Friday, May 24

De Rossi ; Nahodha shupavu anayeacha historia nzito AS Roma

0


ROME, Italia

MSIMU huu umekuwa mgumu kwa timu ya AS Roma, ingawa ni jambo
linalotegemewa katika mchezo wa soka. Kitu pekee ambacho Waitaliano hao
hawakukitarajia ni kuondoka kwa nahodha wao, Daniele De Rossi.

De Rossi ambaye amedumu na ‘Giallorossi’ hao kwa muda wa
miaka 18, akiitumikia katika michezo zaidi ya 600, alitangaza kuwa ataiacha
klabu yake hiyo ifikapo mwishoni mwa msimu huu huku akiacha rekodi
isiyoridhisha.

Ikumbukwe kuwa nahodha huyo aliisaidia timu hiyo kutinga
hatua ya nusu fainali Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka jana, lakini hali imekuwa
mbaya msimu huu hadi kushuhudiwa kocha wao, Eusebio Di Francesco, akitimuliwa.

Hata hivyo, mambo yalianza kutulia baada ya ujio wa kocha, Claudio
Ranieri, ambapo Roma waliweza kucheza mechi saba mfululizo bila kupoteza, lakini
matokeo hayo hayakutosha kuipandisha Roma hadi katika nafasi nne za juu.

Zikiwa zimesalia mechi mbili kabla ya kumalizika kwa Ligi
Kuu Italia msimu huu, Roma inashikilia nafasi ya sita, pointi tatu nyuma ya Atalanta,
lakini wakizidiwa kwa tofauti kubwa ya mabao.

De Rossi ataiacha Roma, lakini hatastaafu soka moja kwa moja
kama ilivyokuwa na mkongwe mwenzake, Francesco Totti, ambaye alistaafu mwaka 2017
baada ya kuitumikia Roma kwa muda wa miaka 24.

Kiungo huyo mwenye shughuli pevu dimbani, anatarajia
kufikisha umri wa miaka 36 ifikapo Julai mwaka huu, lakini anaonesha kuwa bado
ana kitu cha kuendelea kufanya uwanjani.

Licha ya kwamba atakapoiacha Roma na kile cheo cha ‘mchezaji
wa timu moja’ hakitamhusu tena De Rossi, lakini mchango wake kwa vigogo hao wa
Serie A hautasahaulika kamwe.

Ni sawa na ilivyo kwa watu kama Xavi au Andres Iniesta, walipoondoka
Barcelona. De Rossi atabaki kuwa nahodha wa Roma na hatafutika katika mioyo ya
mashabiki wa klabu hiyo.

Mkongwe huyo aliibuka kwenye kikosi cha wakubwa Roma muda
mfupi baada ya klabu hiyo kutwaa taji lao la mwisho la Serie A mwaka 2001. Alicheza
mechi yake ya kwanza Oktoba mwaka huo, mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi
ya Anderlecht.

Alianza kutumika mara kwa mara katika kikosi cha kwanza ilipofika
mwaka 2003, lakini haikuchukua muda mrefu hadi ilipoonekana kuwa umuhimu wake
ni mkubwa ndani ya timu.

De Rossi alianza kutumika katika timu yake ya Taifa ya
Italia mwaka 2004 wakati wa michuano ya Mataifa Ulaya kwa vijana chini ya umri
wa miaka 21, ambapo walitwaa taji la mashindano hayo.

Baada ya hapo akaanza kupewa majukumu ya kucheza timu ya
taifa iliyokuwa chini ya kocha, Marcello Lippi.

Hadi anafanikiwa kutwaa tuzo ya Chipukizi Bora wa Mwaka Serie
A (2006), uwezo wa De Rossi, ulishaonekana na kila mtu; kiungo mwenye uwezo
mkubwa wa kufanya kazi zote katikati ya uwanja.

Roma na Italia kwa ujumla walivutiwa mno na uwezo wake wa
kupokonya mipira na kupiga pasi za kila aina, ingawa hakuwa maarufu sana katika
eneo hilo la pasi kama alivyokuwa Andrea Pirlo.

De Rossi anaondoka Roma na kumbukumbu nyingi, mojawapo ni
kichapo kikali cha mabao 7-1 walichokipata kutoka kwa Man Utd, Aprili 2007, katika
mchezo wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Katika mtanange huo uliowasikitisha mashabiki wa Roma
waliosafiri na timu yao hadi kwenye dimba la Old Trafford, De Rossi ndiye
aliyefunga bao la kufutia machozi kwa upande wa timu yake.

Mwaka uliofuata, nuksi ya Old Trafford ilimwandama tena De
Rossi na safari hii alishindwa kufunga bao kwa penalti na kuipa tiketi Manchester
Utd ya kucheza nusu fainali hadi kuwa mabingwa wa UEFA.

Hata hivyo, katikati ya mechi hizo mbili dhidi ya Man Utd, ambazo
De Rossi hatapenda kuzikumbuka, Roma ilifanikiwa kunyakua mataji mawili
mfululizo ya Coppa Italia.

Misimu mingine ambayo ilikuwa ni mitamu kwa De Rossi,
ilikuwa ni 2007/08 na 2008/09, ambapo akiwa chini ya kocha Luciano Spalletti, kiungo
huyo aliweza kucheza jumla ya mechi 94 na kufanikiwa kunyakua tuzo ya Mchezaji
Bora wa Mwaka Serie A (2009).

Kuanzia hapo sasa klabu kadhaa barani Ulaya zikaanza
kumuwinda De Rossi. Kuna wakati iliibuka hofu dhidi yake licha ya Roma kumpa
mkataba mpya wa miaka mitano ilipofika Ferbuari 2012.

Kwanini walikuwa na hofu kwa De Rossi? Wengi walidhani
pengine kiungo wao huyo atashawishika kuondoka na kujaribu kwingineko, japokuwa
mkataba mpya ulimfanya awe mchezaji anayelipwa zaidi Serie A.

Klabu kama Man City na Man United zilihusishwa naye, lakini
kwa sababu alishaamua kuwa maisha yake yote ni Roma, De Rossi alithibitisha
kwamba atabaki kuwa mwana-Giallorossi.

Msimu wa 2013/14, De Rossi na Roma iliyokuwa ikinolewa na
kocha, Rudi Garcia, walikaribia kuwa mabingwa wa Serie A kwa mara ya kwanza
tangu mwaka 2001, wakishinda mechi zao 10 za awali.

Hata hivyo, sare mfululizo zilizima ndoto zao na vikafuatia
vichapo mfululizo mwishoni mwa msimu kabla ya kujikuta ikimaliza nyuma ya
Juventus kwa tofauti ya pointi 17.

Inasikitisha kumwona De Rossi akimaliza miaka yake 18 ya
kuitumikia Roma bila taji la Serie A, lakini yeye na Totti watakumbukwa milele
na mashabiki wao kutokana na kuithamini na kuiheshimu nembo ya klabu yao.

Kokote atakapoenda, De Rossi, hatasahaulika na watu wa Roma.

Share.

About Author

Leave A Reply