Monday, August 26

Mourinho amgeuka Messi, adai hawezi kupewa Ballon d’Or

0


MADRID, Hispania

BINGWA wa kauli zenye utata, Jose Mourinho, ameibuka na kuelezea wasiwasi wake akisema kuwa anavyodhani nyota wa Barcelona, Lionel Messi, hastahili kupewa tuzo ya mchezaji bora wa mwaka wa dunia,  Ballon d’Or 2019.

Kwa mujibu wa kocha huyo wa zamani wa timu ya Manchester United, nahodha huyo wa Barca kushindwa kwake kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na klabu hiyo ua  Catalan ndicho kinamnyima sifa ya kupewa tuzo hiyo binafsi.

Awali nyota huyo wa Barcelona alikuwa akipewa nafasi hiyo ya kuibuka na tuzo hiyo ya  Ballon d’Or kwa mwaka huu, lakini baadaye wakajikuta wakipoteza ushindi wa mabao  3-0  walioupata wakiwa nyumbani katika mechi ya kwanza ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, baada ya kukubali kipigo cha mabao 4-0 dhidi ya  Liverpool  katika mchezo wa marudiano.

Katika mchezo huo uliopigwa katika Dimba la Anfield, Messi alionekana kushindwa kufurukuta muda wote wa dakika  90 na hivyo akashindwa kuibeba  Barcelona itingi kwa mara ya kwanza katika hatua ya fainali tangu msimu wa  2014-15.

Pamoja na kushindwa kung’ara katika Dimba hilo la Anfield, Messi msimu huu amekuwa msaada mkubwa kwa  Barcelona kutokana na kwamba mshindi huyo mara tano wa tuzo hiyo ya  Ballon d’Or amefunga mabao  48 katika mechi  48  na huku akitoa asisti 22 kwa wachezaji wenzake.

Hata hivyo, Mourinho msimu huu mara nyingi alikuwa akimsifia staa huyo hususan baada ya kuonesha kiwango cha hali ya juu katika mchezo wa kwanza wa nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, ambapo alisikika akimuita Mungu wa soka, lakini sasa Mreno huyo anaonekana kumgeuka akihoji uhalali wa staa huyo kupewa tuzo hiyo binafsi.

“Nina wasiwasi kama anastahili mwaka huu kupewa tuzo hiyo ya  Ballon d’Or kwa sababu ameshindwa katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya,” alisema  Mourinho katika uchambuzi wake katika kituo cha runinga cha  RMC.

Share.

About Author

Leave A Reply