Friday, May 24

Solskjaer akiiba kengele aweke pamba masikioni

0


NA AYOUB HINJO

NI kwenye matatizo pekee ndipo mwanadamu
hufahamu nguvu na uwezo ulio ndani yake.

Usiyachukie wala usichukie kwanini wewe
umepata tatizo, Mungu hajawahi kumpa mja mzigo asioweza kuubeba. Linapokuja
tatizo, furahi, kwa maana wakati wako wa kuigundua nguvu iliyo ndani yako
umewadia.

Mwandishi wa vitabu Mmarekani, Hellen Keller,
akiwa na miezi 19 tu duniani, alipata ulemavu wa macho na masikio.

Hakuweza kuona wala kusikia chochote tena kwa
miaka 87 aliyoishi duniani tangu Juni 27, 1880 alipozaliwa kule Alabama, Marekani.
Ni kupitia tatizo hilo, leo dunia inamkumbuka Hellen kama mlemavu wa kwanza wa
macho na masikio duniani kupata digrii ya sanaa.

Kwa ukaribu zaidi ifikirie Manchester United
ile ya Sir Alex Ferguson kwa kipindi chote alichoifundisha timu hiyo.

Hakuna kingine zaidi ya kuitaja kama moja ya
timu kubwa katika uso wa dunia hii, waliishi katika pepo yao kila walilolifanya
liligeuka kuwa dhahabu.

Ukiziweka kando Real Madrid na Barcelona,
wale Manchester United ilibaki kuwa moja ya timu za ndoto kwa wachezaji wengi
katika kila kona ya ulimwengu.

Iwe America, Afrika, Ulaya na kwingineko
ambako kunatengeneza mabara saba katika ulimwengu huu, hiyo ndiyo ilikuwa
Manchester United.

Miaka sita tangu Ferguson apunge mkono wa
kwaheri, kila kitu kinaonekana kubadilika kwa kasi kubwa ya ajabu pengine
kuliko hata mbio za Hussein Bolt.

Imekuwa timu ya kawaida zaidi, kwa kifupi
limebaki jina na historia yao ya kuvutia ambayo ilijengwa kwa miaka 26 ya kocha
huyo mkongwe aliyeamua kukaa kando.

Tayari makocha wanne wamepita, yaani David
Moyes, Ryan Giggs aliyefundisha kwa muda mfupi, akaja Louis van Gaal, kisha
msema ovyo Jose Mourinho, wote hao walifunguliwa mlango wa kutokea.

Wote wanne waliishi kwa mashaka makubwa,
kuanzia Carrington mpaka Old Trafford palikuwa pagumu kwao, tena cha kushangaza
hakuna ambaye alibahatika kufundisha timu hiyo kwa miaka mitatu.

Pamoja na yote, kuanzia kwa Moyes mpaka
Mourinho wote lawama zao wamezituma kwa uongozi ambao unaongozwa na Ed Woodward
kwa kushindwa kutekeleza mahitaji yao.

Pengine kila mmoja atawaangalia katika sura
ya usajili ambao walifanyiwa na mabosi hao, japo ni kundi kubwa la wachezaji
wenye viwango vya kawaida walisajiliwa ndani ya Manchester United.

Kikubwa ambacho kinawaumiza wengi ndani ya
kikosi hicho ni makocha kushindwa kuwa na kauli ya mwisho kwenye timu, uongozi
ndio unaamua kila kitu.

Kingine kikubwa ambacho kinatoa hukumu kwa
makocha wa Manchester United ni kile kizazi cha mwaka 1992, ndio mafanikio ya
timu hiyo asilimia 70 yalikuwa katika miguu yao.

Ukifungulia Sky Sports unamwona Paul Scholes
akiongea, ukiweka BT Sports utawaona akina Gary Neville wakikosoa, wamekuwa na
midomo ambayo kwa kiasi fulani inaakisi kilichopo ndani ya timu yao pendwa.

Kwa kipindi chao chote hawakukutana na kadhia
hiyo, wanaamini wachezaji wanaoingia United sasa hivi wanafuata pesa,
inawezekana kwa upande mwingine.

Desemba mwaka jana, Manchester United
walimtimua Mourinho na nafasi yake aliichukua Ole Gunnar Solskjaer, mchezaji wa
zamani wa kikosi hicho.

Kama ilivyo kwa makocha wengine waliopita
hivi karibuni, hata Solskjaer naye alikuwa na mwanzo mzuri, tena kuliko hata
Ferguson.

Mambo yalionekana kumnyookea kama kumsukuma
mlevi kwenye mtaro wa maji au mteremko mkali, vijana wa mitaa wanakwambia breki
zimekata.

Lakini katika miezi miwili tangu apewe
mkataba mambo yalibadilika, kila kilicho kizuri kilipotea, mabaya yalichukua
nafasi, hakuna kinachoeleweka kwao.

Imekuwa kawaida Manchester United kuwa na
malengo ya kumaliza ndani ya ‘top four’ tangu Ferguson alipoondoka na ubingwa
wake wa mwisho wa Ligi Kuu.

Kwa jicho la tatu, tatizo la kawaida
linaanzia juu kisha kushuka chini kwa wachezaji, yaani tuanzie kwa Woodward
mpaka kwa akina Paul Pogba.

Solskjaer ataanza msimu ujao akiwa katika
benchi hilo, tayari ameshapiga mkwara mzito wachezaji wake kujitunza katika
likizo yao.

Hivi karibuni ameongea mambo mengi ambayo
kama yakifanikiwa, basi historia itaandikwa, pengine hataki kuwa kama Liverpool
ambao walikaa miaka mingi kama timu ya kawaida.

Kwa kila kinachoendelea ndani ya Manchester
United, Solskjaer hana budi kusimama katika misingi aliyojiwekea japo hana
sauti ya kuamua kila kitu kama ilivyokuwa kwa Ferguson.

Wala hana tofauti na mwizi wa kengele, ili
aweze kukimbia au kuondoka nayo inabidi aweke pamba masikioni, asisikie jinsi
inavyojigonga. Unajua kwanini?

Kwa ufupi tu, itamkatisha tamaa na anaweza
akaitupa kwa kuhofia kukamatwa, Solskjaer ana kazi kubwa sana ndani ya
Manchester United.

Aweke pamba masikioni kukwepa sauti za akina
Scholes na Neville, ikiwezekana azime na macho kutosoma kila kinachoandikwa
kuhusu timu yake mitandaoni au magazetini.

Kila mmoja anaisubiri Manchester United msimu
ujao, dunia nzima inasubiri.  

Share.

About Author

Leave A Reply