Friday, July 19

Mbeya City yawaita mezani Simba, Yanga

0


NA SAADA SALIM


UONGOZI wa Mbeya City umewataka Simba na Yanga kukaa meza moja kwa ajili ya kuzungumza juu ya straika wake, Eliud Ambokile, kuliko kufanya naye mazungumzo pembeni.

Dirisha dogo la usajili linatarajia kufunguliwa Novemba 15, mwaka huu, lakini tayari klabu hizo kongwe nchini zimeanza kunyemelea saini ya Ambokile anayeongoza kwenye orodha ya wafungaji, akiwa na mabao nane.

Akizungumza na BINGWA jana, Katibu wa Mbeya City, Emmanuel Kimbe, alisema uongozi umekuwa ukisikia taarifa za kutakiwa kwa mchezaji wao huyo na viongozi wa timu hizo, huku wakimfuata pembeni lakini kwa upande wao hakuna taarifa rasmi iliyowafikia juu ya kumhitaji.

Alisema timu yoyote inayomhitaji mchezaji wao huyo mwenye mkataba wa mwaka mmoja, inatakiwa kufuata taratibu zote za usajili kuliko kupita njia za mkato.

“Eliud ni mchezaji wetu halali, hivyo hizo klabu kama wana malengo naye waje tuzungumze kama hawawezi wamuache mchezaji wetu acheze mpira, kama ni kweli wanamfuata au kuwasiliana naye basi wanatakiwa kuachana na hayo, kwani wanampotezea malengo yake,” alisema.

Kimbe alisema amekaa na mchezaji wake huyo kwa kuwaeleza juu ya klabu au timu yoyote itakayomhitaji, kutakiwa kufuata taratibu kwa kwenda kufanya mazungumzo na uongozi wake

Share.

About Author

Leave A Reply