Monday, August 19

Huko EPL zimebaki mechi mbili tu, nani kutwaa ubingwa, kushuka daraja, kuingia ‘top four’ au kufuzu Europa?

0


LONDON, England

MAMBO yanazidi kunoga katika Ligi Kuu
ya England, mbio za ubingwa si rahisi kuzitabiri, upande mwingine zipo timu
zinajinasua kushuka daraja msimu huu, pia wapo wanaohitaji kuingia ‘top four’
ili kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

Ukiacha vyote hivyo, kuna timu ambazo
zitapambana kwa ajili ya kutafuta tiketi ya kushiriki michuano ya Ligi ya
Europa kwa msimu ujao.

Hayo mambo yote yanaangaliwa kwa jicho
la tatu ikiwa zimesalia mechi mbili tu Ligi Kuu ya England imalizike ikiwa
tayari kila timu mpaka sasa imecheza michezo 36 huku ikitarajiwa kumalizika Mei
12 mwaka huu.

MBIO
ZA UBINGWA

Mara ya mwisho Liverpool kutwaa ubingwa
wa Ligi Kuu ilikuwa mwaka 1990, miaka 29 imepita tangu wafanye hivyo, hivi sasa
wanaonekana kuwa na ari ya kuhitaji kushinda taji hilo.

Lakini wanapata upinzani mkubwa kutoka
kwa Manchester City ambao wanahitaji kutetea ubingwa wao ili iwe kwa mara ya
kwanza kwenye historia ya klabu hiyo.

Ukiangalia ratiba ya michezo miwili
iliyobaki kwao, Liverpool amebakiza dhidi ya Newcastle United na Wolverhampton,
inabidi wafanye kazi ya ziada ili kumaliza na ushindi katika mechi hizo.

Pia, hata Manchester City amebakisha
michezo miwili ambayo ni dhidi ya Leicester City na Brighton, nayo ni michezo
migumu kwa timu hiyo ingawa mpaka sasa wapo kileleni mwa Ligi Kuu.

Hata hivyo, Liverpool bado wapo kwenye
Ligi ya Mabingwa Ulaya ambayo watacheza dhidi ya Barcelona leo, watazidi kuwa
na ratiba ngumu tofauti na Manchester City ambao walitolewa wiki kadhaa
zilizopita na Tottenham.

UGOMVI
‘TOP FOUR’

Kama ilivyo kwenye mbio za ubingwa, hii
pia ni ngumu kumeza. Tottenham wanaongoza njia wakiwa na pointi 70, Chelsea
wanazo 68 huku Arsenal wakifuata na 66 kisha Manchester United wenye 65.

Ni ngumu kutabiri, kwa timu zote nne
zinazohitaji kuingia kwenye ‘top four’ ikiwa zimebaki mechi mbili za kucheza,
Tottenham watacheza dhidi ya Bournemouth na Everton.

Upande wa pili wa Chelsea atamaliza
ligi dhidi ya Watford na Leicester City, nao Arsenal wana Brighton na Burnley
huku Manchester United akiwasubiri Huddersfield na Cardiff City.

Ingawa, Tottenham anahitaji kushinda
mchezo mmoja tu ili awe na uhakika wa kumaliza ndani ya nne bora, huku Chelsea,
Arsenal na Manchester United kila mmoja akiombea mwenzake apunguzwe kasi ili
kuweka hai mazingira ya kuingia ndani ya ‘top four’ kibabe.

Kuna pointi sita ambazo zinagombaniwa
kwa udi na uvumba, bado mbio za kuitafuta ‘top four’ zimezidi kunoga huku kila
mmoja akisubiri kuona wapinzani wake wanapoteza au kuangusha pointi kwa kutoa
sare.

NANI
KUSHUKA DARAJA?

Ikiwa michezo miwili tu imebaki,
ni rahisi kusema imebaki nafasi moja kukamilisha timu tatu ambazo zitashuka
daraja msimu huu, ikiwa tayari klabu za Fulham na Huddersfield zikiwa zimeshuka
daraja.

Hata hivyo, Fulham wamebakisha
michezo miwili dhidi ya Wolverhampton na Newcastle huku Huddersfield wakicheza
dhidi ya Manchester United na Southampton.

Mpaka sasa inasubiriwa nafasi
moja kukamilisha tatu kwa timu ambazo zinashuka daraja msimu huu, Cardiff City
na Brighton mmoja wao yupo katika hatari hiyo.

Cardiff City wapo nafasi ya 18,
nyuma kwa pointi nne na timu iliyopo kwenye mstari wa kusalia Ligi Kuu ambayo
ni Brighton aliyebakisha michezo miwili dhidi ya Arsenal na Manchester City.

Huku Cardiff City akimaliza
ratiba yake kwa kucheza dhidi ya Crystal Palace na Manchester United, imezidi
kuwa ngumu kwa timu hizo ambazo zinahitaji kusalia katika Ligi Kuu, baada ya
michezo hiyo itajulikana timu ipi itafuata kuungana na Fulham na Huddersfield.

Pia, tayari Norwich City
imeshapanda Ligi Kuu kwa ajili ya msimu ujao huku zikisubiriwa timu mbili kwa
ajili ya msimu wa 2019/20.

EUROPA JE?

Tunapoelekea mwishoni mwa msimu
tayari kumekuwa na mijadala mbalimbali kuhusu timu ambazo zitaiwakilisha
England kwenye michuano ya Europa msimu ujao.

England kwa timu zinazoshiriki
Ligi ya Europa inatakiwa zimalize nafasi ya tano na sita lakini ikitokea kwa
timu zilizopo ndani ya sita bora zikatwaa taji la FA, itabidi klabu iliyopo
nafasi ya saba ichukue nafasi ya kushiriki Europa msimu ujao.

Yaani ikitokea Manchester City
wakashinda taji la FA msimu huu, timu iliyopo nafasi ya saba ambayo ni
Wolverhampton itabidi wachukue nafasi hiyo.

Hata hivyo, mbio za kushiriki
Ligi ya Europa zimezidi kuwa kali kwa timu za Wolverhampton, Leicester City,
Everton na Watford wote wakiwania nafasi ya saba katika msimamo wa ligi. 

Mpaka sasa Watford watacheza
dhidi ya Manchester City katika mchezo wa fainali ya Kombe la FA, kama
wakifanikiwa kushinda taji hilo watafuzu kucheza Ligi ya Europa msimu ujao.

Share.

About Author

Leave A Reply