Tuesday, March 19

Azam FC mzigoni kuivaa Stand leo

0


MAREGES NYAMAKA NA WINFRIDA MTOI

KOCHA Mkuu wa Azam FC, Hans van der Pluijm, leo atakiongoza kikosi chake katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Stand United ya mkoani Shinyanga, huku akiwa na matumaini ya kuvuna pointi tatu.

Mchezo huo unatarajiwa kupigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, ambapo wenyeji wataingia uwanjani wakijiamini kutokana na rekodi ya kutopoteza mechi yoyote hadi sasa, huku pia wakiwa na wastani mzuri wa kuvuna matokeo bora dimbani hapo.

Kocha huyo raia wa Uholanzi, aliliambia BINGWA kuwa maandalizi mazuri yanazaa matunda bora jambo ambalo wanaendelea kujivunia, huku akidai pia nidhamu na uwajibikaji kwa wachezaji ni silaha muhimu kwao.

“Kila mchezo lazima uwe na tahadhari na namna ya kujipanga kuvuna pointi tatu, jambo jema ni kwamba, wachezaji wanayo ari ya kupambana na kila adui na hicho ndicho tunatarajia kukifanya kesho (leo),” alisema.

Katika hatua nyingine, Ofisa Habari wa klabu ya Azam, Jaffar Idd, alieleza kuwa wamemrejesha kikosini mchezaji wao raia wa Ghana, Daniel Amoah, katika kipindi hiki cha usajili wa dirisha dogo.

Alifafanua kuwa Amoah alikuwa nje ya uwanja kwa kipindi cha miezi tisa kutokana na majeraha hivyo hakusajiliwa katika usajili wa dirisha kubwa.

“Amoah tulimkosa kwa miezi tisa lakini sasa amepona na ameanza mazoezi, jina lake tumelituma TFF kama usajili wetu mwingine wa kimataifa katika dirisha dogo,” alisema.

Aidha, alieleza kwamba bado wanasubiri Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) ya mshambuliaji wao, Obrey Chirwa, baada ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuandika barua kwa Chama cha Soka nchini Misri kuomba hati hiyo.

Azam wamejikusanyia pointi 33 zinazowawezesha kushika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu, wakiwa na tofauti ya pointi mbili nyuma ya vinara Yanga waliovuna pointi 35.

Kwa upande wa kocha msaidizi wa Stand United, Athuman Bilali ‘Bilo’, alisema watamenyana na Azam bila ya kuwepo kwa wachezaji wao wawili tegemeo, Alex Kitenge na Blaise Bigirimana, ambao wanakabiliwa na sababu tofauti.

Share.

About Author

Leave A Reply