Sunday, August 25

HALI MBAYA *Solskjaer adai nyota kibao kuondoka United, aukubali muziki wa Man City

0


MANCHESTER, England

HAKUNA namna zaidi ya kukubali ubora wa mpinzani
wako, kocha wa Manchester United, Ole Gunnar Solskjaer, ameshindwa kujizuia kwa
kudai kuwa Manchester City ni kiboko.

Katika mchezo wa Ligi Kuu uliowakutanisha juzi usiku
kwenye Uwanja wa Old Trafford, ulikuwa muhimu kwa timu zote mbili kupata
ushindi ili kuweka mazingira sawa ya ubingwa au kumaliza ndani ya ‘top four’.

Lakini kwa upande mwingine mechi hiyo iliangaliwa na
Liverpool kwa jicho la tatu huku wakitegemea vijana wa Solskjaer washinde
mchezo huo ili kuendelea kusalia kileleni mwa ligi hiyo iliyobakiza michezo 3
kumalizika.

Manchester City waliibuka na ushindi wa mabao 2-0 na
kurejea kileleni mwa Ligi Kuu ya England huku Manchester United wakisalia
nafasi ya sita katika msimamo.

Hata hivyo, Solskjaer, alisema kuwa wapinzani wake
walikuwa bora zaidi ya kikosi chake na kudai kuwa kuna wachezaji wengi
wataondoka ndani ya timu yake.

“Manchester City lazima niwape pongezi sababu
walikuwa vizuri zaidi yetu, kipindi cha pili walibadilika na wachezaji wangu
walishindwa kuendana na kasi yao,” alisema.

Lakini upande mwingine kocha huyo raia wa Norway hakuridhishwa
na viwango vya baadhi ya wachezaji wake na kudai kuwa tayari ameshajua ambao
watabaki na watakaoondoka mwishoni mwa msimu huu.

“Naamini itakapofika muda wa kujiandaa na msimu mpya
nitakuwa na wachezaji ambao wapo tayari kujitoa kwa ajili ya timu hii,
nimeshajua nani na nani wanastahili au hawatakiwi hapa,” alisema Solskjaer.

Share.

About Author

Leave A Reply