Wednesday, August 21

AUSSEMS ‘BYE BYE’ SIMBA

0


NA MWAMVITA MTANDA

KOCHA Mkuu wa Simba, Patrick Aussems, yupo mbioni
kuachana na timu hiyo, huku uongozi wa Wekundu wa Msimbazi hao ukiwa umeanza mchakato
wa kumsaka mbadala wake.

Habari za uhakika zilizolifikia BINGWA wikiendi
iliyopita, zinasema kuwa kocha huyo amefikia uamuzi huo kutokana na
kutoridhishwa na mshahara anaolipwa.

Imedaiwa kuwa kocha huyo raia wa Ubelgiji, analipwa
kitita cha Dola za Marekani 10,000 (takribani Sh mil 22.9) kwa mwezi.

Hayo yanatokea wakati Aussems akiwa ameipa mafanikio
makubwa Simba kwa kuifikisha robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, huku pia
ikiwa na nafasi kubwa ya kutetea ubingwa wao wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Kocha huyo alitua Simba mwanzoni mwa msimu huu baada
ya kutimuliwa kwa Mfaransa, Pierre Lichantre, aliyeipa timu hiyo ubingwa wa
Bara msimu uliopita.

Juu ya habari hizo za kuondoka kwake Simba, BINGWA
jana lilizungumza na Aussems aliyekiri hilo, japo aliweka wazi kuendelea kuwapo
Msimbazi iwapo ataongezewa mshahara.

“Naweza kusema katika timu ambazo nimefanya kazi kwa
amani, lakini kwa presha kubwa katika klabu za Afrika, ni Simba. Natamani
kuendelea kuwepo, lakini kama uongozi utaniangalia tena kivingine, japokuwa ninaisaidia
timu, lakini na mimi naangalia masilahi yangu,” alisema Aussems.

Mbelgiji huyo ambaye kibarua chake Simba kinafikia
ukingoni mwezi ujao, alisema amepokea ofa nyingi hasa baada ya kuifikisha timu
hiyo robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini bado hajakubaliana na
klabu yoyote akisubiria kauli ya mabosi wake wa sasa kama bado wanamhitaji.

Hata hivyo, Aussems alisema kuwa inahitaji uvumilivu
wa hali ya juu kufundisha timu za Afrika kwani asilimia kubwa uongozi wake una
tabia zinazofanana za kutowaamini makocha hata kama timu inafanya vizuri.

Juu ya tetesi za kusakwa kwa mbadala wa Mbelgiji
huyo, imedaiwa kuwa jukumu hilo amekabidhiwa meneja wa mshambuliaji wa Simba,
Meddie Kagere, anayefahamika kwa jina la Patrick Kagumba ‘Super Manager’.

BINGWA lilifanya jitihada za kumsaka meneja huyo ili
kufahamu ukweli kuhusiana na tetesi hizo ambapo alikiri hilo akisema tayari
yupo katika mazungumzo na makocha kadhaa wakubwa Afrika.

“Nilipigiwa simu na uongozi wa Simba kuwa wanahitaji
kocha, hivyo katika harakati zangu, kuna makocha nimeona watawafaa, hivyo nipo
katika mazungumzo nao,” alisema.

Kikosi cha Simba leo kitashuka dimbani kuvaana na
Singida United katika mchezo utakaopigwa Uwanja wa Namfua, Singida ambao
Wekundu wa Msimbazi hao wanahitaji pointi moja tu ili kutwaa ubingwa wa Ligi
Kuu Bara.

Share.

About Author

Leave A Reply