Friday, August 23

Shabiki wa Man City alivyopata dili la kuja Tanzania kwa kuzungumza Kiswahili

0


NA JONATHAN TITO

WAZIRI wa Utalii na Mali Asili
Tanzania, Dk. Hamisi Kigwangala, amempa ofa ya kuja nchini shabiki mkubwa wa
Manchester City, Braydon Bent kwa gharama za serikali baada ya mtoto huyo wa
miaka 10 kupenda kuzungumza Kiswahili.

Kupitia mtandao wake wa Instagram,
Kigwangala aliweka video ya Braydon akizungumza Kiswahili na kutaja Mbuga za Serengeti,
Ngorongoro na Mlima Kilimanjaro na kumkaribisha Tanzania.

“Mimi kama Waziri wa Utalii na Mali Asili
napenda kukukaribisha Tanzania kwa gharama zetu na kukufanya kuwa balozi wetu,
nitafurahi kama utakubali ombi langu kupitia namba zangu,” aliandika
Kigwangala.

Katika video hiyo, Braydon, alisema:
“Mambo vipi Tanzania, habari za Serengeti, Ngorongoro na Kilimanjaro, mimi na
rafiki yangu John Jackson ‘JJ’ nawatakia mapumziko mema.”

Lakini hiyo si video pekee ya Braydon
kuzungumza Kiswahili, kabla hiyo ya kutaja mbunga za Tanzania na Mlima
Kilimanjaro aliweka video nyingine akizungumza Kiswahili na kuwatakia
Watanzania wote Siku Kuu njema ya Pasaka.

Katika mchezo wa robo fainali ya Ligi
ya Mabingwa Ulaya kati ya timu yake ya Man City na Tottenham, Braydon pia
alizungumza Kiswahili wakati anazungumzia mchezo huo.

Braydon ambaye ni mchambuzi wa soka amekuwa
akiweka video zake kwenye mtandao wake wa Instagram na blog, alianza kupata
umaarufu mwaka 2016 baada ya kuiga staili ya kushangilia ya mshambuliaji wa Man
City, Sergio Aguero.

Julai mwaka 2016, Braydon alionekana
tena kwenye teksi mjini Manchester na Kocha wa Man City, Pep Guardiola, akiwa
ameshtukizwa bila kujua kama ndani ya taksi hiyo kutakuwa na kocha huyo.

Braydon ambaye amekuwa akitokea
kwenye mtandao wa Instagram akiwa na mama na baba yake pamoja na mdogo wake,
alifanikiwa kukutana na Aguero baada ya video yake kusambaa.

Tangu hapo umaarufu wa mtoto huyo, Braydon
ulizidi kuongezeka na kuonekana kwenye matukio mbalimbali ya Man City ikiwamo
kualikwa mazoezini, akikutana na wachezaji wa timu hiyo mara kwa mara na
kujumwishwa katika orodha ya watu maarufu.

Mtoto huyo, Braydon aliyezaliwa Machi
6, 2009 nchini England pia amejumuishwa katika orodha ya watu waliozaliwa Machi
6 wenye umaarufu mkubwa kwenye mtandao wa Instagram.

Pamoja na kuwa na umri mdogo, lakini
Braydon ameanza kupiga hela kwa kuingiza mkwanja kwa mwaka na moja ya chanzo
chake cha fedha hizo ikidaiwa kuwa ni mtandao huo wa Instagram.

Kwa mwaka huu anakadiriwa kuingiza
kuanzia dola milioni moja hadi milioni 10 (shilingi bilioni 2 hadi 22), huku
kwa mwaka jana ikiwa ni dola 100 hadi milioni moja (shilingi milioni 229 hadi
bilioni 2.

Share.

About Author

Leave A Reply