Monday, March 18

Simba yatikisa kwa Mfalme Mswati

0


*Mbelgiji awataka Mbanane kijianda kuzimia

NA ZAITUNI KIBWANA

KIKOSI cha Simba kimeitikisa Swaziland baada ya kutua nchini humo jana tayari kwa mchezo wao wa marudiano wa hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mbabane Swallows, utakaopigwa kwenye Uwanja wa Mavuso.

Mara baada ya kuwasili nchini humo wakitokea Afrika Kusini walikoweka kambi ya siku mbili, mashabiki wa soka wa Swaziland ya Mfalme Mswati, walikuwa wakiwashangaa wachezaji wa Simba, wakiwa na kumbukumbu jinsi Wekundu wa Msimbazi hao walivyoisambaratisha Mbabane kwa kuichapa mabao 4-1 wiki iliyopita.

Matokeo hayo ya mchezo huo uliochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, yameiweka Mbabane katika wakati mgumu wa kusonga mbele, wakitakiwa kushinda zaidi ya mabao 3-0 leo wakiwa kwao.

Mchezo huo wa leo unatarajiwa kuanza saa 9:30 kwa saa za huko, sawa na saa 10:30 jioni kwa Afrika Mashariki, ukichezeshwa na mwamuzi, Nelson Emile Fred, atakayesaidiwa na Hensley Danny Petrousse na Gerard Pool, wote wa Shelisheli.

Simba SC itakuwa na kazi nyepesi leo ikihitaji hata sare kusonga mbele kwenye michuano hiyo mikubwa kabisa kwa ngazi ya klabu barani Afrika.

Kikosi cha Simba kinachonolewa na Mbelgiji, Patrick Aussems, jana kilifanya mazoezi ya mwisho kabla ya mchezo huo wa leo, huku wachezaji wakiwa na ari kubwa ya ushindi.

Tayari Aussems ameweka wazi mchezo huo kuwa mgumu kwao kwani wapinzani wao watakaokuwa wakicheza kwao, watabadilika, lakini akiahidi vijana wake kupata matokeo mazuri na kusonga mbele.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wachezaji wa Simba wakiongozwa na nahodha, John Bocco, walisema kikosi chao kina hali nzuri na wamejipanga kufanya vizuri.

“Tumejipanga kufanya vizuri na kusonga mbele hatua inayofuata, kila mmoja anatambua jukumu lililotuleta huku ni ushindi hakuna kitu kingine zaidi ya ushindi,” alisema Bocco.

Naye beki Pascal Wawa, amewataka nyota wenzake kucheza kwa kujitoa na kuwajibika kwenye eneo lake, ili kuhakikisha wanaibuka na ushindi mnono.

Kikosi cha Simba leo kinatarajiwa kuundwa na Aishi Manula,  Erasto Nyoni, Mohammed Hussein, James Kotei, Pascal Wawa, Jonas Mkude, Emmanuel Okwi, Cletus Chama, Meddie Kagere, John Bocco na Shiza Kichuya.

Iwapo Simba itasonga mbele, itakutana na mshindi kati ya Nkana ya Zambia anayocheza Mtanzania, Hassan Kessy na kikosi cha UD Songo ya Msumbiji.

Wakati huo huo, mwandishi wetu, Mwamvita Mtanda, anaripoti kuwa Aussems ametamba kumshangaza Kocha Mkuu wa Mbabane Swallos, Kinnah Phiri, kwa kumfunga akiwa kwao.

Mara baada ya mchezo wa kwanza uliopigwa Dar es Salaam, Phiri alitamba kulipiza kisasi watakapovaana na Simba leo wakiwa kwenye uwanja wao wa nyumbani.

“Baada ya mechi ya kwanza, nilisoma haraka mapungufu ya wachezaji wangu na kuyafanyia marekebisho, wapo vizuri sana, Mbabane wasitarajie ushindi, hawana nguvu ya kutufunga mabao hata kama tupo kwao tutawafunga tu,” alisema Aussems.

Aussems alisema tangu anatua Simba, mipango yake ilikuwa kuifikisha timu hiyo mbali zaidi katika anga ya kimataifa na tayari ameianza safari yake hiyo, akiamini atafanikiwa katika hilo.

Share.

About Author

Leave A Reply