Sunday, August 25

BAADA YA WAMBURA KUFUNGIWA… – Bingwa

0


Karia: Sitamwacha mtu salama

* Atoboa siri ujio wa Rais wa FIFA, aeleza umafia aliofanyiwa na Malinzi

NA MWANI NYANGASSA

RAIS wa Shirikisho la soka nchini (TFF), Wallace Karia, ametema nyongo akieleza kuwa hatomuacha salama mtu yeyote atakaecheza na fedha za shirikisho hilo na kufanya udhalimu katika mpira, hata kama ni rafiki yake.

Karia alitoa kauli hiyo ikiwa ni siku chache tu, tangu Kamati ya Maadili ya TFF imfungie maisha Makamu wa Rais wa shirikisho hilo, Michael Wambura na ugeni mkubwa wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) chini wa Rais wake Gian Infantino uondoke nchini.

Rais huyo aliyasema hayo mbele ya Wahariri wa Habari za Michezo wa vyombo mbalimbali, katika mkutano wake wa kueleza utekelezaji wa TFF juu ya mambo mbalimbali, ambapo alitamka wazi yupo tayari kulaumiwa.

“Niseme tu unaposafisha taasisi kuna gharama zake, TFF inahitaji kuungwa mkono zaidi kwa hatua madhubuti inazochukua za kujisafisha na kusonga mbele, suala la kupambana na vita ya udhalimu kwenye mpira wetu hatutarudi nyuma, tutapambana bila hofu wala woga ilimradi hakuna dhuluma, uonevu wala upendeleo kwa yeyote.

“Natoa wito kama kuna kiongozi au mdau yoyote anayejua ana pesa za TFF kinyume na utaratibu ajisalimishe mwenyewe, ndio maana wakati nachaguliwa niliahidi kusimamia taasisi kwa uadilifu mkubwa bila kumuonea aibu mtu yeyote, wala kumuogopa mtu na hii ni katika kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli za kupambana na uchafu  wa aina zote katika Serikali.

“TFF kuna Magufuli mwingine, masuala ya mchezo na fedha, udhalimu hapana, si masuala hayo peke yake hata waamuzi tunashughulika nao, ile ni kansa kubwa, nimeamua kusafisha taasisi kama nilivyoahidi wakati wa kampeni za uchaguzi ulioniweka madarakani, niseme wazi hakuna mtu asiye muadilifu atabaki katika mpira.

“Nimpongeze Kaimu Katibu Mkuu wangu, Wilfred Kidau, kwa kusimamia kwa ujasiri mkubwa usimamiaji wa maagizo yote halali ya Kamati mbalimbali, amekuwa anasimamia bila uoga bila kujali anavyosakamwa, kwangu linanipa faraja sana,” alisema.

Alieleza TFF, imekuwa ikichukuwa hatua katika kila eneo, wameanza kuchukuwa hatua kwa wizi wa mapato ya milangoni, ndio maana kuna viongozi wamefungiwa, tayari viongozi walioghushi leseni za usajili wamefungiwa, yote ni kuonyesha hana masihara hata kidogo kwenye kuhakikisha mpira unakuwa sehemu ya watu waadilifu.

Akitolea ufafanuzi suala la Fifa Karia alisema, “Fifa walituma timu ya uchunguzi kuangalia yale yote yaliyofanyika tangu mwaka 2013 mpaka mwaka 2017, timu ilikaa nchini kwa takribani wiki mbili ikifanya kazi kwa karibu na Ofisi ya Katibu Mkuu, yaliyogundulika yameacha doa kubwa na walitoa ripoti na maelekezo ya mambo ya kuyafanyia kazi na ya kuchukulia hatua.

“Masharti yote haya yaliambatana na kuzuiwa kwa fedha za miradi yaliyosababishwa na wenzetu wachache, lakini TFF imekosa fedha zinazoitwa ‘Operation Cost’ ikiwa ni shinikizo la Dola Milioni 3 za Marekani (sawa na Sh bilioni 6.7) ambazo tulipaswa kulipwa tangu mwaka 2015-2018.

Karia alisema karibia nchi zote duniani zimenufaika kwa kupata fedha  hizo isipokuwa Tanzania ambayo inatakiwa kuhakikisha inanatekeleza masharti ya Fifa, hivyo walipopata ripoti wameamua kutekeleza kwa asilimia mia moja maagizo yote ya Fifa.

“Haya yanayotokea ni miongoni mwa matokeo ya utekelezaji wa taarifa za wakaguzi wa TFF na wakaguzi na timu ya uchunguzi kutoka Fifa, jambo hili limepitia hatua stahiki kwa mujibu wa taratibu zinazohusiana na taarifa za kiukaguzi, wahusika wameshirikishwa ipasavyo na utetezi wao walipeleka kwenye kamati husika ya ukaguzi miezi iliyopita baada ya kutakiwa kufanya hivyo kwa mujibu wa taratibu.

“Sijui kama watu wanajua kwanini Infantino alikuja Tanzania, alikuja kwa kuwa anamuunga mkono Rais Magufuli na katika kipindi kifupi, amegundua kila senti tano inayoingia inatumika kikamilifu, ndio maana akaenda kumweleza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, si wanaondoka halafu wanasikia kuna mtu anachukua tena hela,” alisema.

