Sunday, August 18

Mfalme Neymar anapokimbia ngome zake taratibu

0


NA AYOUB HINJO

KADIRI siku zinavyosogea kupisha jua kuchomoza na
kuzama kisha mwezi kuchukua nafasi yake kumulika anga wakati wa kiza kinene,
kuna mambo mengi hutokea katika uso wa dunia hii tunayoishi ndani yake.

Ndivyo ilivyo katika maisha yetu ya kila siku ambayo
yamekuwa hayaeleweki kwa baadhi ya watu, huku kwa wengine yakionekana kwenda
sawa kama kupiga mstari mnyoofu na rula ya mita 30.

Wakati mwingine ni ngumu sana kuyaelewa maisha, si
rahisi hata kidogo japokuwa tunaishi ndani ya ulimwengu huu uliojaa shida,
mateso, raha na karaha kwa muda wote.

Kwa ukaribu zaidi, itazame sura ya Neymar, inawezekana
kuna mengi yanakufikirisha kadiri unavyoitazama au kuikumbuka taswira yake
ilivyo.

Inawezekana pia dunia tunayoishi sisi si ile
anayoishi Neymar, achana na mambo mengine yanayomzunguka nje ya uwanja.

Mtazame Neymar aliyeanza safari ya soka miaka mingi
kidogo nyuma akiwa Santos FC ya nchini Brazil, aliishi ndani ya pepo yake
iliyojaa matumaini makubwa ya Wabrazil kuwa shujaa mpya amezaliwa.

Habari za ubora na uwezo wa Neymar zilipenya kwa
kila mmoja duniani japo kwa wakati huo alikuwa akifanya yake nchini Brazil.

Wapo waliowahi kusema kipaji hakijifichi, pamoja na
hayo yote Neymar alisubiriwa Ulaya. Sehemu ambayo inaaminika mwanasoka
atakumbana na mambo mengi hasa ushindani.

Muda ulipofika, kila mmoja alimwona Neymar akiwa
Barcelona, ujio wake uliifanya klabu hiyo kutengeneza kombinesheni ya wachezaji
watatu hatari katika idara ya ushambuliaji MSN (Messi, Suarez na Neymar).

Lakini mwisho wa siku Neymar alikimbia Barcelona,
hakuhitaji kuwa chini ya kivuli cha mchezaji mwingine, alitamani kuishi sehemu
ambayo atatajwa kuwa mfalme.

Aliondoka na kujiunga na PSG tena kwa uhamisho wa
mchezaji ghali zaidi duniani, mambo yalianza kubadilika ndani ya klabu hiyo.

Wote walioonekana wafalme ilibidi waisikilize sauti
ya Neymar inahitaji au inataka nini, si wachezaji tu hata kocha ambaye
alikuwepo alimsikiliza zaidi nyota huyo.

Miezi miwili na siku 14 zilizopita, Neymar alitimiza
miaka 27, inashtua kidogo, ni wakati ambao wachezaji wengi wanaishi kwenye
kilele cha ubora wao katika soka.

Ni muda huo ambao Neymar ameanza kupunga mkono wa
kwaheri, unajua kwanini? Nitakueleza huko mbele jinsi vinasaba vya soka
vinavyojaribu kupita mbali ya staa huyo.

Katika umri wake bora kabisa kisoka, Neymar yuko PSG
akicheza michezo ya kitoto na akina Kylian Mbappe, sidhani kama tunatakiwa
kusubiri zaidi ya kukubaliana kuwa staa huyo ni Theo Walcott wa bei ghali.

Rudi miaka kadhaa nyuma, Neymar alikuwa mmoja wa
nyota ambao walitazamiwa kushindana bega kwa bega na Cristiano Ronaldo au
Lionel Messi.

Moja, Neymar ni mchezaji mwenye kipaji kikubwa mno hasa
pale anapoamua kucheza mpira, binafsi naamini mpaka sasa dunia imeona mambo
machache sana kutoka kwake.

