Tuesday, August 20

Nyota Yanga waweka silaha chini

0


NA HUSSEIN OMAR

BAADA
ya wachezaji wa Yanga kugoma kufanya mazoezi juzi, jana wamefunguka na kusema
wako tayari kuanza mazoezi leo na kusema yaliyopita si ndwele na kuwataka
mashabiki wao kutokuwa na wasiwasi kwani wamerejea na mambo yote yatakuwa shwari
ndani ya klabu hiyo.

Wachezaji
wa Yanga juzi asubuhi waligoma kufanya mazoezi katika Uwanja wa Chuo cha Polisi
Kurasini, jijini Dar es Salaam wakishinikiza kulipwa mishahara yao ya miezi
mitano na fedha za usajili.

Wakati
mgomo huo ukitokea timu hiyo ipo kwenye maandalizi kabambe ya mchezo wa Ligi
Kuu Tanzania Bara dhidi ya Azam FC utakaopigwa Jumatatu ya wiki ijayo kwenye Uwanja
wa Uhuru, jijini Dar es Salaam.

Wachezaji
hao wakizungumza na BINGWA jana wakiwa mazoezini walisema, yaliyopita si ndwele
na sasa wanaangalia kinachokuja mbele yao baada ya upepo mbaya kupita.

Mshambuliaji
wa timu hiyo, Amisi Tambwe, alisema kuwa wamezika tofauti zao rasmi na sasa
kazi ni moja tu kuhakikisha wanamaliza michezo iliyobaki ya ligi salama.

“Hakuna
mgomo si umeona leo wote tumefika mazoezini, hali ni shwari kabisa wasitake
kutuchafua wachezaji wote tupo fiti sasa kazi wanayo Azam,” alisema Tambwe.

Straika
huyo aliyejiunga Yanga mwaka 2014 wakati wa usajili wa dirisha dogo akitokea
Simba, alisema suala la mishahara ni gonjwa la taifa kwani taasisi nyingi hapa
nchini zimeyumba kiuchumi.

“Suala
la mishahara ni gonjwa la taifa zima si sisi peke yetu ni kila sehemu kwahiyo
nina imani tutalipwa, kwasasa acheni kwanza tucheze mpira kwani kila ofisi sasa
hivi wafanyakazi wanalia kuhusu kuchelewa au kutolipwa mishahara yao, hivyo hali
ni ngumu sana kwahiyo hiki ni kilio cha taifa zima,’’ alisisitiza Tambwe.

Alisema
wamekubali yaishe baada ya kutakiwa kuwa wapole na viongozi wa timu hiyo katika
kipindi hiki ambacho hali ya hewa imechafuka ndani ya Yanga.

Kwa
upande wake, nahodha msaidizi wa timu hiyo ya Yanga, Juma Abdul, alisema hakuna
mgomo mambo yote sasa ni shwari kwani kila kitu kinakwenda vizuri.

“Mambo
yako poa tu na hatuna mgomo tupo kamili kwa ajili ya kuitetea timu yetu katika
mchezo dhidi ya Azam,” alisema Juma.

Lakini
kwa upande wa kocha wa timu hiyo, Mwinyi Zahera, ilikuwa tofauti baada ya kusisitiza
kuwa atawatumia wachezaji wa kikosi cha pili ambao aliwaongoza katika mazoezi
ya jana na kuongeza kuwa hilo halimpi shida kwani ana uwezo wa kumtumia
mchezaji yeyote.

“Si
unaona kama hivi leo tumefanya mazoezi na wachezaji wa kikosi cha pili hilo
halinitishi, kila mchezaji ana nafasi ya kucheza na hawa hawa ndio watacheza dhidi
ya Azam FC. Mimi ndio staa hapa hakuna mchezaji aliye juu zaidi yangu, kama
wanafikiri wao ni wakubwa kuliko timu wanajidanganya sitaki masihara,’’ alisema
Zahera.

Katika
hatua nyingine, mratibu wa timu hiyo, Hafidh Saleh, alisema wanaendelea vizuri
na maandalizi licha ya mazoezi ya leo kufanywa na wachezaji wengi wa kikosi cha
pili.

 “Maandalizi yanaendelea vizuri wachezaji wote
wana morali kama ulivyoona kilichobaki ni kazi tu hakuna kitu kingine,” alisema
Haifdh.

Wakati
mazoezi hayo yakiendelea wachezaji wa kikosi cha kwanza walikuwa wamekaa nje
kwa ajili ya kuweka mambo yao sawa kabla kesho kuendelea na program ya mazoezi.

Share.

About Author

Leave A Reply