Wednesday, August 21

CHID BENZ; HAPA NDIPO TUNAPOSHINDWA KUKUELEWA – Bingwa

0


NA ZAITUNI KIBWANA

WIKI  iliyopita Rashid Makwilo ‘Chid Benz’, alishangaza watu kwa kudai amefanya kolabo na wasanii maarufu duniani kama Jada Kiss, R-Kelly, 50 Cent, huku akisisitiza kuwa ana wimbo aliorekodi na rapa Jay Z na anatarajia kuutoa hivi karibuni.

Katika hali ya kushtusha, Chid alisema ana nyimbo nyingine alizoimba pamoja na mkali wa Pop, Christina Aguillera pamoja na Lil Wayne!

Chid Benz alisisitiza kuwa hajachanganyikiwa wala hajavuta madawa ya kulevya kama watu wanavyodhani na atazitoa nyimbo hizo hivi karibuni.

Hii si mara ya kwanza Chid Benz kushangaza na kauli zake tata, amewahi kutoa kali ya mwaka kwa kudai kufanya kolabo na Tupac ambaye kwa sasa ni marehemu.

Tupac ambaye wanadunia wengi wanaamini jamaa alivuta toka mwaka 1996, Chid Benz anasema yupo hai huko Cuba na atafanya mpango wa kumleta Bongo.

Hapa ndipo tunaposhindwa kumuelewa Chid Benz, hakuna asiyejua Tupac alifariki dunia kwa kupigwa risasi mwaka 1996 akiwa na miaka 25, ikiwa ni dakika kadhaa baada ya kutoka kwenye pambano la Mike Tyson.

Wakati bado tunaendelea kushangazwa na kauli hizo, anaibuka eti ana wimbo ambao Beyonce kamshirikisha kwenye chorus japo anataka kumtoa na kumuweka msanii Linah Sanga.

Hatukuelewi Chid Benz! Umekumbwa na nini? Tupac huyu huyu anayetimiza miaka 22 toka alipofariki, leo hii unataka kufanya naye kolabo? Bado umetuacha na viulizo kaka.

Tunatambua una akili zako timamu lakini  Jay Z huyu huyu ambaye tunamfahamu mwenye ‘couple’ ya muziki yenye pesa nyingi zaidi nchini Marekani ndio ufanye naye wimbo, hapa utakuwa labda umeteleza kaka.

Ngoja labda nikuulize, unatumia nini kama starehe? Ganja, fegi ama mitungi? Kama unatumia kati ya hivyo basi ujue ipo siku atakuja kutwambia umeonana na Kanali Muammar Gaddafi.

Mwenye akili timamu akitafakari kwa kina haya matamshi yako, anaibuka na maswali mengi mno japo unadai upo sawa na hutumii kileo chochote kwa sasa.

Au labda kaka una msongo wa mawazo? Mana upo wa aina nyingi, wapo wanaoongea peke yao, baadhi wanatembea kama wanarudi nyuma na wengine hata hawajui wanaenda wapi.

Wapenda burudani labda wangekuelewa ungeibuka na kauli ya kuhakikisha unarudisha jina lako ambalo limeanza kusahaulika kwenye gemu kutokana na kushindwa kutoa nyimbo kali na kuzidiwa na vijana.

Hakuna ubishi, Chid Benz kwa sasa amefulia na amepotea kabisa kwenye ‘game’ kutokana na kushindwa kuendana na kasi ya vijana ambao wamekuwa wakitoa nyimbo kali kila kukicha.

Wapenda burudani hawashangai anguko lako baada ya kupoteza dira hasa baada ya kujiingiza kwenye matumizi ya dawa za kulevya.

Chid Benz alikiri kuathirika na dawa za kulevya na akapata msaada wa kupelekwa kwenye kituo cha ushauri nasaha na uangalizi kilichopo Bagamoyo mkoani Pwani.

Huku alikaa kwa muda mfupi akarudi mjini kuendelea na harakati zake kama kawaida na baadaye tukasikia amekamatwa tena mkoani Dodoma kwa tuhuma za kukutwa na dawa za kulevya.

Kwa ujumla Chid Benz anaumwa na anahitaji msaada. Licha ya kutokusema hasa anaumwa nini, matamshi yake tu yanaonyesha hayupo sawa.

Kiuhalisia Chid Benz anahitaji msaada wa kiafya na kisaikolojia ili aweze kurejea kwenye hali yake ya kawaida.

Nawaomba wasanii na Watanzania wamsaidie Chid Benzi aweze kupona na kurudi katika afya yake ya kawaida na aweze kutoa ngoma kali zitakazomrudisha kwenye chati.

The post CHID BENZ; HAPA NDIPO TUNAPOSHINDWA KUKUELEWA appeared first on Bingwa.Read More

Share.

About Author

Comments are closed.