Saturday, August 24

Simba wajanja aisee

0


*WAMVITA MTANDA

VIONGOZI wa Simba ni wajanja sana asikwambie mtu,
kwani wakati wenzao wa Yanga wakionekana kuwa na mzuka wa usajili wa wachezaji,
hasa wa kigeni, wao wamepozi wakipanga kuibuka kwa kishindo kitakachowaacha
midomo wazi mashabiki wao.

Msimu huu Simba ilikuwa na kikosi cha nguvu
kilichosheheni wachezaji wazoefu na wenye viwango vya juu, wakiwamo wa ndani na
wa kigeni ambao mwisho wa siku, wameiwezesha timu hiyo kufika robo fainali ya
Ligi ya Mabingwa Afrika na kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Wakifahamu kuwa msimu ujao watashiriki michuano hiyo
ya Afrika, Simba wamepanga kufanya usajili kwa utulivu wa hali ya juu
kuhakikisha wanawanasa wachezaji bora zaidi ili kuongeza nguvu kwa wale
watakaowabakiza.

Hivyo pamoja na Yanga kuanza kwa kasi mchakato wa
usajili, wao wameendelea kupiga hesabu wakipanga kuitikisa nchi kwa kushusha
wachezaji wa kiwango cha juu kwa gharama yoyote ile.

Katika kile kilichoonekana ‘kuwa-beep’ wapinzani
wao, Simba wanatarajiwa kushusha nchini kiungo mshambuliaji hatari wa klabu ya
KCCA aliyeiwezesha kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya nchini kwao Uganda.

Mchezaji huyo si mwingine, bali ni Sadam Ibrahim Sadam,
ambaye anatarajiwa kutua nchini muda wowote kuanzia sasa.

Akizungumza na BINGWA jana, mmoja wa viongozi wa
Simba, alisema wamepanga kuwa watulivu mno katika suala zima la usajili.

“Hatutakurupuka katika usajili, tumepanga kuwa makini
sana kwani lengo letu ni kusajili wachezaji wazuri zaidi ya hawa tulionao ili
msimu ujao tuweze kufanya vizuri zaidi ya msimu huu katika michuano ya Afrika,”
alisema kiongozi huyo.

Alipoulizwa juu ya Sadam, alisema: “Kuna mchezaji
nimeambiwa anatoka KCCA ya Uganda, lakini bado sijafahamu jina lake, ila
nimeambiwa ni kiungo, akifika tutawajulisha.”

Aliwataka mashabiki wa Simba kutobabaishwa na
usajili aliouita wa pupa unaofanywa na watani wao Yanga, akitamba muda ukifika,
wanaweza kushusha vifaa vya nguvu hata saba ndani ya saa 24 tu.   

Share.

About Author

Leave A Reply