Thursday, August 22

NI SIMBA DAY

0


*ZAITUNI KIBWANA

MABINGWA wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba, leo
wanatarajia kukabidhiwa kombe la ubingwa baada ya mchezo wa ligi hiyo dhidi ya
Biashara United utakaopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Wekundu wa Msimbazi hao wametwaa taji hilo kwa
mara ya pili mfululizo, wakifikisha alama 91 kabla ya mechi ya leo, ambazo haziwezi
kufikiwa na timu yoyote, wakiwamo watani wao wa jadi, Yanga, ambao hadi sasa
wana alama 83, baada ya michezo 37.

Akizungumza na BINGWA jana, Ofisa Habari na
Mawasiliano wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Clifford Ndimbo, alisema
mchezo huo utaanza saa 9:00 alasiri, ili kutoa nafasi ya sherehe za Simba kukabidhiwa
kombe lao.

Alisema Bodi ya Ligi imejipanga kuhakikisha zoezi
hilo la kukabidhi ‘mwali’ linakamilika, ikiwa ni sambamba na Wekundu wa
Msimbazi kukabidhiwa medali za ubingwa.

“Maandalizi yamekamilika, ndiyo maana mechi
itaanza saa 9:00 ili kupata nafasi ya kutoa zawadi hizo mapema zaidi,” alisema.

Wakati Ndimbo akisema hayo, Kocha Mkuu wa Simba, Patrick
Aussems, alisema kikosi chake kipo vizuri na tayari ameyafanyia kazi mapungufu
yaliyojitokeza katika michezo iliyopita.

Wakati huo huo, wachezaji wa Simba, wakiongozwa
na Nahodha, John Bocco, wameahidi kuwapa burudani mashabiki wao na wapenzi wa soka
hapa nchini katika mchezo huo, akiwataka kumiminika kwa wingi uwanjani leo.

“Tunajiandaa kwa ajili ya kushinda, tunaomba
mashabiki waje kutupa sapoti, wao ndio mchezaji wa 12 uwanjani, tunaahidi
hatutawaangusha. Waje kwa wingi kuujaza Uwanja wa Taifa ili kunogesha sherehe
za kukabidhiwa kombe letu,” alisema.

Taji hilo linakuwa la 20 kwa Wekundu wa Msimbazi hao,
wakizidi kupunguza pengo lililopo dhidi ya mabingwa wa kihistoria, Yanga,
waliolibeba mara 27.

Ufalme wa Simba msimu huu umepatikana baada ya
miamba hao kupoteza mechi tatu tu za ligi, mbili dhidi ya Kagera Sugar ya
Kagera na moja waliyofungwa na Mbao FC ya Mwanza.

Share.

About Author

Leave A Reply