Saturday, August 24

Mo Dewji: Mkude haendi popote

0


EZEKIEL TENDWA NA SAADA SALIM

BILIONEA wa Simba, Mohammed Dewji, amewakata
kilimilimi wapinzani wao wa jadi, Yanga, baada ya kutamka wazi kwamba kiungo
wao fundi, Jonas Mkude, haendi popote.

Akitumia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa
facebook, Dewji alitupia picha ya Mkude na kuandika: “Wanasimba msiwe na
wasiwasi, Mkude haendi popote! Jumaah Kareem.”

Maneno hayo ya Mo Dewji, ni kama majibu kwa Yanga,
ambao wamesema walishaanza mazungumzo na Mkude ili kumsainisha kwa ajili ya
msimu unaokuja.

Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela,
ndiye aliyesema wameshaanza mazungumzo na Jonas Mkude, na muda wowote angesaini
mkataba wa kuitumikia timu hiyo, lakini kauli ya Mo Dewji ni kama imezima uvumi
huo.

Taarifa zaidi kutoka Simba zinadai kuwa, Mo Dewji
alimuita Mkude nyumbani kwake juzi usiku baada ya kumalizika mechi ya kirafiki
ya kimataifa dhidi ya Sevilla ya Hispania na kuweka mambo sawa.

Mbali na Mkude, taarifa hizo zinadai kuwa, Mo
Dewji ameanza rasmi kazi ya kuzungumza na nyota waliomaliza mikataba yao, ambao
wapo kwenye mipango ya Kocha Patrick Aussems, wakiwamo Haruna Niyonzima, Erasto
Nyoni, Emmanuel Okwi, Shomari Kapombe na Aishi Manula.

“Mo alikutana na Mkude jana (juzi) usiku nyumbani
kwake, baada ya kumalizika mchezo dhidi ya Sevilla, ameanza rasmi kazi ya
kuzungumza na wachezaji waliomaliza mikataba na wapo kwenye mipango ya Kocha.

“Hizi siku chache atamalizana nao wote, akiwamo
Niyonzima (Haruna), Okwi (Emmanuel), Aishi Manula, Erasto Nyoni pamoja na
Kapombe (Shomari),” alisema kigogo mmoja ndani ya Simba.

Alisema mpaka sasa wachezaji wa kigeni wenye
asilimia kubwa ya kuonyeshwa mlango wa kutokea ni Asante Kwasi na Nicholas Gyan,
huku akidai Zana Coulibaly ambaye mashabiki wamekosa imani naye akikingiwa kifua
na kocha na huenda akaendelea kuwepo msimu unaokuja.

Share.

About Author

Leave A Reply