Sunday, August 18

Kagere aahidi ushindi Kaitaba

0


NA HUSSEIN OMAR

MSHAMBULIAJI wa Simba, Meddie Kagere, ameahidi kuwa wataendeleza wimbi la ushindi katika mchezo wao mwingine wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Kagera Sugar utakaopigwa leo kwenye Uwanja wa Kaitaba, mjini Bukoba.

Simba watacheza mchezo huo baada ya kutoka kuwachapa
Coastal Union 2-1 katika mtanange huo uliopigwa katikati ya wiki kwenye Uwanja
wa Mkwakwani, Tanga, ambapo Kagere alifunga mabao yote mawili.

Akizungumza na BINGWA jana, Kagere alisema ili
kutimiza azma yao ya kutetea ubingwa wao wa Ligi Kuu msimu huu, ni lazima
waendeleze wimbi la ushindi kwa kila timu watakayokutana nayo.

“Moja ya mikakati tuliyojipangia ni kutetea ubingwa wetu
ili mwakani tucheze tena michuano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika, hivyo
suala la ushindi ni muhimu katika kila mchezo tutakaocheza ikiwamo wa kesho
(leo),’’ alisema Kagere.

Nyota huyo Kagere alisema kuelekea mchezo huo wa leo
atajitahidi kadiri ya uwezo wake kuhakikisha anaendeleza kasi yake ya ufungaji
ili kuweza kujiweka katika nafasi nzuri ya kutwaa kiatu cha ufungaji bora,
ambapo kwa sasa anafungana kwa mabao 16 na mshambuliaji wa Mwadui FC, Salum
Aiyee.

Naye kocha wa timu hiyo, Patrick Aussems, amesema wataendelea
kuwapa nafasi wachezaji wake ambao alikuwa hawatumii mara kwa mara katika mechi
zilizopita.

“Nitaendelea kutoa nafasi kwa mchezaji kwenye kikosi
changu, hivyo kila mmoja lazima atambue wajibu wake na kufuata maelekezo
anayopewa,” alisema Aussems.

Wakati Simba wakitangaza vita kwa Kagera Sugar, kocha msaidizi
wa timu hiyo, Ally Jangalu, amesema kuelekea mchezo huo wa leo wanaiheshimu
Simba lakini wamejipanga kuwatibulia kama ilivyo kawaida yao.

“Tunajua tunacheza na timu nzuri lakini sisi pia
hatutaingia kinyonge kama unavyojua msimu huu si mzuri sana kwetu, hivyo tuna
kila sababu ya kupata alamu tatu,” alisisitiza Jangalu.

Kwenye msimamo wa ligi Kagera Sugar imecheza michezo
32 na imejikusanyia pointi 36, ikiwa na nafasi ya 17 huku wapinzani wao Simba
wanashika nafasi ya tatu baada ya kucheza michezo 23 na pointi 60.

Share.

About Author

Leave A Reply