Thursday, August 22

Dusan Tadic; Jembe linalofaa kumrithi Sanchez Old Trafford

0


LONDON, England

HATIMA ya Alexis Sanchez katika kikosi cha Manchester United
iko shakani, ikielezwa kuwa anaweza kuondoka zake wakati wa majira ya kiangazi.

Hali ni mbaya kwa nyota huyo wa zamani wa Arsenal kwani
tangu kuanza kwa msimu huu, amefunga bao moja pekee katika mechi za Ligi Kuu,
licha ya mshahara mnono wa pauni 400,000 anaolipwa kwa wiki pale Old Trafford.

Majina ya mastaa wanaotajwa kwenda kuchukua nafasi yake ni
pamoja na Gareth Bale wa Real Madrid, lakini haionekani kuwa Man United
watakubaliana na gharama za mchezaji huyo.

Badala yake ni nyota wa kimataifa wa Serbia anayeichezea
Ajax, Dusan Tadic, ndiye anayeweza kuwa mtu sahihi wa kuvivaa viatu vya Sanchez
raia wa Chile.

Licha ya umri wake wa miaka 30, Tadic ni mmoja kati ya
silaha muhimu za Ajax, akichangia robo tatu ya mabao 160 yaliyofungwa na kikosi
hicho msimu huu.

Moto wake katika mikikimikiki ya Ligi ya Mabingwa Ulaya,
hadi Ajax inatinga nusu fainali ikiziondoa Real Madrid na Juventus, Tadic
ameshafunga mabao sita na kutoa ‘asisti’ tatu, idadi ambayo haijumuishi mechi
za hatua ya awali.

Kama hiyo haitoshi, wakati Serbia inakata tiketi ya kucheza
fainali za Kombe la Dunia za mwaka jana kule Urusi, Tadic ndiye aliyeongoza
‘jeshi’, akizifumania nyavu mara nne katika mechi za kufuzu.

Si tu Tadic ana uzoefu na Ligi Kuu ya England, ikikumbukwa
kuwa aliwahi kuichezea Southampton kwa misimu minne. Alisajiliwa mwaka 2014,
kipindi ambacho kikosi hicho kilikuwa kikinolewa na kocha wa kimataifa wa
Uholanzi, Ronald Koeman.

Akiwa England, wengi watakumbuka rekodi yake ya kuwa
mchezaji mwenye ‘asisti’ nyingi katika mechi moja ikiwa ni baada ya pasi zake
za mwisho kuzaa mabao manne katika ushindi wa mabao 8–0 dhidi ya Sunderland.

Pia, wachambuzi wa soka barani Ulaya, wanasema atakuwa
msaada mkubwa kwa Man United kwa kuwa ni mchezaji mwenye uwezo wa kucheza
nafasi mbalimbali uwanjani ‘kiraka’. 
Mbali ya kuwa anaweza kutumika kama mshambuliaji wa kati, pia ni hatari
anapotokea kushoto.

Akiungana na washambuliaji waliopo Old Trafford, Romelu
Lukaku na Marcus Rashford, inaweza kuwa moja kati ya kombinesheni za kumtuliza
kichwa Ole Gunnar Solskjaer, ambaye kwa sasa ni kama amevurugwa.

Hata linapokuja suala la mkwanja wa kumnasa, Tadic hazidi
euro milioni 30, bei ambayo Mashetani Wekundu hawawezi kumpata Bale, ambaye
hata hivyo si wa kumtegemea sana kutokana na majeraha yake ya mara kwa mara.

Share.

About Author

Leave A Reply