Wednesday, August 21

Mexime ataingia katika rekodi ya kuishusha Kagera Sugar daraja?

0


MZEE WA KUPASUA, kapssmo@gmail.com
0716985381

NA ONESMO KAPINGA

PAZIA la Ligi Kuu Tanzania Bara  linatarajia kufungwa kesho kwa timu zote
kushuka uwanjani na kufunga hesabu za msimu huu.

Kutokana na msimamo wa ligi hiyo, vita kali itakuwa kwa
timu tisa ambazo zinapigania kubaki msimu ujao, baada ya Simba kufanikiwa
kutetea ubingwa wao kwa kufikisha pointi 92 ambazo hazitafikiwa na timu
nyingine.

Yanga wanaoshika nafasi ya pili, wakishinda mchezo
wao dhidi ya Azam watakuwa na uwezo wa kufikisha pointi 89, wakati Azam
wanaoshika nafasi ya tatu wanatakuwa na pointi 75 wakipata pointi tatu kwa Wanajangwani
hao.

Tayari African Lyon imetangulia kushuka daraja ikiisubiri
timu nyingine itakayoungana nayo kushiriki Ligi Daraja la Kwanza msimu ujao.

Timu hiyo ambayo ilirejea msimu uliopita baada ya
kushuka daraja katika msimu wa Ligi Kuu Bara uliotangulia imerudi tena ilikotoka,
ikishindwa kuhimili mikikimikiki ya ligi hiyo.

African Lyon hata ingefanikiwa kushinda mchezo mmoja
uliosalia, kwani ikishinda  itakuwa na
uwezo wa kufikisha pointi 26 ambazo hazitaisaidia kubaki msimu ujao.

Kati ya timu zinazopigania kubaki msimu ujao ni
Kagera Sugar ambayo ipo chini ya kocha Mecky Mexime, kwani katika misimu tatu
imekuwa ikinusurika kushuka daraja.

Kwa sasa Kagera Sugar inashika nafasi ya 17 kutokana
na pointi 43, hivyo kuhitaji ushindi katika mchezo wake wa kesho dhidi ya Mbao
ili iweze kujihakikishia kubaki msimu ujao.

Kagera Sugar ikipoteza mchezo huo itabidi isubiri
kuangalia matokeo ya timu nyingine ambazo zipo katika hali mbaya ya kushuka
daraja msimu huu.

Ukiangalia msimamo wa ligi hiyo, kuanza nafasi ya 12
timu yoyote ikipoteza mchezo wake wa mwisho inaweza kuungana na African Lyon
kushiriki Ligi Daraja la Kwanza msimu unaokuja.

Hivyo, Kagera Sugar watakuwa na kazi ya ziada ya
kusaka ushindi kutoka kwa Mbao ambao wanahitaji pointi tatu ili waweze kubaki
kwenye ligi hiyo.

Mbao wanashika nafasi ya 15 kutokana na pointi 44,
hivyo wanahitaji ushindi dhidi ya Kagera Sugar ili kujihakikishia kubaki msimu
ujao.

Kocha Mexime atakuwa katika historia iwapo timu hiyo
itashuka Ligi Kuu Bara ambayo haijawahi kushuka tangu ilipopanda daraja.

Pamoja na Mexime kuikuta timu hiyo ikiwa katika
changamoto ya kushuka daraja, lakini msimu huu umejirudia tena na asipokuwa
makini Kagera Sugar inaweza kuungana na African Lyon kushiriki Ligi Daraja la
Kwanza kwa msimu unaokuja.

Mexime bado ana kazi ya kuhakikisha anaibakisha ligi
kuu, kwani itakuwa ni timu yake ya kwanza aliyoifundisha kushuka daraja.

Lakini timu nyingine ambayo iko katika hali mbaya ya
kushuka ni Biashara United, licha ya kupata sare ya bao 1-1 kutoka kwa Simba
lakini wanahitaji kupata pointi tatu dhidi ya Mbeya City.

Katika mchezo huo, Mbeya City hawana cha kupoteza
kwani tayari wamejihakikishia kubaki kutokana na kufikisha pointi 47 huku
wakiwa wanashika nafasi ya nane kwenye msimamo wa ligi hiyo.

Amri Said ambaye ni kocha wa Biashara United,
atakuwa na kazi kubwa kuhakikisha hazamishi jahazi la timu hiyo iliyopanda Ligi
Kuu msimu uliopita.

Timu nyingine zinazopigania kubaki msimu ujao ni JKT
Tanzania, Mwadui, Ruvu Shooting, Tanzania Prisons na Stand United.

Tukutane
Jumatatu ijayo

Share.

About Author

Leave A Reply