Tuesday, August 20

Liver wakinasa silaha hizi Man City wataisoma namba

0


LONDON, England

WENGI wa mashabiki wa Liverpool watakuwa wamebaki na
mfadhaiko baada ya timu yao kukosa tena ubingwa wa Ligi Kuu England dhidi ya Manchester
City.

Msimu huu vijana hao wa Jurgen Klopp waliweza
kufikisha rekodi ya pointi 97, lakini mafanikio hayo mazuri hayakuweza kutosha
kuipora ubingwa Man City ambayo iliwazidi pointi moja.

Hata hivyo, Reds kwa sasa ni moja ya timu zenye
kikosi imara Ulaya ambacho kinaweza kushindana na timu yoyote ngumu.

Hii ni kutokana na baadhi ya wachezaji wazuri ambao
iliwasajili hivi karibuni wakiwamo, Mohamed Salah na Virgil van Dijk ambao
wamekuwa na mafanikio makubwa na kuifanya timu hiyo kuwa moja ya timu bora.

Hata hivyo, pamoja na Liverpool kuwa na mafanikio
hayo makubwa bado kuna nafasi kadhaa ambazo kocha wao, Klopp anapaswa kuzijaza
ili kuweza kumaliza upungufu na udhaifu uliojitokeza ambao wataifanya Reds kumaliza
utawala wa Man City katika michuano hiyo ya Ligi Kuu England kuanzia msimu ujao.

 Wafuatao ni
wachezaji watatu ambao endapo itafanikiwa kuwasajili wataisaidia kupata
mafanikio hayo ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu England.

 1. Matthijs de Ligt

Kwa sasa klabu mbalimbali kubwa Ulaya zinahusishwa
kumnyatia staa huyo  Matthijs de Ligt, kufuatia
mafanikio ambayo Mholanzi huyo ameyapata akiwa na klabu yake ya Ajax. Hata
hivyo, pamoja na nyota huyo kuhusishwa na klabu hizo, lakini Liverpool ndiyo
inaweza kuwa mbadala kwa De Ligt, ili aweze kushirikiana na mwenzake, Virgil
van Dijk.

Wengi wa mashabiki wameshashuhudia jinsi timu ya
Taifa ya Uholanzi inavyofanya makubwa Ulaya ikiwa chini  ya De Ligt na Van Dijk wanapokuwa pamoja
katika safu ya ulinzi wa kati.

Ushirikiano wa mastaa hao ndio umeifanya Oranje
kuweka rekodi ya kutoruhusu bao wakati ilipokutana na timu za Mataifa ya Ufaransa
na Ujerumani wakati wa michuano ya Ligi ya timu za Taifa Ulaya.

Licha ya msimu huu, Joel Matip kuonesha ushirikiano
mzuri na Van Dijk, lakini wengi wa mashabiki wanaamini staa huyo mwenye umri wa
miaka 27 si mbadala kwa nyota huyo wa zamani wa  Southampton.

 De Ligt anaonekana
kuwa mzuri zaidi kuliko Mcameroon huyo katika eneo hilo la ulinzi licha ya kuwa
na umri mdogo  wa miaka tisa dhidi ya Matip.

Kinda huyo mwenye umri wa miaka 19, anaonekana kuwa
na kila kitu ambacho kinaweza kumfanya awe mzuri zaidi chini ya utawala wa Klopp
kutokana na kwamba ana uwezo mkubwa wa kupiga pasi na kufunga mabao akiwa
katika mazingira yoyote.

 Mbali na hilo,
kinda huyo pia hana wasiwasi katika safu ya ulinzi jambo ambalo limemfanya kuwa
na wastani wa asilimia nne wa kutoruhusu bao kwa kila mechi katika mashindano
yote.

Licha ya Liverpool kukanusha kuwa na nia yoyote ya
kumsajili, De Ligt, lakini  Reds watakuwa
wamelamba dume endapo watafanikiwa kumsajili kinda huyo mwenye kipaji cha hali
ya juu.

