Thursday, August 22

Diamond, baba yake mambo poa, Zari akana kuchepuka

0


NA CHRISTOPHER MSEKENA

HATIMAYE staa wa Bongo Fleva, Naseeb Abdul ‘Diamond
Platnumz’, amemaliza tofauti alizokuwanazo na baba yake mzazi, Abdul Juma
ambaye hakuwahi kuonana naye kwa miaka 20 zaidi ya kuwasiliana kwenye simu.

Hatua hiyo ilikuja baada ya wawili hao kukutanishwa
kwa ‘surprise’ katika Studio za Wasafi Fm, ambapo Diamond Platnumz alikwenda
kuzindua kipindi cha Block 89 na kuzungumza mambo mbalimbali ambayo mashabiki
wamekuwa wakitaka kuyajua kuhusu familia, muziki na mengineyo.

Awali, barua ya wazi ya baba Diamond ilisomwa hewani
ikimtaka Diamond amsamehe kama kuna kosa aliwahi kulifanya, asisubiri mpaka afe
kwani atakuwa hana radhi naye kama mzazi wake hivyo anapenda waonane wamalize
tofauti zao.

Akizungumzia ishu hiyo, Diamond Platnumz alisema:
“Mimi siwezi kusema baba yangu amenikosea, nimsamehe mimi amenikosea nini? Walikuwa
na matatizo yeye na mama nikashindwa kulelewa pamoja na wazazi wote wawili.
“Siwezi kusema nina ukaribu sana na mzee wangu utakuwa uongo, kwa sababu sikukua
naye lakini siku zote huwa namwambia akiwa na jambo aniambie nitamtimizia, kumbukumbu
zangu mara ya mwisho tunaachana na mzee hakuwa masikini, alikuwa na fedha, majumba
na magari yake, anajiweza kwa hiyo sikuweka akilini kama mzee hana kitu
anahitaji nimhudumie kila mwezi tofauti na mama ambaye najua anahitaji
nimhudumie.”

Naye baba Diamond Platnumz alisema: “Unajua mimi si
mtu wa kuomba msamaha, mara nyingi mzazi akikosa anakuwa hana kosa ila nilikuwa
naona kitu cha ajabu kuona mama yake anakwenda naye sawa, lakini mimi kila
nikimwandikia meseji zangu hajibu halafu anakuja kuwapa sapoti watu wengine,
ndiyo maana nilitaka kujua kitu gani cha ajabu nilichokifanya mpaka asinisamehe,
naomba unisamehe tuendelee kuishi vizuri.”

Baada ya wawili hao kukutanishwa na kufanya
mazungumzo marefu yaliyovuta hisia za wengi, wakapiga picha ya pamoja kuonyesha
kumaliza tofauti zao.

Aidha, katika mahojiano hayo Diamond Platnumz aligusia ishu ya kuachana na mama watoto wake, Zari The Boss Lady, kuwa ni usaliti kwani wakati wapo kwenye uhusiano mrembo huyo wa Kiganda alikuwa anachepuka.

“Baada ya kutengana na mwezangu ilikuwa tofauti kwa
sababu ana ‘play fair’ mtandaoni lakini kiuhalisia hafanyi hivyo, kila mwezi
natuma dola 2,000 sawa na shilingi milioni nne kwa ajili ya matunzo ya watoto ila
nina miezi miwili au mitatu sijatuma.

“Ni mtu ambaye namheshimu kwa sababu amenizalia,
nilikuwa nampenda lakini mwenzangu alikuwa ananipenda sana, kitu kibaya
alichowahi kunifanyia alikuwa anatoka na Peter wa P Square, nimeshakuta hadi
meseji zao lakini pia mwalimu wake wa mazoezi alikuwa anatokana naye wanakuja
mpaka nyumbani kwangu, lakini mimi si mtu wa kuongea sana nakausha, japokuwa na
mimi ni mwendawazimu kweli, mimi sijawahi kuachwa, mwanamke akinikorofisha
namchapa matukio mpaka anaondoka mwenyewe,” alisema Diamond.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Zari alijibu
mapigo kwa kukanusha tuhuma hizo akisema: “Kamwe usimwamini mwanamume ambaye
alikwenda redioni kuikataa damu yake, mtoto wake Dully (aliyezaa na Hamisa
Mobetto) na kumwambia mwenye mimba yake ajitokeze leo unauamini vipi mdomo
ulioongea uongo, naomba tuheshimiane.”

