Sunday, August 18

Gmifrak Master; Mkali wa ‘Free Style’ anayewatamani Rosa Ree, Chemical

0


NA CHRISTOPHER MSEKENA

KARIBU tena katika safu hii ya Jiachie na Staa Wako, safu inayokukutanisha na watu maarufu kwenye sekta ya burudani ndani na nje ya Bongo na leo hii tupo na  George Michael ‘Gmifrak Master’, rapa ambaye alikuwa karibu zaidi na marehemu Godzilla aliyefariki miezi miwili iliyopita, karibu.

SWALI:
Emanuel Mwakyoso kutoka Mbeya, anauliza kwanini nguzo ya hip hop (Free Style)
haipewi nafasi kubwa Bongo?

Gmifrak: Mimi
nadhani hakuna maeneo mengi ya wasanii kuonyesha uwezo wao, hakuna hamasa
ukizingatia ni wasanii wachache wanaofanya mitindo huru, nawapongeza Micasa Lounge
kwa kutoa sehemu ambayo hip hop huwa tunaonyesha uwezo, tunapanua wigo wa
muziki wetu na tunajijenga kwa sababu ‘Free Style’ ni kitu kizuri.

SWALI: Dura
Kitogo wa Gongo la Mboto, anauliza ulikuwa karibu sana na Godzilla, je, unadhani
viatu vyake vya ‘Free Style’ nani atavivaa?

Gmifrak:
Alikuwa ni rapa ambaye namkubali kwenye ‘Free Style’, pia Nikk Mbishi, kwa hiyo
sioni wa kuvaa viatu vyake japokuwa Nikki Mbishi anafanya vizuri na ana heshima
yake.

SWALI:
Fadhili Mataruma wa Tabora, anauliza kwanini kuna wasanii wachache wa kike
kwenye hip hop?

Gmifrak: Kwa
sababu watu wengi wanaegemea katika muziki unaofanyika sana ambao ni Bongo
Fleva na nyimbo za mapenzi ila kungekuwa na mashindano ya michuano kwa
wasichana, basi tungekuwa na marapa wengi wa kike.

SWALI: Hamidu
Thomas wa Mdabi, anauliza wasanii gani wa kike wa hip hop unawakubali hapa
Bongo?

Gmifrak: Wapo
wengi ila Rose Ree namkubali, anafanya kazi nzuri japo hajaanza muda mrefu,
Chemical naamini wakijitokeza wasichana wengine wanaofanya Free Stlye, itakuwa
nzuri maana muziki wa hip hop unasikilizwa sana kipindi hiki.

SWALI: Jacob
Wamwenura wa Kibaha Kongowe, anauliza msanii gani alikuvutia ukaingia kwenye
muziki wa rap?

Gmifrak: ‘Role
Model’ wangu ni Mr Blue, toka muda mrefu namfuatilia kwenye harakati za muziki
wake na maisha anayoishi.

SWALI:
Godfrey Chikarati wa Manzese, anauliza utafanya jambo gani ili ufanye muziki wa
hip hop kwa faida?

Gmifrak:
Kikubwa ni kufanya muziki mzuri ambao utanunulika sokoni, nitafanya ngoma za
ladha tofauti tofauti ambazo zipo kwenye soko, mfano wimbo wangu wa Tatanisha
Boy unachezeka kama vile anavyofanya Billnas na nyimbo baadhi za Godzilla ambazo
zinachezeka.

SWALI: Manase
Michael wa Kigoma, anauliza wasanii gani wapya wa hip hop unawakubali?

Gmifrak:
Wapo
wengi kama Young Killer Msodoki ambaye ameendelea kuwa juu kadiri siku
zinavyokwenda, Rose Ree pia.

SWALI:
Hafidhi Ng’ange kutoka Dar, anauliza baada ya wimbo wako wa Godzilla, Battery
Low sisi mashabiki zako tutegemee nini?

Gmifrak: Kuna
kazi zinakuja ambazo naamini zitanivusha nje ya mipango ya Bongo, nashukuru
vyombo vya habari kwa kuniona na kuamua kunipa sapoti. Naamini Battery Low japokuwa
kaka Zilla hayupo, imeniongezea kitu hasa mashabiki kama wewe.

SWALI: Meshack
Mtimi wa Dodoma, anasema anapenda unavyo ‘Free Style’, je, watu gani
unaowashukuru kwa kukujengea huo uwezo?

Gmifrak:
Namshukuru Godzilla lakini pia majaji wa ‘Free Stlye’ pale Micasa Lodge kama P
The Mc, Mansulee, One The Incredible kwa sababu wanafanya kazi kubwa ya
kuwajenga wasanii wa hip hop na kuibua vipaji vipya.

Wiki
ijayo tutakuwa na msanii wa hip hop kutoka Arusha anayeishi Marekani Chindoman
aliyewahi kupitia mkasa wa kufiwa na mtoto, baada ya kuungua na moto, tuma
maswali yako kwake kupitia namba hapo juu, meseji tu.

Share.

About Author

Leave A Reply