2.
Nabil Fekir

Ni wazi kila shabiki atakuwa anafahamu fika kwamba Liverpool
hawajawahi kupata mchezaji mbadala wa Philippe Coutinho, tangu Mbarazil huyo
aliposajiliwa kwa ada ya Euro milioni 120 na Barcelona wakati wa usajili wa majira
ya baridi Januari mwaka jana.

 Kutokana na
hali hiyo, Nabil Fekir msimu uliopita alikuwa karibu achukue mikoba ya Coutinho
kwenye klabu hiyo ya Anfield, lakini ndoto za staa huyo kujiunga na Ligi Kuu
England zikayeyuka dakika za mwisho.

Hata hivyo, Liverpool wanaweza kujaribu kurusha tena
ndoano wakati wa usajili wa majira haya ya joto.

Licha ya msimu huu Mfaransa huyo kutokuwa kwenye
ubora kama aliokuwa nao msimu wa 2017-18, lakini kipaji chake kikubwa bado
anacho.

 Mpaka sasa Liverpool
hawana kiungo mshambuliaji ambaye ana uwezo kama alivyokuwa Coutinho.

Kutokana na hali hiyo, Fekir anaweza kuwa nyongeza
kubwa katika kikosi chake kwani msimu huu ameweza kufunga mabao tisa kwenye
ligi na huku akitoa ‘asisiti’ saba.

Vilevile staa huyo amekuwa mchezaji tegemeo katika
kikosi cha Lyon kipindi chote cha michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na ndiye
aliyefunga na kutoa ‘asisiti’’ wakati wa mechi ya hatua ya makundi dhidi ya Manchester
City.

 Staa huyo ni
kiungo mkabaji mwenye uwezo wa kufunga mabao na kutengeneza nafasi kwa wachezaji
wenzake, hivyo Fekir anaweza kuwa hazina kubwa katika harakati za  Liverpool katika kusaka ubingwa.

 3. James Rodriguez

Staa huyo raia wa Colombia anaonekana kupoteza
kipaji chake tangu aliposajiliwa kwa ada ya Euro milioni 80 kwenda  Real Madrid mwaka 2014.

Staa huyo alionekana kuwa na makali katika msimu
wake wa kwanza alipotua Los Blancos, ambapo aliweza kufunga mabao 13 na kutoa
‘asisiti’ nyingi kipindi chote cha msimu huo wa 2014-15.

Hata hivyo, kwa bahati mbaya mambo yakaja kubadilika
mwaka 2016 wakati  Zinedine Zidane alipopandishwa
cheo na kuwa kocha mkuu wa Real Madrid.

Baada ya Mfaransa huyo kukabidhiwa mikoba hiyo, staa
huyo alijikuta akicheza mechi 13 za kikosi cha kwanza kati ya  22 jambo ambalo lilimfanya aondoke na kwenda
kucheza kwa mkopo Bayern Munich.

Hata hivyo, Bavarian pia wanaonekana kuwa na
wasiwasi kuchagua kumnunua moja kwa moja kutokana na kuwa na kiwango tofauti tofauti
tangu alipotua nchini Ujerumani.

Licha ya hali hayo, lakini kipaji cha Rodriguez bado
kinamfanya kuwa mmoja kati ya viungo bora Ulaya.

Msimu huu staa huyo amefunga mabao saba na kutoa
asisiti tatu licha ya kocha wake, Niko Kovac kumpanga mara 13 kwenye kikosi cha
kwanza katika michuano ya Ligi ya Bundesliga.

 Uwezo kiuchezaji
vilevile bado ni mzuri kutokana na kuwa amekamilisha asilimia 87 na wastani wa
utoaji pasi ukiwa ni asilimia 2.6.

Msimu uliopita pia alikuwa ni mchezaji tegemeo kwa Bayern
katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ambapo aliweza kucheza mechi 12 na
alishiriki kupatikana mabao matatu kipindi chote cha mashindano hayo.

Kutokana na uimara wake katika safu ya kiungo na
jicho lake lenye uwezo wa kuona lango, staa huyo wa Real Madrid anaweza kuwa
mtu mbadala wa kuchukua nafasi ya James Milner katika klabu hiyo ya Anfield.

Share.

About Author

Leave A Reply