Sunday, August 25

‘DANI ALVES’ Mkulima aliyetusua katika soka akiongoza kwa mataji ulimwenguni

0


LONDON, England

WAKATI PSG
wakilitetea taji la Ligi Kuu ya Ufaransa ‘Ligue 1’ wikiendi iliyopita, Dani
Alves alikuwa anaandika historia ya kuwa mchezaji aliyekusanya vikombe vingi
zaidi katika ulimwengu wa soka.

Hilo lilikuwa
taji la 42 kwa nyota huyo wa Kibrazil mwenye umri wa miaka 36, hivyo alimpiku
mshambuliaji wa zamani wa Zamalek na timu ya taifa ya Misri, Hossam Hassan,
ambaye hadi anatangaza kustaafu alikuwa na 41.

Pia, amezidi
kumwacha mbali aliyekuwa kiungo hatari wa Barcelona, Andres Iniesta, ambaye
anashikilia mataji 37 kama ilivyo kwa beki wa Barca, Maxwell na mkongwe wa
Misri, Ibrahim Hassan.

Alikuwa winga,
baba akamng’oa

Alves, mzaliwa wa
Juazeiro, jiji linalopatikana katika Jimbo la Bahia, ni mtoto wa mkulima, mzee Domingos
Alves da Silva ambaye inaelezwa kuwa alikuwa na kwaida ya kumfanyisha mwanawe
kazi hiyo.

Hata hivyo, Alves
alipenda soka akionekana mara kadhaa akicheza na marafiki zake. Akiwa na umri
wa miaka sita, Alves alikuwa akicheza winga lakini kwa kuwa hakuwa mfungaji
mzuri, ndipo baba alipotaka awe beki wa kulia, nafasi anayocheza hadi leo hii.

Alivyoanza kuwa
staa

Ukweli ni kwamba
nyota yake ilianza kung’ara mwaka 2011, akiwa na kikosi cha Bahia ya Ligi Kuu
ya Brazil, ambayo aliipa mara mbili taji la Copa do Nordeste na Campeonato
Baiano.

Uwezo wake wa kupandisha mashambulizi na kuwazima washambuliaji wasumbufu uliwavuta Sevilla ingawa hakushinda taji lolote kwa misimu yote mitatu ya mwanzo klabuni hapo.

Hata hivyo, mwaka
2006 aliipa ubingwa wa Uefa Cup, ambalo pia waliweza kulitetea msimu uliofuata,
wakishinda pia taji la Uefa Super Cup.

Aliweza pia
kunyakua Copa del Rey, kabla ya kuchukua Spanish Super Cup kwa kuitandika Real Madrid katika mtanange wa fainali.

Ni kipindi hicho ndipo Alves aliposhinda taji lake la kwanza akiwa na timu ya taifa ya Brazil, walipoichapa Argentina na kutwaa ubingwa wa Copa America.

Alivyomkomesha shabiki La Liga

Alitua Barca
mwaka 2008 na kwa kipindi chote cha miaka nane alichokaa Camp Nou, ameweza
kuchangia upatikanaji wa mataji 23, yakiwamo ya La Liga (6) na Ligi ya Mabingwa
Ulaya (3).

Kwa upande
mwingine, maisha yake ya soka katika klabu hiyo yana kisa cha shabiki wa
Villarreal katika moja ya mechi za La Liga. Shabiki huyo aliyefahamika baadaye
kwa jina la David Campaya Lleo, alitupa ndizi karibu na Alves, ikiwa ni ishara
ya ubaguzi wa rangi.

Tofauti na nyota
wengine wenye asili ya Afrika ambao mara nyingi hulalamikiwa waamuzi au
kuwajibu kwa ishara mbaya mashabiki wanaowafanyia vitendo hivyo, Alves
aliinama, akaichukua, akaila ndizi na kisha kuendelea na kazi zake uwanjani.

Baadaye, alisema
ili kukabiliana na uhuni huo mchezaji anayefanyiwa hivyo hapaswi kulipa umuhimu
suala hilo na badala yake afanye kazi iliyompeka uwanjani.

Mke wa zamani ndiye wakala

Kuna stori ya
kusisimua juu ya wakala wa Alves, Dinora Sanata. Wawili hao walikuwa wapenzi
kuanzia mwaka 2005, kabla ya kufunga ndoa miaka mitatu baadaye na kisha
kubahatika kupata watoto wawili.

Lakini, ndoa yao haikudumu
zaidi ya miaka mitatu, sababu ikitajwa kuwa ni Alves kubainika kutoka kimapenzi
na mwigizaji mwenye jina kubwa nchini Brazil, Thaissa Carvalho.

Hata hivyo, licha
ya kutwangana talaka mwaka 2011, bibiye huyo ameendelea kuwa karibu kibiashara
na Alves, akiwa ndiye wakala anayesimamia dili zote za usajili. Si tu katika
soka, pia wawili hao wanamiliki kwa pamoja kampuni tano, zikiwa za kilimo,
ukiacha kuwa ni majirani huko Paris, Ufaransa.

Hivi sasa, Alves
ni mume wa mwanamitindo wa Kihispania, Joana Sanz, ambaye amekuwa akishiriki
mashindano makubwa ya tasnia hiyo nchini Ufaransa, Paris Fashion Week.

Utajiri

Kufikia mwishoni
mwa mwaka jana, jarida la Forbes lilimtaja mkali huyo kuwa na utajiri wa Dola
za Marekani milioni 60 (zaidi ya Sh bil 137 za Tanzania). Kwa mujibu wa jarida
hilo, ilitabiriwa kuwa mwaka huu kiasi hicho kitaongezeka na kufikia Dola
milioni 100.

Ukiacha dili za
matangazo kutoka kampuni mbalimbali, mshahara pekee ungetosha kumpa jeuri staa
huyo kwani pale PSG anakunja si chini ya Dola 290,572 (zaidi ya Sh mil. 600)
kwa wiki.

Share.

About Author

Leave A Reply