Wednesday, May 22

Kumekucha shindano la Master Tanzania 2018/19

0


NA MWANDISHI WETU

SHINDANO la Master Tanzania 2018/19, lilizinduliwa Machi mwaka huu jijini Dar es Salaam, likilenga kutoa fursa kwa vijana wa kiume wa Tanzania kutimiza ndoto zao kupitia vipaji vyao, ikiwamo uanamitindo na sanaa kwa ujumla.

Vijana lukuki walijitokeza kushiriki shindano hilo na kukabidhiwa vyeti na Rais wa Kampuni ya Kiafrika Zaidi, waratibu wa kinyang’ayiro hicho, Winny Casey, ambaye anafanya shughuli zake nchini Marekani.

Hata hivyo, baada ya uzinduzi huo, mchakato wa shindano uliishia hapo kabla ya msisimko wa shindano hilo kuibuka tena Oktoba mwaka huu, baada ya Winny kumteua mdau wa tasnia ya urembo, uanamitindo na sanaa kwa ujumla, Michael Maurus, kuwa mratibu wa kinyang’anyiro hicho hapa nchini.

Mara baada ya uteuzi huo, Maurus alianza upya mchakato wa shindano hilo kwa kushughulikia kibali cha kuendesha shughuli za sanaa kinachotolewa na Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) na kufanikiwa katika hilo.

Baada ya hapo, mchakato wa kusaka washiriki ulianza upya, lakini wale waliokuwapo katika uzinduzi wa shindano hilo, wakipewa kipaumbele kabla ya kualikwa wengine zaidi.

Hadi sasa, zaidi ya washiriki 35 wameshajiandikisha kushiriki shindano hilo ambalo fainali zake zinatarajiwa kufanyika Februari mwakani.

Mwandishi wa gazeti hili, hivi karibuni alifanya mahojiano na Maurus kufahamu mchakato mzima wa shindano hilo, sifa za washiriki, zawadi na mengineyo.

Katika mahojiano hayo, Maurus anasema: “Shindano letu la Master Tanzania kwa sasa lipo kisheria likiwa limepata baraka zote na Basata ambao walituma mwakilishi wao siku ya uzinduzi wa awali ya pili mapema mwezi uliopita.

“Hadi sasa tumeshapata washiriki zaidi ya 35 na bado wanaendelea kujiandikisha, lengo letu ni kuwa na washiriki wasiopungua 50.”

Alisema fomu za shindano hilo zinapatikana katika ofisi za Kampuni ya New Habari (2006) Limited zilizopo Sinza Kijiweni, Dar es Salaam, wazalishaji wa magazeti ya Bingwa, Dimba, Mtanzania na Rai pamoja na Mtanzania Digital, lakini pia Forty Forty Club iliyopo Tabata Bima na Ofisi za Basata.

“Kama sehemu ya kulinadi shindano letu, tumeshaanza ziara za kutembelea maeneo mbalimbali. Jumamosi iliyopita tuliwatambulisha washiriki kwa wadau pale Forty Forty Tabata na wikiendi hii tunatarajiwa kusafiri hadi mkoani Morogoro na baadaye Kisarawe kwa mheshimiwa Mkuu wa Wilaya hiyo, Jokate Mwegelo, ambaye ni mdau maarufu wa mambo ya sanaa,” anasema Maurus.

Maurus ambaye ni miongoni mwa wahariri wa gazeti la Bingwa, anasema kuwa wanatarajia kufanya shoo maalumu ya utambulisho wiki ya pili ya Desemba ambapo kutakuwa na burudani ya nguvu kutoka kwa moja ya bendi kongwe hapa nchini na msanii mkali wa Bongo Fleva.

Juu ya sifa za ushiriki, Maurus anasema kuwa kijana yeyote wa kiume mwenye umri kati ya miaka 19 na 28, ndiye anayeruhusiwa kushiriki, lakini akiwa ni yule ambaye hajaoa.

Anasema kuwa vigezo vitakavyotumika kumpata mshindi ni nidhamu, kipaji, jukwaa na vinginevyo vitakavyowekwa wazi baadaye baada ya kikao cha pamoja kati ya uongozi wa Kiafrika Zaidi na Basata.

Kuhusiana na zawadi za washindi, Maurus anasema watakaoshika nafasi tano za juu, watapata tiketi ya kwenda Marekani kutembelea maeneo maarufu ya Hollywood, majumba ya wanamuziki na wasanii maarufu duniani kama Michael Jackson, Beyonce na wengineo wengi.

“Hapo sasa itabaki kwa washiriki wenyewe kujiuza huko kulingana na uelewa na vipaji vyao maana watatembezwa katika kampuni mbalimbali za mitindo na sanaa, hivyo wale watakaowagusa wahusika, wanaweza kupata mikataba ya kufanya nao kazi,” anasema Maurus.

Maurus anawataka vijana wa kiume wa Tanzania kuchangamkia fursa hiyo adimu, huku akiwaomba wadau wa sanaa na uanamitindo nchini kuwapa sapoti ili waweze kufanikisha kutimiza ndoto za washiriki wa shindano hilo.

 

Share.

About Author

Leave A Reply