Hata hivyo, Karia alielezea kuhusu vyombo vya maamuzi vya TFF vinavyofanya kazi, akieleza zinafanya kwa mujibu wa katiba yake ya mwaka 2013 na kufanyiwa marekebisho mwaka 2015.

Katiba hiyo inataka Kamati ya Utendaji kufanya kazi na vyombo mbalimbali ambavyo ni kamati ndogondogo, Bodi ya Ligi na Kamati za Kisheria pamoja na Kamati za Uchaguzi.

Karia pamoja na kugusia kamati zote, aligusia kamati ya maadili iliyomuhukumu Wambura ambayo ipo ndani ya Kamati za kisheria za TFF

Alitoa ufafanuzi, “Ufanyaji wa kazi wa kamati hizi umeelezewa katika Katiba ya TFF kwa maana Kamati za Kisheria zinajitegemea, huwa haziingiliwi kwenye maamuzi yake, ingawa vikao vyake vyote huwa vinaratibiwa na ofisi ya Katibu Mkuu.

“Kwa hiyo maamuzi ya kamati hizi huwa ni ya kujitegemea, hivyo watu wote ambao wamekuwa wanahukumiwa na kamati hizi ni vema wakawa wanajua utaratibu wa kamati zinavyofanya kazi na mimi binafsi nimeendelea kuheshimu kamati zifanye kazi bila kuingiliwa na mtu yoyote yule,” alisema Karia.

Lakini Karia hakuacha kueleza hisia zake juu ya aliyekuwa Rais wa TFF, Jamali Malinzi, ambapo aliweka wazi kuwa kwa sasa hawezi kumlaumu kwa aliyoyafanya wakati wa uongozi wake kwani aliyafanya kwa kufuata katiba ila atamlaumu kwa kumnyima haki yake  ya kuingia katika vikao vya Kamati ya Fedha.

“Mimi nilitulia miaka minne kwa kuwa nilikuwa naijua katiba, wakati nagombea nilijua nitaenda kumsaidia Malinzi lakini niliposoma katiba nilielewa na kutulia tu,” alisema.

Aidha, Karia alielezea suala la mapato na matumizi katika kipindi cha miezi saba, akiweka wazi kuwa shirikisho limefanikiwa kukusanya kiasi cha Sh bilioni 3.6 kutoka katika vyanzo mbalimbali, ambavyo ni kama wadhamini Sh bilioni 2.2 sawa na asilimia 62.5 ya mapato yote, makusanyo ya viingilio uwanjani milioni 378 sawa na asilimia 10.3%, huku  asilimia 27.2 ikitokana na fedha kutoka Fifa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Alieleza kuwa matumizi ya fedha hizo katika kipindi hiki, shirikisho lilitumia kiasi cha Sh bilioni 3.7 na sehemu kubwa ya matumizi yalielekezwa kwenye usimamizi wa ligi mbalimbali, pamoja na kuandaa timu za taifa ambapo jumla ya Sh bilioni 2.4 sawa na asilimia 64 ya matumizi yote zilitumika.

“Asilimia 36 ya fedha zilizobaki zilitumika kulipia madeni ya taasisi, kama mishahara ya wafanyakazi, kusaidia mikoa katika maeneo ya miundombinu, kuwajengea uwezo wafanyakazi pamoja na kuendesha mafunzo mbalimbali.

Aliweka wazi kuwa shirikisho lilianza zoezi la kutathmini madeni iliyoyarithi kutoka kwenye uongozi uliopita, ambapo deni hilo linafikia Sh bilioni mbili linalodaiwa na watoa huduma mbalimbali, wafanyakazi, wachezaji na makocha na asilimia kubwa ya deni lilitokana na malimbikizo ya deni la Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ‘Workers Compensation Fund’ na NSSF ambalo lililimbikizwa kwa zaidi ya miaka miwili.

“Shirikisho lilifanikiwa kulipa deni lote la michango ya wafanyakazi NSSF jumla ya Sh milioni 88, zilizokuwa hazijalipwa kipindi cha miaka miwili na lilifanya majadiliano na TRA kuhusu ulipaji wa deni la Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) linalofikia Sh bilioni moja, ambapo jumla ya Sh milioni 315 zimelipwa na kiasi kilichobaki tumekubaliana kitalipwa kwa awamu kadhaa mpaka deni lote litakapomalizika,” alisema.

Aliongeza kuwa, shirikisho limefanikiwa kupunguza mishahara kwa wafanyakazi kutoka Sh milioni 85 mpaka kufikia milioni 50 baada ya kupunguza idadi ya wafanyakazi kutoka 44 hadi 21.

“Baada ya kuingia madarakani tulifanya majadiliano na makocha wa timu za Taifa kuhusu uhalisia wa malipo yao na kufanikiwa kuokoa zaidi ya Dola 200,000 za Marekani (Sawa na Sh milioni 450) kwenye mikataba yao na fedha zilizookolewa zitasaidia shughuli nyingine za mpira wa miguu” aliongeza.

The post BAADA YA WAMBURA KUFUNGIWA… appeared first on Bingwa.Read More

Share.

About Author

Comments are closed.