Saturday, August 24

Nyota hawa walizingua tu EPL 2018-19

0


LONDON, England

KWA mashabiki wa soka wanatambua kuwa usajili ni kamari. Kwamba si kila mchezaji anayenunuliwa anaweza kuwa kwenye kiwango kilichotarajiwa.

Hiyo huchangiwa na sababu nyingi lakini kubwa ni mchezaji mpya kutoizoea ligi aliyohamia, hivyo kushindwa kwenye kiwango alichotoka nacho katika klabu yake ya zamani.

Si kila mchezaji anaweza kuwa na bahati ya Lucas Torreira wa Arsenal au Raul Jimenez anayeichezea Wolves, ambao licha ya kuwa huu ulikuwa msimu wao wa kwanza Ligi Kuu ya England (EPL), bado waliweza kuonesha makali yao.

Kama ni hivyo, ni wachezaji gani walitarajiwa kuwika lakini walishindwa kuonesha makali yao msimu huu wa EPL uliomalizika siku chache zilizopita kwa Manchester City kunyakua ubingwa?

Sergio Rico (Fulham)

Mlinda mlango huyo mwenye umri wa miaka 25, alitua Fulham msimu huu kwa mkopo akitokea Sevilla ambako katika mechi 170, alicheza 58 bila kuruhusu nyavu zake kutikiswa.

Hata hivyo, mambo hayakwenda vizuri kwa upande wake, ikiishuhudia timu hiyo ikishuka daraja.

Katika mechi 29 alizopewa nafasi, ni tano tu ambazo Mhispania huyo aliondoka uwanjani akiwa hajapitisha bao, akitobolewa mara 56, huku matatu yakiwa ni kwa uzembe wake.

Stephan Lichtsteiner (Arsenal)

Huyo ni beki na nahodha wa timu ya taifa ya Uswis. Alitua bure pale Arsenal akitokea Juventus, akiaminika uzoefu wake ungekuwa na msaada mkubwa kwa vijana wa Unai Emery.

Hata Hector Bellerin alipothibitika kuwa majeraha yangemweka nje ya uwanja kwa msimu mzima, bado Lichtsteiner alishindwa kujihakikishia namba mbele ya Ainsley Maitland-Niles.

Mbaya zaidi, katika mechi 14 za Ligi Kuu msimu huu, ameambulia asilimia tatu tu ya krosi zilizowafikia walengwa, wakati uzembe wake ulichangia Arsenal ifungwe bao moja.

Caglar Soyuncu (Leicester City)

Mashabiki wa Leicester City walitarajia makubwa kutoka kwake. Kwanza, ni kiwango alichokuwa nacho katika kikosi cha Freiburg. Pili, ni dau nono lililotumika kumsajili, Pauni milioni 19.

Tatu, alikuwa akigombewa na klabu kadhaa, wakiwamo wakali wa Kaskazini mwa Jiji la London, Arsenal.

Lakini sasa, aliuanza msimu huu kwa majeraha ya misuli, akikosa mechi nyingi tu. Hata baada ya kupona, ilikuwa tabu kwake kupata namba kikosini. Itoshe kusema beki huyo wa kati aliumaliza msimu huu akiwa amecheza mechi sita tu za Ligi Kuu.

Terence Kongolo (Huddersfield) 

Huddersfield walimng’oa Monaco na kumpa mkataba wa miaka mitano, wakiamini angewasaidia. Walivutiwa na kiwango kilichooneshwa na beki huyo walipokuwa naye kwa mkopo.

Katika mechi 13 alizokuwa amecheza, mbili zilimalizika bila timu hiyo kupitisha bao. Lakini msimu huu haukuwa mzuri kwake, Huddersfield ilishuka daraja na katika mechi 32 alizocheza, alichangia timu hiyo kufungwa mabao mawili, moja akijifunga na jingine ukiwa ni uzembe wake.

Rachid Ghezzal (Leicester City)

Kama ilivyokuwa kwa Soyuncu, Ghezzal naye alikuwa mzigo kwa Leicester msimu huu licha ya winga huyo kufunga bao katika mechi yake ya kwanza. Leicester walimnunua baada ya makali yake ya kutoa asisti nne katika mechi 26 za Ligue 1 akiwa na Monaco.

Kwa Ligi Kuu ya England msimu huu mambo yalikuwa magumu kwani mechi 23 alizocheza msimu mzima zilimshuhudia nyota huyo wa kimataifa wa Algeria akiwa hana ‘asisti’, huku akiwa amepiga mashuti 19 tu. 

Alireza Jahanbakhsh (Brighton)

Msimu uliopita akiwa na AZ Alkmaar, winga huyo raia wa Iran alikuwa moto huko Uholanzi, akifunga mabao 21 katika mechi za Ligi Kuu. Huku England, upepo ulikuwa mbaya kwa msimu mzima, kwani alicheza mechi 19 tu za EPL, tena akishindwa kupachika hata bao moja.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 25 ambaye majeraha yalimsumbua kwa kiasi fulani, amekiri kuwa alitarajia makubwa England.

Max Meyer (Crystal Palace)

Mjerumani huyo ambaye alikuwa moto wa kuotea mbali Bundesliga, alilazimisha kuondoka Schalke 04 na kutua Palace alikopewa mkataba wa miaka mitatu.

Hata hivyo, mambo hayakwenda kama alivyotarajia kwani katika msimu wake wa kwanza tu, Meyer (23) alicheza mechi 29 za Ligi Kuu, akifunga bao moja na kutoa asisti tatu tu.

Riyad Mahrez (Man City)

Alichukua ubingwa wa Ligi Kuu akiwa na Leicester City msimu wa 2015-16. Licha ya kuwa ameendelea kubeba vikombe pale Manchester City, bado msimu huu ulikwisha akiwa ni mchezaji wa kuanzia benchi.

Kati ya mechi zake 27 za Ligi Kuu, 13 alikuwa ‘sub’ kutokana na makali ya Raheem Sterling na Bernando Silva.

Fred (Man United)

Akiwa na Shakhtar Donetsk, Mbrazil huyo alikuwa balaa lakini mambo yalibadilika ghafla baada ya kutua Manchester United, ikifikia hatua ya Roy Keane kumponda hadharani.

Licha ya kushuka dimbani mara 17, alifunga bao moja, hivyo ni wazi msimu huu haukuwa mzuri kwake.

Gonzalo Higuain (Chelsea)

Alitua Chelsea mwanzoni mwa mwaka huu, ukiwa ni usajili wa mkopo akitokea Juventus, ikiwa ni baada ya kushindwa kung’ara AC Milan. Licha ya kupambana, bado huyu si Higuain wa misimu kadhaa iliyopita.

Kumbuka alivyokuwa Napoli na kocha wake wa sasa, Maurizio Sarri, ambapo alifunga mabao 92 katika mechi 147.

Msimu wa EPL ulikwisha akiwa ameshuka dimbani mara 14 lakini alifunga mabao matano tu na kuna kipindi alimaliza mwezi bila kuziona nyavu. 

Share.

About Author

Leave A Reply