Monday, March 25

SIMBA UTEMI HADI UGENINI

0


*Watua kibabe Sauzi, wapewa heshima ‘bab kubwa’

*Mbelgiji atembea na jina la Mo mfukoni

NA ZAITUNI KIBWANA

KIKOSI cha Simba, kimetua kibabe nchini Afrika Kusini na kupata mapokezi ya heshima kubwa kutoka kwa mashabiki wao wanaoishi huko, wakiwa njiani kuelekea Swaziland kuifuata Mbabane Swallows kucheza nao mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

Mchezo huo ni wa hatua ya awali ambapo katika ule wa kwanza uliochezwa wiki iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Simba ilishinda mabao 4-1, hivyo kujiwekea mazingira mazuri ya kusonga mbele.

Wakifahamu kuwa hali ya hewa ya Afrika Kusini ni sawa na ile ya Swaziland, Simba waliona ni vema kujichimbia katika nchi hiyo kujifua kwa siku mbili kabla ya kuwafuata wapinzani wao hao watakaocheza nao kesho kwenye Uwanja wa Mavuso uliopo eneo la Manzini, Swaziland.

Katika jambo la kufurahisha zaidi, msafara mzima wa Simba ulipewa heshima kubwa na mashabiki wao waliowapokea ambao ni wenyeji Afrika Kusini, wakionekana kuvutiwa na ushindi mnono walioupata Wekundu wa Msimbazi hao wiki iliyopita.

Akizungumza na BINGWA jana kutoka Afrika Kusini, Meneja wa Simba, Abbas Suleimani, alisema msafara wao uliongozwa na Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi, Mulamu Nghambi na kwamba waliwasili nchini humo saa 12:12 mchana jana na kuweka kambi kwenye Hoteli ya Lugogo Sun.

Alisema mapokezi waliyoyapata ni deni kwa wachezaji wao kwani watatakiwa kupambana ili kupata ushindi ambao ndio kiu ya mashabiki wao ambao wamekuwa wakiwaunga mkono.

“Tunashukuru kwa mapokezi tuliyopata, hii ni heshima kwetu, mapokezi haya wanatupa ishara kuwa wanataka matokeo mazuri kwenye mchezo huo, wachezaji wanatakiwa kujituma ili kuhakikisha tunalipa fadhila.

“Wachezaji wote wana morali ya juu, tumekuja kwa ajili ya kutafuta ushindi ili tufuzu hatua inayofuata na si vinginevyo, tulikuwa na wakati mzuri wa kujiandaa katika kambi yetu jijini Dar es Salaam, tulikuwa eneo tulivu ambalo kocha alitumia kuwaongezea wachezaji mbinu za ushindi, lengo letu ni kuchukua ubingwa wa michuano hii,” alisema Suleimani.

Aliongeza: “Wachezaji watapumzika kidogo leo (jana), kutokana na uchovu wa safari, lakini kesho (leo) tutafanya mazoezi ya mwisho katika uwanja utakaochezewa mechi kabla ya kukabiliana na Mbabane Swallows Jumanne,” alisema Suleimani.

Kwa upande wake, Kocha Mkuu wa Simba, Mbelgiji Patrick Aussems, alisema wameenda Afrika Kusini kwa ajili ya kusaka ushindi licha ya kukiri mchezo huo utakuwa mgumu.

“Bado hatujamalizana na hawa Mbabane Swallows, hatuwezi kuwadharau isipokuwa tutapambana kuhakikisha tunashinda tena uwanja wa ugenini,” alisema.

Kwa upande wake, nahodha wa Simba, John Bocco, alisema: “Nawaheshimu Mbabane, bado tunakumbuka yale mabao 4-1, ila si sababu ya kubweteka, tutaingia uwanjani kupambana.”

Ili kusonga mbele, Simba wanahitaji ushindi au sare yoyote na kwamba iwapo Wekundu wa Msimbazi hao watavuka, watakutana na mshindi kati ya Nkana ya Zambia anayocheza Mtanzania, Hassan Kessy au UD Songo ya Msumbiji.

Share.

About Author

Leave A Reply