Sunday, August 18

Liverpool watamba kuizima Barca

0


LONDON, England

KAMA
huipendi Liverpool basi tambua utapata tabu sana, kwani Barcelona wataambulia
kichapo tu pale Anfield kwa mujibu wa James Milner, kuelekea mchezo wao wa siku
11 zijazo.

Mtanange
huo utatanguliwa na ule wa Tottenham na Ajax, ambao utachezwa Aprili 30 jijini
London kabla ya ule wa marudiano kule Uholanzi.

Liverpool
ni tofauti na Machester United iliyotolewa na Barca hatua ya robo fainali,
kwani katika msimamo wa Ligi Kuu iko juu kwa pointi 21 dhidi ya Mashetani
Wekundu hao.

Hilo
lilithibitishwa na aliyekuwa beki wa pembeni wa Man United, Gary Neville,
aliposema: “… Liverpool ni bora zaidi kuliko Man United.

“Liverpool
wana kikosi kizuri na kina nguvu kuliko Barcelona hii. (Liverpool) hawana ubora
kivile katika kiungo lakini wako sawa eneo la ulinzi na ushambuliaji.”

Kwa
upande wa Milner, katika mahojiano yake na gazeti la Mirror, Milner alisema
wana uwezo wa kuwasukuma nje ya mashindano hayo Barca ingawa alikiri haitakuwa
rahisi.

“Ni
timu nzuri na ni ngumu kuwakabili lakini sidhani kama wamekutana na zinazocheza
soka la aina yetu,” alisema ‘kiraka’ huyo.

Wakati
Milner raia wa Uingereza akitamba kwa upande huo, rekodi mpya iliyoibuliwa na
gazeti la Liverpool Echo imezidi kuiweka pabaya Barca kuelekea mchezo huo wa
Mei mosi.

Iko
hivi, vijana wa kocha Jurgen Klopp watashuka dimbani siku hiyo wakijua fika
kwamba Liverpool ndiyo timu pekee ya Ligi Kuu ya England iliyowahi kuibuka na
ushindi katika Uwanja wa Nou Camp, hiyo ikiwa ni mwaka 2007.

Hata
hivyo, wakati Milner akiwa na jeuri hiyo, kocha wa Barca, Ernesto Valverde,
alishasema wana kiu ya kutinga fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya
kuikosa hatua hiyo kwa misimu kadhaa.

“Tumefurahi
(kuingia nusu fainali). Ni muda sasa tangu tulipocheza nusu fainali. Sasa
tungependa kucheza fainali,” alisema Valverde akimsifia staa wake, Lionel
Messi, ambaye kwa kuwatungua mara mbili Man United aliweza kufikisha mabao 10 msimu
huu wa Ligi ya Mabingwa.

Share.

About Author

Leave A Reply