Saturday, July 20

HAKATWI MTU

0


Vibonde hawa ukikutana nao jipange

LONDON, England

KWA mashabiki wa kandanda duniani kote, ni wazi zipo timu si za kuzipa uhakika wa kumaliza ‘top four’, ukiacha kuchukua ubingwa wa England, La Liga, Bundesliga, Serie A au Ligue 1.

Kama bado hujaelewa, hapa nazizungumzia zile ambazo hutabiriwa kushuka daraja hata kabla ya kuanza kwa ligi.

Wakati huo huo, timu zenye majina makubwa kama Real Madrid, Barcelona, Manchester City, Bayern Munich hupewa uhakika wa kutwaa taji.

Katika msimu huu wa 2018-19, zipo baadhi ya timu zilizokuwa zikionekana vibonde kabla ya kuanza kwa msimu huu wa ligi hizo kubwa tano barani Ulaya.

Hata hivyo, kinyume na matarajio ya wengi, ni Madrid na Bayern ndizo zinazopata tabu huku hizo zilizokuwa zikitabiriwa kuwa jamvi la wageni, zikizidi kuwa tishio hasa zinapokutana na timu kubwa.

Montpellier (Ligue 1)

Msimamo wa mwishoni mwa msimu uliopita ulionesha kuwa wanashika nafasi ya 10, lakini safari hii hakuna atakayeshangaa kuwaona Ligi ya Mabingwa Ulaya au Ligi ya Europa.

Ukiutazama msimamo wa Ligi Kuu ya Ufaransa ‘Ligue 1’ msimu huu, utaikuta katika nafasi ya pili nyuma ya PSG waliojichimbia kileleni.

Katika michezo yake 12, imeweza kujikusanyia pointi 25, hivyo inahitaji 11 kuwafikia matajiri hao wa jijini Paris.

Kinachoweza kuwashangaza wengi ni kwamba, Montpellier haijafungwa katika mechi 10 zilizopita, huku silaha yake kubwa ikiwa ni safu ya ulinzi.

Kwa kuwa wameruhusu mabao saba pekee katika mechi 12, ubora wa mabeki wao hautofautiani na wale wa PSG ambao pia wamepitisha idadi hiyo.

Alaves

Hakika inashangaza kuona hadi kufikia raundi ya 11 ya mechi za La Liga, Alaves inakamata nafasi ya nne, tena ikiwa imeachwa pointi nne pekee na Barca walio kileleni kwa pointi 24.

Ni kwa sababu msimu uliopita walimaliza ligi wakiwa nafasi ya 14 kwenye msimamo wa La Liga inayoshirikisha timu 20.

Msimu huu, si tu Alaves imekuwa ikicheza soka la kuvutia, bali ushindi wake dhidi ya Real Madrid na Espanyol ulionesha wazi kuwa wamekuja kivingine.

Hadi sasa, safu ya ulinzi ya vijana hao wa kocha Abelardo Fernandez imeruhusu mabao 11, wakizidiwa matatu tu na Barca.

Siri ya mafanikio yao msimu huu ni ujio wa Fernandez, beki wao wa zamani ambaye alikabidhiwa mikoba ya benchi la ufundi msimu uliopita na kuiwezesha kumaliza ligi ikiwa nafasi ya 14.

Bournemouth

Msimu uliopita haukuwa mzuri kwao kwani walimaliza ligi wakiwa nafasi ya 12, ni pointi 13 pekee zilizokuwa zimewatofautisha na West Brom walioburuza mkia na kushuka daraja.

Safari hii, mashabiki wa Ligi Kuu ya England wanawajua vizuri wabishi hao wanaofahamika pia kwa jina la ‘The Cherries’.

Tishio kubwa la Bournemouth msimu huu ni makali ya eneo lao la ushambuliaji ambalo tayari limeshafunga mabao 20 katika michezo 11, ikiwa ni zaidi ya Manchester United na Tottenham.

Jeuri yao katika eneo hilo ni uwepo wa Callum Wilson na Joshua King ambao kwa pamoja wameipa timu yao mabao 10.

Aidha, mabao ya Bournemouth yamekuwa yakitokea katika eneo la kati, ambako viungo Fraser na Brooks, wamekuwa msumari wa moto kwa mido wa timu nyingine.

Moja kati ya sababu za timu hiyo kuwa tishio, ikishika nafasi ya sita kwenye msimamo, nyuma ya vigogo Arsenal, ni benchi la ufundi chini ya kocha Eddie Howe.

Howe, ambaye ameshaiongoza timu hiyo katika mechi 400, alithibitisha kuwa ni miongoni mwa makocha waliokuja kuleta mapinduzi Ligi Kuu ya England alipochukua tuzo ya Kocha Bora wa Kipindi cha Miaka 10, kuanzia mwaka 2005 hadi 2015.

 

Share.

About Author

Leave A Reply