Mobetto
atoa siri ya kupata dili

NA JEREMIA ERNEST

MWANAMITINDO Hamisa Mobetto amesema heshima aliyojiwekea katika jamii ndiyo siri kubwa inayofanya kampuni nyingi zihitaji kumtumia kama balozi wa bidhaa zao.

Mobetto ambaye hivi karibuni aliingia mkataba wa
kuwa balozi wa vipodozi vya Tridea ambayo katika msimu wa Pasaka ilikuwa
ikigawa zawadi kwa wateja wake jijini Dar es Salaam, alisema anamshukuru meneja
wake, Maxmillia Rioba ambaye amekuwa akimwongoza vizuri.

“Nimekuwa nikiheshimu wakubwa na wadogo lakini pia
katika mikataba ambayo nimeingia, ninajenga nidhamu na heshima hiyo ndiyo
sababu inayovutia  kampuni nyingine kuja
kunitumia,” alisema Mobetto ambaye pia ni Balozi wa Dstv, Tridea na Dar
Ceramica.

Magreth Sembuche kuzindua kitabu, albamu Dodoma

NA MWANDISHI WETU

MWIMBAJI wa nyimbo za Injili, Magreth Sembuche, anatarajia kufanya uzinduzi mkubwa wa kitabu cha Kanisa Lisilo Onekana na albamu yake ya Sioni Vita Wala Mapigano Mei 5, mwaka huu katika Kanisa la Anglicana, Dodoma Mjini.

Akizungumza na Papaso la
Burudani, Magreth alisema uzinduzi huo utapambwa na waimbaji mbalimbali hivyo
wapenzi wa muziki huo wanakaribishwa kuhudhuria kwa wingi.

“Uzinduzi utafanyika kuanzia
saa 6:00 mchana, kutakuwa na waimbaji kama Edson Mwasabwite, Emmanuel Mgogo,
Rebeca Magaba, Mc Joyce Ombeni na kwaya mbalimbali zitakuwepo kumtukuza Mungu,”
alisema Magreth.

‘Like Jesus’ ya Doxel yatua Bongo

KINSHASA, KONGO

MWANAMUZIKI kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Jonathan Doxel, ameshangazwa na upendo alioonyeshwa na mashabiki wa muziki Tanzania kwa kuipokea vyema video ya wimbo wake, Like Jesus.

Doxel, ameliambia Papaso la Burudani kuwa
wimbo huo kutoka kwenye albamu yake ya Wake Up umekuwa baraka kwa wengi na
anashukuru kuona umepokewa kwa kishindo na Watanzania.

“Mungu ameendelea kuachilia baraka zake,
mapokezi yamekuwa makubwa hapo Tanzania, nashukuru na sasa video yangu ipo
YouTube watu wanaweza kuiona,” alisema Doxel.

Pierre
anogesha Kesho ya Dragon

NA JEREMIA ERNEST

MNYWAJI wa pombe maarufu zaidi mtandaoni kwa sasa, Peter Mollel ‘Pierre’, ameendelea kupasua anga la mafanikio mara baada ya msanii wa Bongo Fleva, Juma Ramadhan ‘Dragon’, kumshirikisha katika wimbo Kesho.

Akizungumza na Papaso la Burudani, Dragon alisema
anashukuru wimbo huo umepata mapokezi makubwa tofauti na alivyotarajia kutokana
na Pierre kuonyesha uwezo wa hali ya juu.

“Nashukuru wadau kwa kuupokea vyema wimbo wangu, umepata
mapokezi makubwa kuliko matarajio yangu, Pierre ana uwezo katika sanaa,”
alisema Dragon.

Share.

About Author

Leave A Reply