Stars kutokana na rekodi za timu hizo.

Kumbukumbu zinaonyesha kwamba,  Taifa Stars na DR Congo zimekutana mara tano michezo ya kirafiki na mashindano mbalimbali na Stars  kuibuka na ushindi mara mbili na kutoa sare moja.

Kutokana na rekodi hizo, tunaamini kwamba wachezaji wakijituma katika mchezo wa leo wanaweza kuwapa raha mashabiki pale watakapoondoka na ushindi.

BINGWA na Watanzania tupo nyuma ya Taifa Stars kuhakikisha tunaishangilia ili kuiwezesha kufanya vizuri katika mchezo huo.

Kila la heri Taifa Stars

The post TAIFA STARS TUPO NYUMA YENU appeared first on Bingwa.Read More

Share.

About Author

Comments are closed.