Sunday, August 25

Shimivida waja na bonge la bonanza la michezo

0


NA MICHAEL MAURUS

HAKUNA ubishi, michezo imekuwa ni sehemu muhimu mno
katika ustawi wa jamii kwani pamoja na kuimarisha afya ya washiriki, lakini pia
ni ajira inayolipa mno.

Zamani michezo haikuwa ikichukuliwa kama ajira,
badala yake washiriki walilenga kuimarisha afya zao na kutoa burudani.

Lakini kadiri miaka ilivyozidi kwenda, michezo
imegeuka kuwa chanzo cha ajira, tena inayolipa mno.

Michezo ambayo imekuwa ikiongoza kwa kutoa ajira kwa
washiriki ni soka, ndondi, gofu, mpira wa kikapu, tenisi, mieleka na mingineyo.

Kwa hapa nchini, wapo wanamichezo ambao walibadili
maisha yao kwa kiasi kikubwa kutoka ya hali ya chini hadi kuwa matajiri baada
ya kufanya vema, hasa katika ngazi ya kimataifa.

Miongoni mwa wanamichezo hao ni mwanariadha, Filbert
Bayi na wenzake wa kizazi chake, lakini pia akiwamo mwanasoka Mbwana Samatta
anayetamba Ulaya kwa sasa, mwanariadha Samson Ramadhani na wengineo.

Ni kutokana na kufahamu hilo, watu wa rika, jinsia
na hali mbalimbali wamekuwa wakijikita katika michezo ili kuvitendea haki
vipaji vyao na mwisho wa siku, kuona kama wanaweza kuboresha maisha yao kupitia
sekta hiyo.

Vijana wenye ulemavu wa kusikia yaani viziwi wa Dar
es Salaam, wameanzisha Shirikisho la Michezo la Mkoa huo (Shimivida) ili kuibua
na kuendeleza vipaji katika michezo mbalimbali na kuvitangaza.

Juzi uongozi wa Shimivida ulitembelea ofisi za New
Habari (2006) Limited zilizopo Sinza Kijiweni, Dar es Salaam ambazo ni
wazalishaji wa magazeti ya BINGWA, DIMBA, MTANZANIA na RAI ili kuzungumzia
mkakati wao wa kuibua vipaji vya michezo na kuviendeleza.

Katika mahojiano na mwandishi wa makala haya,
Mwenyekiti wa Shimivida, Jamal Mbaraka, anasema shirikisho lao hilo
lilianzishwa mwaka 2001 na kwamba hadi sasa lina wanachama zaidi ya 600.

Anawataja viongozi wenzake kuwa ni Seleman Zalala
(Makumu Mwenyekiti), Frida Mkumbo (Katibu), Mselem Maona (Katibu Msaidizi),
Anna Gugu (Mweka Hazina) na Mbwana Athuman (Mweka Hazina Msaidizi).

Katika kulitangaza shirikisho lao, wameandaa bonanza
la michezo mbalimbali linalotarajiwa kufanyika baada ya Mwezi Mtukufu kwenye
viwanja vya Leaders Club, Dar es Salaam.

“Bonanza hilo litashirikisha michezo ya soka, netiboli,
riadha, mpira wa kikapu, voliboli, riadha na kuvuta kamba,” anasema.

Anasema wanatarajia bonanza hilo litashirikisha
wanamichezo zaidi ya 500 kutoka wilaya zote tano za Dar es Salaam, yaani Ilala,
Kinondoni, Kigamboni, Temeke na Ubungo.

“Wilaya zote za Dar es Salaam zitashiriki kwani nako
kuna viongozi wao ambao tunaendelea kuwapa taarifa,” anasema Mbaraka ambaye ni
miongoni mwa wanafunzi waliopata elimu ya sekondari, Ruvu Sekondari iliyopo
Mlandizi mkoani Pwani.

Anasema pamoja na kuanza maandalizi ya bonanza hilo,
lakini hadi sasa hawajapata mdhamini, wakiwaomba wadau kujitokeza kuwapa sapoti.

Kwa upande wake, Katibu wa Shimivida, Frida, anasema
bajeti ya bonanza hilo ni Sh 10,000 na kwamba vitu wanavyovihitaji ni mipira,
jezi, vinywaji, maturubai, viti, waamuzi, huduma ya kwanza, ulinzi na
vinginevyo.

“Nitoe wito kwa Serikali, Shirikisho la Michezo la Viziwi
Taifa na jamii kutupa sapoti ili tuweze kufanikisha bonanza hili.

“Kwa muda mrefu tumekuwa tukitengwa katika michezo
japo wapo viziwi wenye vipaji ambao wanaweza kufanya vizuri hadi ngazi ya
kimataifa na kuliletea sifa Taifa,” anasema Frida.

Share.

About Author

Leave A Reply