Wednesday, August 21

Samatta amtambia Ali Kiba

0


WINFRIDA MTOI

NAHODHA wa timu ya Taifa ya Tanzania, Mbwana
Samatta, ametamba kuendeleza ubabe dhidi ya timu Ali Kiba katika mechi yao ya hisani,
itakayopigwa  keshokutwa kwenye Uwanja wa
Taifa, jijini Dar es Salaam.

Samatta na msanii wa muziki, Ali Kiba, wameandaa
mechi hiyo kwa lengo la kuchangisha fedha za kusaidia watu wenye mahitaji
maalumu pamoja na shule za msingi kupitia mfuko wao wa ‘SamaKiba Foundation’.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana,
Samatta, ambaye anacheza katika kikosi cha Genk nchini Ubelgiji, alisema Kiba
ajiandae kuondoka uwanjani kichwa chini baada ya kupokea kipigo cha maana.

Alisema kipigo atakachoshusha ni zaidi ya kile
cha  mwaka jana cha mabao 4-1, ili kumwonyesha
jinsi mpira unavyochezwa na si maneno.

Samatta alisema kikosi chake kimesheheni nyota
wenye uwezo mkubwa, pamoja na yeye watahakikisha wanaisulubu timu ya Kiba ambao
wamekuwa wakiongea sana nje ya uwanja.

“Mimi siongei sana, shughuli mtaona wenyewe
uwanjani mtu atakapopigwa bao nne, sita, ninaomba mashabiki wa soka wajitokeze
kwa wingi ili kufanikisha lengo letu, kwani ujio wao ndio muhimu,” alisema
Samatta.

Kwa upande wake Kiba, alipoulizwa ataweza kulipa
kisasi kwa Samatta, alisema yupo vizuri, huku akitambia nyota wake kama Meddie
Kagere kuwa watamtoa kimasomaso.

“Sisi kazi tumemaliza, Samatta na wenzake
wajipange, wafahamu kuwa nina Kagere ndani na tumefanya mazoezi ya nguvu
kuhakikisha tunamnyamazisha,” alisema Kiba.

Alitaja viingilio vya mchezo huo kuwa mzunguko ni
Sh 2,000, VIP B 5,000 na majukwaa maalumu yanayoitwa Champion King na Champion
Samatta ni Sh 20,000.

Share.

About Author

Leave A Reply