Monday, March 18

Ijue sababu ya Charles Mkwasa kuitwa Master

0


NA HENRY PAUL   

KATIKA kumbukumbu zako za kufuatilia mchezo wa soka
uliwahi kujiuliza ni sababu zipi zilimfanya nyota  wa zamani wa Yanga na Taifa Stars,  Charles Mkwasa, kuitwa Master wakati wakicheza
soka ya ushindani?

Kama ulikuwa unajiuliza swali hilo bila kupata
jibu, basi leo utafahamu ukisoma makala hii, sababu zilizomfanya nyota huyu
kuitwa jina hilo.

Lakini kama hukubahatika kumwona wakati
akicheza, kuanzia leo utafahamu sababu zilizowafanya mashabiki kumwita Master.

Mkwasa alijiunga na Yanga katika msimu
wa 1979/80 akitokea Klabu ya Tumbaku ya Morogoro, akiwa na mshambuliaji, Omar
Hussein ‘Keegan’.

Wakati huo alianza kuchipukia kucheza
soka lakini Keegan tayari alikuwa nyota na mchezaji wa timu ya Taifa Stars.

Baada ya Mkwasa kujiunga na Yanga
aliwakuta viungo wengine watatu wazoefu, Sammy Kampambe, Juma Mkambi na Issack
Mwakatika, hivyo  kuwa mchezaji wa akiba
katika kikosi hicho.

Mara nyingi alikuwa akiingia kipindi cha
pili kuchukua nafasi ya kiungo mmojawapo ya hao ambaye alikuwa akicheza safu ya
kiungo mshambuliaji.

Lakini kadiri siku zilivyokuwa zikienda Mkwasa
akawa anapata uzoefu, hivyo  kuanza
kupangwa katika kikosi cha kwanza akicheza nafasi hiyo huku akiwa na kiungo
mkabaji Juma Mkambi ambaye kwa sasa ni marehemu.

Mkwasa akicheza safu ya kiungo
mshambuliaji alianza kung’ara mno na kuiwezesha Yanga kufanya vizuri katika
michuano mbalimbali.

Pamoja na nyota huyo kucheza idara ya
kiungo, lakini mara kadhaa alikuwa akipangwa kucheza nafasi ya ulinzi wa kati
aliyeimudu vizuri.

Mwaka 1983, Yanga ilicheza mchezo wa
mwisho wa kuwania ubingwa wa Jamhuri ya Muungano dhidi ya Small Simba ya
Zanzibar, uliochezwa Oktoba mosi mwaka 1983 kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar
es Salaam (sasa Uhuru) na Yanga ilishinda mabao 4-1.

Katika mchezo huo, Mkwasa alichezeshwa
safu ya kiungo mshambuliaji na kunga’ara mno, kwani alionekana ni mwiba mkali
kwa Small Simba.

Katika ushindi wa mabao manne, Mkwasa alifunga
mabao matatu.

Bao la kwanza la Mkwasa alilifunga dakika
ya tisa baada ya kupokea pasi kutoka kwa Mkambi na kuwapiga chenga mabeki
wawili wa Small Simba na kupiga shuti kali lililomshinda kipa wa Small Simba,
Ally Mahsin na mpira kutinga wavuni.

Baadaye, alifunga bao dakika ya 41
ambalo lilikuwa ni la tatu kwa Yanga, kwani bao la pili lilifungwa na Abeid
Mziba.

Mkwasa alifunga bao hilo kwa kichwa
baada ya kupokea krosi muruwa kutoka kwa winga ya kushoto kwa Juma Kampala.

Dakika ya 76, Mkwasa alifunga bao la nne
baada ya kuunganisha krosi kutoka kwa Hussein Iddi, aliyeingia kipindi cha pili
kuchukua nafasi ya Kampala.

Ushindi huo wa mabao 4-1 uliiwezesha
Yanga kutwaa taji la ubingwa wa Jamhuri ya Muungano kwa mwaka huo.

Baada ya Mkwasa kufunga mabao matatu
katika mechi hiyo, aliangaliwa kuwa kwa kiasi kikubwa ndiye aliyeiwezesha timu
hiyo na kutwaa taji hilo.

Kuanzia hapa wapenzi wa klabu Yanga
‘walimbatiza’ jina la Master kutokana na uwezo alioonyesha katika mchezo ule.

Wapenzi wa Yanga walisikika wakisema
kuwa huyu Mkwasa ni kiboko, akicheza kiungo anafunga mabao huku akicheza
sentahafu anaimudu nafasi hiyo, hivyo toka siku hiyo jina hilo likawa limeingia
vichwani mwao.

Jina la Master liliendelea kuzoeleka kwa
mashabiki hata alipokuwa akichezea timu ya Mkoa wa Dar es Salaam  maarufu Mzizima United na Taifa Stars na alipostaafu
kucheza soka ya ushindani miaka ya 1980, anaendelea kuitwa jina hilo.

Share.

About Author

Leave A Reply