Mbili, hakuuheshimu muda jaribu kuitazama Barcelona
hii ya sasa kama Neymar angekuwepo ndani yake, taratibu alikuwa anachukua
ufalme wa Messi.

Tangu aingie barani Ulaya hakuna Neymar bora zaidi
ya yule aliyewahi kuvaa jezi ya Barcelona, licha ya kuwa chini ya Messi bado
aliweza kufanya mambo makubwa na kwa kiasi fulani alitengeneza pepo yake kando
ya staa huyo wa Argentina.

Mchezaji wa kariba ya Neymar, ana uwezo wa
kufanya kitu ambacho hujawahi kukiona kokote kule. Kitu ambacho hujawahi kukipatia
picha.

Aina ya mabao aliyokuwa akifunga ni yale
ambayo hata wataalamu wa kutengeneza filamu za michezo waliwaza na kujaribu
kutengeneza filamu ya shujaa wa soka aliye kwenye maisha ya uhalisia.

Huyo ndiye Neymar. Mchezaji anayefanya
maajabu kwenye maisha ya kweli.

Ilikuwa ni ngumu kutabiri atakachokifanya
sekunde tatu baadaye akiwa na mpira mguuni mwake, lakini tayari unakuwa ushajua
kuna kitu cha ajabu kitatokea.

Angeweza kukokota mpira kwa kasi ya roketi na
kuwapita wachezaji wanne au watano, akichanganya miguu kwa chenga za gemu la
Fifa. Rahisi kihivyo tu.

Angeweza kufunga bao la dakika za mwisho kwa
mguu wowote na mpira ungeenda kutua nyavu za juu, pembeni kabisa. Kwisha kazi.

Angeweza kufunga bao kali la mpira wa adhabu
kutoka umbali wa yadi 40. Kwenye pembe ngumu mno.

Alibarikiwa kila kitu, lakini mpaka kufikia
sasa akiwa na miaka 27, bado hajui anahitaji kitu gani, sahau kuhusu pesa
anazozipata kutokana na utanashati wake.

Weka kando wasichana wanaogongana katika
ghetto lake kila kukicha, kwa umri wake alistahili kuwa mmoja wa wachezaji walioiweka
dunia chini ya nyayo zake.

Inaaminika umri huo unakuwa tayari umepitia
mambo mengi, vishawishi na starehe nyingi. Kwa kifupi, kunakuwa hakuna kipya
ndani yake.

Nyota wengi waliotamba kwa vipindi katika
soka, walikuwa kwenye umri wa aina hiyo, kumbuka akina Ricardo Kaka, Robin van
Persie na wengine wengi kwa wakati tofauti.

Bado tunaendelea kumtazama Neymar, haeleweki
yupo katika kundi gani bado hatazamiki kama zamani.

Katika fainali za Kombe la Dunia mwaka jana
nchini Urusi, kila shabiki wa soka alionekana kuwa kinyume na Neymar, hakufanya
kile alichotegemewa na wengi, alikatisha tamaa na kuvunja mioyo ya walikuwa na
imani naye.

Neymar hana utofauti na Luis Nani ambaye
alitabiriwa kufanya makubwa kando ya Ronaldo wakati wapo Manchester United hata
alipoondoka kwenda Real Madrid.

Nani alishindwa kujazia mchanga shimo
lililoachwa na Ronaldo, mwisho wa siku licha ya kipaji chake kikubwa alionekana
mchezaji wa kawaida kuwahi kutokea Manchester United.

Si rahisi kihivyo kuishi kwenye ndoto za
wengi ingawa bado ni rahisi kutimiza kile kinachotazamiwa na wengi kama
kutakuwa na juhudi kubwa kwa mtu husika.

Sioni mwendelezo wa Neymar bora zaidi, bado
haeleweki duniani wala mbinguni. Tayari amevunja mioyo ya wengi, tatizo ni
kwamba jamaa hayupo ‘siriaz’ sana.

Share.

About Author

Leave A Reply